Hivi Ndivyo Unavyoweza Kufundisha na Kuhubiri Kwa Watoto wa Siku Hizi

Rafiki yangu mpendwa katika Krsito,

Tunaishi katika karne ambayo imepewa jina la “Karne ya Sayansi na Teknolojia”. Maendeleo makubwa ya Sayansi na teknolojia yamesababisha mabadiliko karibu katika nyanja zote za maisha ya mwanadamu na mabadiliko hayo yanatokea kwa kasi sana kuliko karne zilizopita. Maendeleo tunayoyashuhudia si kitu cha kushangaza kwa wasomaji wa Biblia maana ni unabii unaolezwa katika kitabu cha Danieli 12:4: “Lakini wewe, Ee Danieli, yafunge maneno haya, ukakitie muhuri kitabu, hata wakati wa mwisho; wengi wataenda mbio huko na huko, na maarifa yataongezeka”.

Mabadiliko yanayotokana na maendeleo ya Sayansi na teknolojia yamewagusa watoto pia na yamewafanya wawe tofauti. Watoto wa siku hizi wanaishi katika mazingira tofauti na yale waliyoishi wazazi wao na ni tofauti hata na ya watoto walioishi miaka kumi tu iliyopita.  Ukweli huu unaweza kujidhihirisha tukijaribu kupiga picha miaka kumi iliyopita na kulinganisha tofauti iliyopo, kwa mfano, katika eneo moja tu la teknolojia ya habari na mawasiliano. Ni dhahiri kwamba kuna mabadiliko makubwa sana katika eneo hili. Kila mzazi, mwalimu, mhubiri na mtu yeyote anayeshughulika na watoto anapaswa kuelewa mabadiliko hayo ili awasaidie watoto kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na mabadiliko hayo na pia aweze kutafuta njia za kisasa za kuwasaidia kumfahamu Yesu.

.

Ukiachilia mbali mabadiliko katika sayansi na teknolojia, kuna mabadiliko mengine mengi ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaathiri ufundishaji wa watoto masomo ya kawaida na masomo ya kiroho. Leo nitaangazia eneo moja la mabadiliko hayo na namna mwalimu au mhubiri wa watoto anavyopaswa kuzingatia hali hiyo katika kufundisha au kuhubiri watoto. Mabadiliko nitakayoangazia ni mabadiliko katika familia.

Familia nyingi za siku hizi hasa za mijini zina idadi ndogo ya watoto pamoja na wanafamilia wengine. Ule utamaduni wa Kiafrika wa kuzaa idadi kubwa ya watoto na kuishi na ndugu, jamaa na marafiki unaonekana kupitwa na wakati na kwa kiasi umeanza kupungua. Katika mazingira haya, watoto wa siku hizi hawana mwingiliano wa karibu baina yao na watu wengine zaidi ya wazazi wao na ndugu wachache wa karibu. Kutokana na wazazi wengi kuwa na shughuli nyingi na kutokuwa na muda wa kukaa na watoto wao, matokeo yake watoto hujikuta wakiwa huru lakini bila mtu wa karibu anayejali mambo yao na kuwaelekeza katika maadili yanayofaa. Vilevile, familia nyingi huhamahama kimakazi kutokana na kuhamishwa kikazi au wao wenyewe kuamua kuhamishia shughuli zao za kujipatia riziki sehemu nyingine. Vilevile, baadhi ya watoto wanasoma shule za bweni wakiwa na umri mdogo zaidi kuliko miaka ya nyuma. Siku hizi si ajabu kukuta mtoto wa chekechea akiwa katika shule ya bweni. Yote haya huwafanya watoto wasijenge uhusiano wa karibu sana na watu wengine wakiwemo hata wazazi wao. Kwa hiyo, watoto wa siku hizi ni watoto wapweke kuliko watoto wa zamani.

Mabadiliko haya katika familia, yamewafanya watoto wengi hasa wa mijini wawe na ombwe la mahusiano. Kwa hiyo, watoto walio katika mazingira haya, wanahitaji mtu wa kuwapenda, kuwajali na kuwa karibu nao. Ukiacha wazazi, mtu mwingine anayetegemewa kuwa karibu nao ni mwalimu au mhubiri wao. Kama mwalimu au mhubiri atafanya hivyo, bila shaka watoto hao watampenda na hawataishia kumpenda yeye tu bali watampenda na Mungu wake ambaye ndiye Mungu wao pia.

Wahubiri na walimu wanaofundisha mambo ya kiroho, ni lazima watafute njia zitakazowafanya kuwa na uhusiano wa karibu na wanafunzi wao. Ni lazima watambue kuwa Mungu huonyesha upendo wake kwa watoto kupitia kwa walimu hawa. Mtoto akigundua kuwa mwalimu wake anampenda na anamjali, atakuwa huru kumueleza matatizo yake yote yakiwemo matatizo binafsi na pia atakuwa huru kuuliza maswali kwa mwalimu bila woga. Kwa namna hii, ombwe la mahusiano na wazazi na ndugu, kama lipo, litapungua kama siyo kuzibwa kabisa.

Walimu wa masomo ya kiroho na wahubiri wa watoto wanapaswa kujifunza kwa Mwalimu Mkuu Yesu Kristo namna alivyokuwa na mahusiano ya karibu na wanafunzi wake. Hata alipokuwa anaongea na makutano, kila mtu katika mkutano alihisi kuwa Yesu alikuwa anafahamu matatizo binafsi ya mtu huyo.  Yesu alitumia kila njia kuwafikia watu ikiwemo njia ya ana kwa ana na mtu mmoja mmoja. Visa vya Nikodemo (Yohana sura ya 3), Mgonjwa katika birika la Bethzatha (Yohana 5:1-9) na Mwanamke Msamaria (Yohana sura ya 4) ni mifano ya namna Yesu alivyoweza kujali mahitaji ya mtu mmoja mmoja. Mwalimu wa leo naye anapaswa kujali mahitaji ya mwanafunzi mmoja mmoja. Ili kufanya hivyo, ni lazima atoe muda wa kutosha kumhudumia mtoto mmoja mmoja ili kujenga mahusiano ya karibu naye.

Mzazi, mwalimu, mhubiri na mtu mwingine yeyote anayeshughulika na watoto anapaswa kuwa rafiki wa kila mtoto ili aweze kufanikiwa kuwasaidia watoto kumfahamu Yesu vizuri. Mwandishi wa vitabu vya kiroho Ellen G.White katika kitabu chake cha Adventist Home, uk. 43 anashauri yafuatayo “Jiweke katika mahitaji ya watoto na wafanye wakupende. Ni lazima uteke matamanio yao, kama unataka kuwavuta kuelekea ukweli wa dini katika mioyo yao”. Kama tutazingatia ushauri huu, bila shaka ufundishaji wetu utaleta tofauti kubwa kwa watoto.

Rafiki yangu mpendwa, hapa nimekushirikisha moja kati ya mabadiliko mengi yaliyotokea na kufanya ufundishaji wa watoto wa siku hizi kuwa tofauti na nini cha kufanya unapofundisha watoto ili uweze kuendana na mabadiliko hali hiyo. Je, unapenda kufahamu mabadiliko mengine na changamoto  zingine pamoja na nini cha kufanya ili uweze kufundisha watoto mambo ya kiroho kwa ufanisi. Je, unapenda kujifunza zaidi kuhusu namna ya kufundisha au kuhubiri watoto wa siku hizi? Basi pata kitabu juu ya Ustadi wa Kuhubiri na Kufundisha Watoto. Kitabu hiki kitakupatia mbinu zote kwa ajili ya kufundisha na kuhubiri watoto wa umri tofauti tofauti. Kupata kitabu hiki  na vitabu vingine unaweza kuwasiliana nasi namba za simu; +255-754-405582 (Simeon Shimbe), +255-714-606278 (Devotha Shimbe), Email: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mpango wa Mungu kuhusu mafanikio yako? Basi jiunge na mtandao wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio kwa kubonyeza kiungo hiki; www.mkristomafanikio.co.tz Mtandao huu umeanzishwa kwa kusudi la kuwapatia maarifa ya msingi kuhusu masuala ya fedha, biashara, mahusiano (uchumba, ndoa na malezi ya watoto) na mambo ya kiroho. Katika mtandao huu utapata maarifa katika maeneo ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano, malezi ya watoto na mambo ya kiroho.

About Devotha Shimbe

Devotha Shimbe ni Mwalimu na mwanasaikolojia. Amepata pia mafunzo ya Theolojia. Devotha amejitoa kumtumikia Mungu katika maisha yake yote na amekuwa akifundisha na kutoa semina mbalimbali kuhusu mahusiano na maisha ya kiroho kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *