Hivi Ndivyo Mnavyoweza kusimamia Fedha katika Ndoa Yenu

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Mtu mmoja aliwahi kusema “kila ndoa ina rangi yake” akiwa na maana kuwa ndoa hazifanani katika namna wanandoa wanavyoendesha mambo yao. Moja ya mambo ambayo kuna tofauti kubwa kati ya ndoa moja na nyingine ni namna wanandoa wanavyosimamia pesa zao.

Kuna aina mbalimbali za wanandoa kuhusiana na namna wanavyosimamia masuala ya fedha. Zifuatazo ni ni baadhi ya aina hizo:

  • Wanaounganisha vipato vyao
  • Wanaounganisha sehemu ya kipato
  • Wasiounganisha kabisa kipato
  • Wanaoshirikiana majukumu ya pamoja kwa uwiano wa vipato vyao
  • Wanaogawana majukumu ya kifamilia
  • Mwanandoa mmoja anamlipa posho mwenzi wake
  • Wanaoishi kwa kipato cha mwenzi mmoja

Njia ipi ni bora kuliko zingine?

Pengine swali la kujiuliza ni hili, kati ya njia za kusimamia fedha katika ndoa zilizotajwa hapo, ni njia ipi ni bora kuliko zote? ibu langu kwa swali hili ni fupi tu: hakuna njia inayoweza kuwafaa wanandoa wote. Njia moja inaweza kuwafaa wanandoa fulani na isiwafae kabisa wana ndoa wengine kutokana na sababu mbalimbali. Njia gani wanandoa wanachagua inategemeana na mambo mengi kama vile kipato cha wanandoa, mitazamo yao, utamaduni, tabia zao kuhusiana na matumizi ya fedha na vipaumbele vya kila mmoja.

Kuna msemo wa kiingereza kuhusiana na masuala ya fedha binafsi unasema “personal finance is personal”. Msemo huu una maana kuwa fedha binafsi ni suala binafsi. Hivyo, namna mtu anavyosimamia fedha zake anaamua mwenyewe na si lazima afanye kama wengine. Pamoja na ukweli kuwa kuna kanuni za usimamizi bora wa fedha binafsi, bado uzingatiaji wake unatofautiana kati ya mtu na mtu kutegemeana na hali ya mtu huyo. Kabla ya kuamua ni njia gani mnatumia, yapasa mjadiliane na kukubaliana na mwenzi wako. Kama hamna uhakika ni njia ipi inaweza kuwafaa, mnaweza kujaribu njia kadhaa ili kuona uzuri na changamoto zake kisha ndipo muamue njia inayowafaa.

Wanandoa wanapaswa kuwa “Kuwa uchi” kwenye suala la pesa

Katika njia yoyote ile utakayoamua kusimamia fedha na mwenzi wako, kama wewe ni mkristo unapaswa uchague njia ambayo itawafanya muwe kitu kimoja badala ya kuwafanya muwe watu wawili. Katika kitabu cha Mwanzo 2:24-25, biblia inasema “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu na mkewe, wala hawakuona haya”.

Unapokuwa katika mahusiano ya ndoa, kipaumbele chako ni katika mambo yenu (wewe na mwenzi wako) na siyo mambo yako binafsi. Mnapokuwa katika mahusiano ya ndoa mnakuwa timu moja na hivyo mambo yenu yote mnapanga pamoja. Lakini, kama kila mmoja anapanga mambo yake kivyake, mnakuwa pamoja lakini siyo wamoja na hivyo siyo mwili mmoja. 

Kama ambavyo Adamu na Hawa walikuwa uchi na hawakuona haya (Mwanzo 2:25), wanandao wa leo nao huwa hawaoni haya kuwa uchi wakiwa pamoja. Katika 1 Wakorintho 7:4, wakristo wanaambiwa kuwa “Mke hana amri juu ya mwili wake bali mumewe, vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Uchi wa wanandoa unaotajwa katika Mwanzo 2:25 haupaswi kuishia kwenye uchi wa kimwili tu bali wanapaswa kuwa uchi kwa kila jambo, yaani uwazi katika kila jambo.

Wenzi wanapaswa kufahamu kila kitu cha mwenzake yakiwemo masuala ya pesa. Ni kitu cha ajabu kuwa uchi wa mwili kwa mwenzi wake ambao una thamani kubwa na kuficha fedha ambayo thamani yake ni ndogo kuliko mwili. Hakuna kitu kilicho cha thamani kuliko mwili. Thamani ya mwili haiwezi kulinganishwa na pesa. Pesa, hata kama ni nyingi kiasi gani, bado mwili una thamani kubwa kuliko pesa hiyo.

Wanandoa wanapoweka wazi vipato vyao na kupanga mipango ya fedha pamoja wanakuwa uchi katika masuala ya fedha. Huo ndio mpango wa Mungu. Mpango tofauti na huo ni kujitafutia matatizo. Kama kuna sababu ya msingi, inayomfanya mwanandoa mmoja asiweke wazi mapato yake na mipango yake kuhusu fedha, sababu hiyo inabidi ijadiliwe na itafutiwe ufumbuzi kwa ajili ya afya ya ndoa.

Wanandoa ambao wanakubaliana na mpango wa Mungu wa kuwa mwili mmoja  na kuwa uchi wanapaswa kuwa na kawaida ya kukaa chini na kujadiliana kwa pamoja mipango yao ya kifedha, vipaumbele vyao, changamoto zao na namna ya kuzitatua. Wanandoa wa aina hii wanategemewa kuwa na utaratibu wa kukubaliana vipaumbele vyao na kupanga kwa pamoja bajeti ya kutekeleza vipaumbele hivyo. Kila mmoja wao yuko wazi kwa mwenzi wake na hakuna ambaye anamficha mwenzake kile anachopata na anavyotumia kipato hicho. Kwa kufanya hivi, wanandoa hawa watakuwa wamepunguza kama siyo kuondoa kabisa migogoro ya kifedha baina yao.

Kati ya njia zote za usimamizi wa fedha katika ndoa zilizotajwa hapo juu, wanandoa wanapaswa wachague njia ambayo inawafanya wawe wazi katika vipato, mipango na matumizi ya fedha zao. Hii ndiyo maana ya kuwa mwili mmoja kwenye masuala ya fedha.

Ungependa kujifunza zaidi kuhusu masuala ya fedha katika ndoa?

Hapa nimekutajia tu bila kufafanua namna mbalimbali za usimamizi wa fedha katika ndoa. Kama unapenda kujifunza zaidi mada hii, basi jipatie kitabu chetu kinachoitwa Siri za Mafanikio ya kifedha Katika Ndoa na Familia: Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

Je, unataka kupata mafunzo endelevu kuhusu mafanikio kwa mkristo?

Kama unataka kuendelea kujifunza kuhusu masuala mbalimbali juu ya mafanikio kwa mkristo unaweza kujiunga na mtandao huu ili uweze kupata makala mbalimbali kuhusu masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), maisha ya kikristo, malezi ya watoto na mengine mengi. Kwa kufanya hivyo, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa katika mtandao huu.

Ili kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini.

About Devotha Shimbe

Devotha Shimbe ni Mwalimu na mwanasaikolojia. Amepata pia mafunzo ya Theolojia. Devotha amejitoa kumtumikia Mungu katika maisha yake yote na amekuwa akifundisha na kutoa semina mbalimbali kuhusu mahusiano na maisha ya kiroho kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *