Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Kuna mitazamo tofauti miongoni mwa wakristo kuhusu suala la bima. Wapo wanaounga mkono kukata bima ya aina yoyote lakini wapo wengine ambao wana mtazamo kuwa kukata bima kunaonesha upungufu wa imani juu ya uweza wa Mungu. Kwa sababu ya mgawanyiko huu wa mtazamo, tutajadili kidogo suala hili.
Kwanza ieleweke kuwa, bima haijatajwa moja kwa moja katika biblia. Lakini kutotajwa kwa kitu chochote katika biblia haimanishi kuwa hakikubaliki na pia haimanishi kuwa kinakubalika. Kwa kuwa bima haijatajwa moja kwa moja katika biblia, ni lazima tutumie kanuni na mafundisho ya jumla au mahususi ya maandiko. Kama kuna fundisho fulani la maandiko ambalo linapingana na kitu hicho basi tunaweza kuikataa. Lakini kama haipingani na kanuni yoyote basi hatuna sababu ya kulikataa. Hebu tuangalie kanuni zinazoweza kutuongoza katika kukataa au kukubali bima ya aian yoyote.
Wanaopinga kukata bima hutumia mafungu kama vile “Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini ; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi ? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia ? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake” (Mathayo 6:25-34). Fungu jingine ni “Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona (Mathayo 10:37-39).
Kwa kutumia mafungu tajwa hapo juu, watu wanaopinga kujiunga na bima wanadai kuwa tunapaswa kumtegemea Mungu kikamilifu na siyo vitu vingine kama vile bima. Ni kweli kabisa, Mungu ana uwezo wa kutuepusha na majanga ya aina yoyote na hivyo tunapaswa kutegemea uwezo wa Mungu kwa asilimia 100. Lakini ni ukweli ulio wazi ambao unathibitishwa na maandiko na uzoefu wetu katika maisha kuwa Mungu pia huruhusu tupitie changamoto mbalimbali ikiwemo majanga. Mifano ni mingi katika biblia lakini mfano unaofahamika kwa wengi ni Ayubu ambaye licha ya kuwa mkamilifu, mwelekevu na mcha Mungu (Ayubu 1:1), alipitia changamoto nyingi zikiwemo kupoteza watoto wake wote na mali zake zote (Ayubu suara ya 1) na yeye mwenye kupata ugonjwa mbaya (Ayubu 2:7). Ukiacha masimulizi ya biblia, tujiulize leo, je ni kweli kwamba majanga hayawapati wakristo ? Je, wakristo hawapati ajali, magonjwa mabaya, misiba na majanga mengine. Jibu, liko wazi kuwa wakristo wa leo na wa zamani leo wanapata majanga kama wanavyopata wasio wakristo. Sasa kama wanapata majanga, kuna ubaya gani kuandaa mpango ambao utasaidia kuepuka au kupunguza madhara ya majanga haya ?
Kujiunga na bima siyo ukosefu na imani bali ni kutambua kwa vitendo kuwa tuko katika dunia ya dhambi na majanga ni sehemu ya maisha katika dunia hii. Kwa kuwa tukiugua huwa tunaenda kwa madaktari kupata tiba, kwa nini tutumie gharama zetu kufanya hivyo badala ya kukata bima. Kama vyombo vyetu vya usafiri vikipata ajali huwa tunaenda gereji kutengeneza, kwa nini tutumie gharama zetu kufanya hivyo badala ya kutumia bima ? Kama tumeshuhudia wakristo wenzetu wakipata ajali na kuwa walemavu na hivyo kushindwa kufanya kazi na pengine kushindwa kuhudumia familia zao, tunajuaje kwamba majanga hayo hayawezi kutupata sisi ? Je, kwa ni tusichukue tahadhali ili mambo hayo yakitukuta tusiathirike sisi wenyewe na familia zetu ?
Biblia inasema kuwa tuna wajibu wa kutunza familia zetu. “Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini (1 Timotheo 5:8). Hivyo, kukata bima ni namna ya kutunza familia zetu. Bima itasaidia familia yako kupata matibabu wanapougua, kupata fidia ikiwa wewe utafariki na pia itasaidia kuepuka au kupunguza athari za majanga mbalimbali kama vile moto, ajali na kadhalika. Bima pia ni njia ya kudhibiti matumizi ya fedha maana badala ya kutumia fedha zako kurekebisha athari za majanga, bima ndiyo inatumika na fedha yako inatumika kuhudumia mahitaji mengine ya familia.
Biblia inasisitiza kuwa tunapaswa kutii mamlaka iliyo kuu, kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu ; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu (Warumi 13:1). Hivyo, kama tunatakiwa na sheria kuwa na bima, hatuna budi kuwa nayo. Kwa kuwa baadhi ya bima ni za lazima kukata kwa mujibu wa sheria na kama kwa kuwa kufanya hivyo hatukiuki maelekezo yoyote ya Mungu, basi hatuna budi kutii sheria hii bila shurti. Kutokata bima ni kuvunja sheria ya nchi na pia ni kuvunja maelekezo ya Mungu ya kutii mamlaka.
Kujipanga kwa ajili ya mambo yajayo ni jambo linalopatana na biblia. Kisa cha Yusufu na mipango ya hekima yake iliokoa taifa la Misri lakini pia na watu wa Israeli na ukoo wa Kristo (Mwanzo 41). Kama wakristo, tunapaswa kuiga kanuni hii ya Yusufu katika maisha ya leo na kuhakikisha kila wakati tumeweka mipango kwa ajili ya maisha yetu ya kesho. Kukata bima ni mojawapo ya njia ambazo tunaweza kujipanga kwa ajili ya maisha ya kesho.
Je, unataka kujifuunza zaidi kuhusu masuala ya fedha katika ndoa na familia?
Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu biashara na mafanikio kwa ujumla ? Basi tafuta kitabu chetu kinachoitwa Siri za Mafanikio ya kifedha katika Ndoa na Familia. Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com
Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mapngo wa Mungu kuhusu mafanikio yako?
Basi jiunge na mtandao huu kwa kubonyeza hapa. Mtandao huu umeanzishwa kwa kusudi la kuwapatia maarifa ya msingi katika nyanja mbalimbali za maisha. Katika mtandao huu utapata maarifa katika maeneo ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano, malezi ya watoto na mambo mengine ya kiroho.