Hivi ndivyo akina baba wanavyoweza kuwapeleka watoto wao kwa Yesu

 Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Mwalimu mmoja asiyeamini kwamba Mungu yupo (atheist), siku moja alimtuma mwanafunzi wake kwenda nje ya darasa na kungalia juu. Aliporudi mwalimu aliuliza, umeliona anga? Umeyaona mawingu? Umeuona mwanga wa jua? Mwanafunzi alikuwa akijibu “ndiyo” kwa kila swali. Na mwisho mwalimu alimuuliza, “Umemuona Mungu”? Mwanafunzi alijibu “Hapana”. Kufuatia jibu hilo mwalimu akasema, “Kama hujamuona Mungu, basi huu ni ushahidi kuwa hakuna Mungu”.

Darasa zima lilikuwa kimya kwa muda na ndipo mwanafunzi mmoja alijitokeza na kuanza kumuuliza yule mwanafunzi aliyekuwa akiulizwa na mwalimu. Alimuomba aangalie kila upande ndani ya darasa lao na ndipo akaanza kumuuliza, “umeuona ubao wa kuandikia mwalimu (blackboard)?” “Umeviona vitabu?” “Umeyaona madawati?”.”Umemuona mwalimu?”. Yule mwanafunzi alijibu “ndiyo” kwa kila swali.

Swali la mwisho lilikuwa ni  hili, “Umeuona ubongo wa mwalimu”? Yule mwanafunzi alijibu, “hapana”. Yule muuliza swali akasema, “huu ni ushahidi kuwa mwalimu wetu hana ubongo maana hujauona”.

Hatuwezi kumuona Mungu. Naamini kati yetu hakuna aliyemuona Mungu. Pamoja na kwamba hatumuoni, tunaamini kwamba yupo. Mungu wetu ni Mungu asiyeonekana, anaweza kuonekana kupitia kwa baba zetu wa duniani. Baba zetu ni mabalozi wa Mungu katika familia zenu. Kila mtu anayeitwa baba ni balozi wa Mungu hapa duniani.

 Kupitia kwa akina baba wa duniani, watoto wao wanaweza kuwa na picha ya Mungu. Nadhani ndiyo maana anaitwa Baba wa mbinguni. Huu ni mzigo mkubwa kwa akina baba maana watoto wakiangalia jinsi ulivyo wanapata picha ya Mungu. Ukiwa baba mzuri, watoto wanapata picha nzuri ya Mungu na kama mwenendo wako ni mbaya, watoto watapata picha mbaya juu ya Mungu.

Siku moja Mchungaji mmoja wa chuo (chaplain) alikuwa na wakati mgumu wakati akitoa ushauri wa kichungaji (pastoral counselling) kwa binti mmoja ambaye alikuwa na picha mbaya juu ya Mungu. Kila aliposikia watu wakimtaja Mungu kama “Baba wa mbinguni” alikuwa akishangaa na kukunja uso. Baadaye mchungaji alikuja kugundua kuwa yule binti alikuwa akinyanyaswa sana na baba yake mzazi tangu utotoni.

Kwa binti huyu, kipimo cha Baba wa mbinguni kilikuwa ni baba yake wa duniani. Kwa kuwa baba yake mzazi hakuwa mwema, binti huyo alipata shida sana kumuelewa Mungu wa mbinguni kama baba mwema. Binti yule alidhani Mungu wa mbinguni naye ni mbaya kama baba yake mzazi na hivyo alimchukia na akawa hataki kusikia habari za Mungu.

Laiti kama akina baba wa leo wangetambua kuwa ni mabalozi wa Mungu katika familia zao, wasingefanya baadhi ya vitendo wanavyowafanyia watoto wao. Kuwa baba ni jukumu linaloambatana na wajibu mzito maana Mungu anaonekana kwa watoto wako kupitia kwako. Kwa watoto wako, Mungu anafanana na wewe. Kama ni baba mwenye upendo, mwema na anayejali, watoto wako watakuwa na picha nzuri ya Mungu. Lakini kama ni baba mwenye kugomba kila wakati na usiye na muda na watoto wako ni picha gani ya Mungu inaonekana kwa watoto wako?

Mwalimu mmoja aliwauliza wanafunzi wake swali, “Ni kitu gani huingia nyumbani kama simba na kuondoka kama kondoo?” Mwanafunzi mmoja aliinuka haraka haraka na kujibu, “baba!” Unadhani mtoto kama huyu atakuwa na picha sahihi juu ya Baba wa mbinguni? Ni magazeti gani, kwa mfano, watoto wako wanakuona unasoma? Ni magazeti ya udaku? Ni vipindi gani vya redio na televisheni au picha za video watoto wako wanakuona unaangalia? Je, Yesu angekuwapo hapo nyumbani kwako angesoma, kusikiliza na kungalia vitu hivyo?

Hapa kuna ushauri kwa kila mmoja wetu, “tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi (Waefeso 4:32). Watoto wako watamuona Mungu kuwa ni mwema, mwenye fadhili na aliye tayari kusamehe   kama wewe baba yao una sifa hizo. Kuwaadibisha watoto haimanishi kuwa mkali na kukaripia watoto kila wakati.

Ni bora usiwaadhibu kabisa watoto wako kuliko kuwaadhibu ukiwa na hasira. Matokeo yake mara nyingi huwa ni mabaya. Mungu si mnyanyasaji wa watoto na hivyo akina baba ambao ni mabalozi wake hawapaswi kunyanyasa watoto.  Familia ambayo haina upendo ni sawa tu la bweni la shule au chumba kwenye nyumba ya kulala wageni. Hebu ifanye nyumba yako ilipuke kwa furaha kwa kuwepo kwako nyumbani.

Angalia katika 2 Wafalme 14, Neno la Mungu linatuambia namna Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alivyotawala. Amazia alikuwa mfalme wa aina gani? Fungu la tatu linasema “…Akafanya kama yote aliyoyafanya baba yake Yoashi…” Tunapaswa kujiuliza, kwa nini alifanya kama baba yake?

Hebu kisa hiki kimuamshe kila baba na kumfundisha kuwa hata watoto wake watafanya yote anayoyafanya! Hebu kila baba amruhusu Yesu maishani mwake ili watoto watakapokuwa kama baba basi wawe kama Yesu.

Neno la Mungu linatuelekeza kuwa wavumilivu, “… vumilianeni na watu wote…” (1 Wathesalonike 5: 14). Akina baba wanapaswa kuwa wavumilivu vinginevyo watoto hawawezi kumwelewa Mungu kuwa ni mvumilivu. Watoto wenye wazazi wenye hasira za haraka wanaishia kumuogopa Mungu kwa kuwa anakasirika haraka.

Tatizo la watoto wadogo ni kwamba uwezo wao wa kutofautisha ni mdogo. Wana uwezo wa kulinganisha tu. Wanawalingalisha baba zao na Baba wa mbinguni. Wasipokuamini, hata Baba wa mbinguni watafikiria kuwa naye haamininiki.

Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu kuhusu malezi ya watoto?

Kama unataka kujifunza zaidi kuhusu malezi ya watoto, unaweza kujipatia kitabu cha Ustadi wa Kuhubiri na Kufundisha Watoto. Kitabu hiki kitakupatia mbinu za kisasa kabisa kuhusu juu ya kuwafundisha Neno la Mungu watoto wa siku hizi. Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

Vilevile, ili kupata mafunzo endelevu kuhusu malezi ya watoto na masuala mengine ya mafanikio kwa muktadha wa kikristo, unaweza kujiunga na mtandao wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio. Katika mtandao huu utapata maarifa katika maeneo ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano, malezi ya watoto na mambo mengine mengi.

Kujiunga na mtandao huu jaza fomu hii hapa chini.

 

 

 

About Devotha Shimbe

Devotha Shimbe ni Mwalimu na mwanasaikolojia. Amepata pia mafunzo ya Theolojia. Devotha amejitoa kumtumikia Mungu katika maisha yake yote na amekuwa akifundisha na kutoa semina mbalimbali kuhusu mahusiano na maisha ya kiroho kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *