Unajua Umuhimu wa kuwafundisha watoto elimu ya kiroho?

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Wazazi, walezi na jamii kwa ujumla wana wasiwasi kuhusu kuwalea watoto katika ulimwengu wa leo unaokabiliwa na changamoto za utandawazi. Hata hivyo, hatuna sababu ya kuwa na wasiwasi kama tukifuata ushauri huu: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha hata atakapokuwa mzee”(Mithali 22:6). Watoto waendeleapo kukua, wanahitaji ‘njia’, yaani kanuni wanazopaswa kuzifuata. Kanuni hizi haziji zenyewe bali zinapatikana kwa kuwapatia watoto elimu itakayokuwa mwongozo katika maisha yao yote.  Elimu hiyo ni elimu ya kiroho ambayo inapaswa ianzie nyumbani na kuendelezwa kanisani na katika shule za Kikristo.

Watoto nao wanahitaji elimu ya kiroho?

Ni muhimu sana kuwapatia watoto elimu ya kiroho mapema iwezekanavyo badala ya kusubiri wawe watu wazima. Watoto wasipopewa elimu bora ya kiroho kwa kudhani kwamba wataipata wakiwa watu wazima ni sawa na kujenga nyumba yenye msingi usio imara halafu ukajenga kuta na paa imara. Ni dhahiri, nyumba hiyo haitakuwa imara. Vivyo hivyo, tusipojenga msingi bora wa kiroho kwa watoto, tusitegemee kuwa na watu wazima walio imara kiroho. Ili kuwajengea msingi imara wa kiroho, inatubidi kuwapatia elimu bora ya kiroho.

Kuna haja kubwa ya kuwapatia watoto elimu kiroho kwa sababu kuna tofauti kubwa kati ya watoto na watu wazima  katika kujifunza. Kwanza, watoto ni wepesi kupokea mafundisho ya aina yoyote. Pili, watoto wana uwezo mkubwa wa kukumbuka mambo wanayofundishwa ukilinganisha na watu wazima. Tatu, mioyo ya watoto inaweza kupokea kwa urahisi Neno la Mungu na kuliamini na hivyo wanaweza kuwa Wakristo kwa urahisi kuliko watu wazima.

Utafiti uliofanywa nchini Marekani na kuchapishwa katika kitabu kiitwacho Transforming Children into spiritual Champions cha mwaka 2003,unaonesha uhusiano kati ya umri wa mtoto na uwezekano wa kumpokea Yesu. Katika utafiti huo uliofanywa taasisi maarufu katika masuala yanayohusiana na malezi ya watoto ya kiroho iitwayo Barna Research Institute, ulionesha kuwa watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 12 walikuwa na uwezekano wa asilimia 32 wa kumpokea Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yao. Watoto wenye umri wa miaka 13 hadi 18 walionesha uwezekano wa asilimia 4. Watoto wenye umri wa miaka 19 na kuendelea walikuwa na uwezekano wa asilimia 6 wa kumpokea Yesu. Kwa mujibu wa  utafiti huu, ni dhahiri kwamba watoto wadogo wana uwezekano mkubwa zaidi wa kumpokea Yesu ukilinganisha na watu wazima. Kwa maneno mengine, kwa kadri umri unavyozidi kuwa mkubwa uwezekano wa kumpokea Yesu unakuwa mdogo. Hii inamaanisha kuwa tunapaswa kuwapatia elimu bora ya kiroho watoto wetu wangali na umri mdogo maana katika umri huu ndipo tunapoweza kuwajengea msingi imara wa imani.

Nini kifanyike ili kuwapatia watoto wetu elimu bora ya kiroho?

Kwa kuzingatia kuwa elimu ya kiroho inaanzia nyumbani na kuendelezwa kanisani na shuleni, mambo matatu yanaweza kufanyika. Kwanza, kila mzazi na mlezi ajifunze  njia bora za kurithisha imani yake kwa watoto wake. Pili, walimu wanaofundisha somo la Dini shuleni wawe na uwezo wa kufundisha vizuri somo hilo ili waweze kuwaelekeza watoto kwa Yesu. Tatu, walimu na wahubiri wa watoto makanisani wawe na maarifa na mbinu bora kwa ajili ya kuwapatia watoto elimu bora ya kiroho. Ili kufanikisha mambo haya matatu, walimu na walezi na wadau wa watoto kwa ujumla wanahitaji elimu juu ya namna ya kufundisha na kuhubiri watoto walio katika umri mbalimbali ili waweze kufundisha na kuhubiri kwa ufanisi watoto nyumbani, shuleni na kanisani.

Je , kuna tofauti ya ufundishaji wa elimu ya kawaida na elimu ya kiroho?

Ufundishaji wa masuala ya imani unafanana kwa namna fulani na ufundishaji wa taaluma ya kawaida kwa sababu ufundishaji wa aina zote unagusa akili ya mtoto. Lakini kwa namna nyingine, kufundisha masuala ya imani ni tofauti na kufundisha masomo ya kawaida kwa kuwa ufundishaji wa masuala ya imani unalenga kuwafanya watoto wampende Yesu, kitu ambacho hakifundishwi katika masomo ya kawaida. Kumpenda Yesu si suala linalohusisha akili tu bali moyo pia. Ni suala linalohusisha mabadiliko katika maisha ya mtoto kutoka ndani ya moyo na kumfanya ajitoe kikamilifu kumfuata Yesu. Ni Roho Mtakatifu ndiye anayebadilisha moyo na akili ya mtoto. Kwa hiyo, si sahihi kudhani kuwa maarifa na ujuzi wetu kuhusu watoto, mtaala mzuri wa kufundishia na mbinu bora za ufundishaji vinatosha kuwafanya watoto wakue kiroho. Imani na wokovu ni karama kutoka kwa Mungu na Mungu huvitoa kwa kadri ya utayari wetu wa kuvipokea.

Walimu na wote wanaoshughulika na watoto wanapaswa kutegemea kikamilifu kazi ya Roho Mtakatifu katika kumpeleka mtoto kwa Yesu maana Roho Mtakatifu  ni muhimu sana katika ukuaji wa kiroho. Hata hivyo, hii haimanishi kwamba, wasijibidishe kujua namna watoto wanavyokua kiroho na namna ya kuwasaidia kukua kiroho. Ni muhimu kufahamu haya na kuyafanyia kazi. Kwa hiyo, kazi ya wazazi, walimu na wahubiri ni kujenga mazingira mazuri kwa ajili ya Roho Mtakatifu kufanya kazi yake lakini hawawezi kufanya kazi ya Roho Mtakatifu na Roho Mtakatifu hawezi kufanya kazi yao. Wao wana sehemu yao na Roho Mtakatifu ana sehemu yake. Elimu juu ya namna ya kufundisha na kuhubiri watoto itawasaidia wazazi, walimu na wahubiri kufanya sehemu yao lakini haiwezi kuwasaidia kufanya sehemu ya Roho Mtakatifu. Ninaamini Mungu yuko tayari kushirikiana nasi tunapofanya sehemu yetu katika kuwaandaa watoto kwa ajili ya maisha ya hapa duniani na pia kwa ajili ya maisha ya milele.

Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu namna ya kufundisha na kuhubiri watoto ? Basi pata kitabu kizuri juu ya Ustadi wa Kuhubiri na Kufundisha Watoto. Kitabu hiki kitakupatia mbinu zote kwa ajili ya kufundisha na kuhubiri watoto wa umri tofauti tofauti. Kupata kitabu hiki  na vitabu vingine unaweza kuwasiliana nasi namba za simu; +255-754-405582 (Simeon Shimbe), +255-714-606278 (DevothaShimbe), Email: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mpango wa Mungu kuhusu mafanikio yako? Basi jiunge na mtandao wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio kwa kunyonyeza hapa ili uweze kupata makala kwenye email yako. Mtandao huu umeanzishwa kwa kusudi la kuwapatia maarifa ya msingi kuhusu masuala ya fedha, biashara, mahusiano (uchumba, ndoa na malezi ya watoto) na mambo ya kiroho. Katika mtandao huu utapata maarifa katika maeneo ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano, malezi ya watoto na mambo ya kiroho

About Devotha Shimbe

Devotha Shimbe ni Mwalimu na mwanasaikolojia. Amepata pia mafunzo ya Theolojia. Devotha amejitoa kumtumikia Mungu katika maisha yake yote na amekuwa akifundisha na kutoa semina mbalimbali kuhusu mahusiano na maisha ya kiroho kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *