Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Tafiti zilizofanyika katika nchi mbalimbali zinaonesha kuwa mojawapo ya mambo yanayooongoza kusababisha migogoro na kuvunjika kwa ndoa ni fedha. Kwa mfano, Mwaka 2017, kampuni moja ya kimarekani inayojishughulisha na utafiti na utoaji wa elimu ya masuala ya fedha itwayo Ramsey solutions, ilifanya utafiti uliowahusisha watu 1072 nchini humo. Lengo la utafiti huo lilikuwa kupata uelewa kuhusu mtazamo na tabia za watu kuhusiana na usimamizi wa fedha binafsi na namna ambavyo masuala ya fedha yana athari katika mahusiano ya ndoa. Matokeo ya utafiti huo yalionesha kuwa wanandoa waliokuwa na madeni makubwa walikuwa na ugomvi wa mara kwa mara kuhusu fedha. Karibu nusu ya wanandoa waliokuwa na madeni makubwa yaliyotokana na mikopo walisema kuwa pesa ndicho chanzo kikubwa cha ugomvi baina yao. Wale waliokuwa na ndoa zisizo na matatizo, walibainika kuwa walikuwa na tabia ya kujadiliana na kukubaliana mara kwa mara kuhusu masuala ya fedha ukilinganisha na wale ambao walikuwa na matatizo katika ndoa.
Matokeo zaidi ya utafiti wa Ramsey Solutions yanaoenesha kuwa theluthi moja (1/3) ya wanandoa waliosema walikuwa na ugomvi kuhusu masuala ya fedha, walikuwa wakifanya manunuzi ya vitu bila kuwashirikisha wenzi wao kwa hofu kuwa ikiwa watawashirikisha wasingeweza kukubaliana na manunuzi hayo. Utafiti huo ulibaini pia kuwa asilimia 94 ya wanandoa wasio na migogoro, huwa wanajadiliana kuhusu fedha ukilinganisha na asilimi 45 ya wana ndoa ambao walisema kuwa ndoa zao zina migogoro. Asilimia 84 ya wanandoa ambao hawana migogoro katika ndoa walisema kuwa huwa wanakaa na kupanga pamoja mipango yao inayohusiana na fedha. Asilimia 47 ya wana ndoa wenye mikopo walieleza kuwa madeni yao yanawasababishia wasiwasi na msongo wa mawazo.
Utafiti mwingine uliofanywa mwaka 2015 na taasisi ya Suntrust ya Marekani, unaonesha kuwa changamoto za kifedha zinaongoza kusababisha migogoro katika ndoa. Kwa upande wake taasisi ya Institute for divorce imefanya utafiti na kubaini kuwa masuala ya kifedha yanachangiia kuvunjika kwa ndoa kwa asilimi 22%.
Utafiti mwingne ulifanyika katika nchi jirani ya Zambia mwaka 2018 kuhusu mambo yanayoongoza kusababisha migogoro ya ndoa. Utafiti huo uliofanywa na Chuo kikuu cha Rusangu cha nchini humo,ulibainisha kuwa fedha ni sababu ya kwanza kati ya sabau 10 zilizobainishwa na utafiti huo kuwa ni vyanzo vya migogoro ya ndoa nchini Zambia.
Kutokana na tafiti hizi, ni dhahiri kuwa masuala ya fedha yanachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha au kubomoa mahusiano katika ndoa na familia. Hata hivyo, ni vizuri ieleweke kuwa kinachosababisha migogoro ya ndoa siyo kukosa fedha wala siyo kuwa na fedha nyingi. Japo ni kweli kuwa wapo wanandoa walioachana kwa sababu ya mtikisiko wa kifedha na wengine wameachana baada ya kuwa na fedha nyingi, lakini ni kweli pia kuwa kuna watu wengi wana ndoa zisizo na migogoro wakati wana maisha yenye changamoto kubwa ya kifedha na vilevile wapo wanaoishi maisha mazuri ya ndoa wakati wana fedha nyingi.
Kwa kuwa migogoro ya ndoa inawapata watu wa aina zote, maskini na matajiri, basi hatuwezi kusema kuwa migogoro ya kifedha katika ndoa inasababishwa na ama kuwa na fedha nyingi au kukosa fedha. Ukweli ni kwamba sababu kubwa inayosababisha migogoro ya kifedha katika ndoa na familia ni kukosekana kwa elimu ya msingi ya usimamizi wa fedha binafsi. Unaweza ukawa na fedha nyingi lakini kwa sababu hauna maarifa juu ya usimamizi wa fedha, ukajikuta unaingia katika migogoro ya kifedha. Lakini kama una maarifa ya kutosha katika kusimamia fedha binafsi, utapunguza kwa kiasi kikubwa migogoro ya kifedha katika ndoa bila kujali una fedha nyingi au kidogo.
Kimsingi, fedha ni sehemu muhimu ya maisha ya hapa duniani. Bila fedha mambo mengi yatakwama ikiwemo utimizaji wa wajibu ambao tumepewa na Neno la Mungu kuhusu utunzaji wa familia. Kwa sababu maswala ya fedha ni muhimu katika maisha, kupitia hekima yake isiyo na kipimo, Mungu ametupatia mafundisho muhimu katika Neno lake ambayo mkristo anapaswa kuyafuata na pia akatupatia kanuni muhimu ambazo zitatusaidia kufanikiwa katika swala hili. Kwa sababu hiyo kuna kila sababu ya kuwa na uelewa sahihi wa namna ya kupata fedha, kuitunza na kuizalisha kwa kutumia kanuni sahini kibiblia na kiuchumi ili kuwa na maisha bora hapa duniani wakati tunajiandaa kwenda kufurahia maisha mazuri mbinguni. Endelea kufuatilia makala katika mtandao huu ili uweze kupata maarifa hayo muhmu kwa ajili ya ustawi wako binafsi na wa familia yako.
Je, unataka kujifuunza zaidi kuhusu masuala ya fedha katika ndoa?
Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu biashara na mafanikio kwa ujumla ? Basi tafuta kitabu chetu kinachoitwa Siri za Mafanikio ya kifedha katika Ndoa na Familia. Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com