Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Katika malezi ya watoto kikristo, wazazi wote wawili wana nafasi yake. Japo wanatakiwa kushirkiana lakini baba ana nafasi yake mahususi na mama pia ana nafasi yake. Tayari tumeshaona kwa kifupi namna gani akina baba wana walivyo na mchango katika kumpeleka mtot kwa Yesu. Katika makala ya leo tutaangalia mchango wa akina mama na na tutajikita Zaidi katika mkisa cha Musa.
Wachambuzi wa historia ya Biblia wanaeleza kuwa Musa alizaliwa takribani mwaka 1520 K.K na wazazi wa kiebrania waliokuwa wakiishi utumwani Misri. Wakati anazaliwa, Farao alikuwa ametoa amri kuwa watoto wote wa kiume waliokuwa wamezaliwa kipindi hicho wauawe. Kufuatia amri hii, wazazi wake walimhifadhi katika kisafina kizuri na kumweka kando kando ya mto hadi alipookotwa na binti Farao na kumfanya kuwa mwanae.
Binti yule alimuomba mama mmoja miongoni mwa waebrania amunyonyoshe Musa hadi atakapokua. Bila kujua, binti Farao alimpeleka Musa kwa Yokobedi ambaye ndiye alikuwa mama yake mzazi. Musa alinyonyeshwa na mama yake hadi alipokua na kupelekwa kwa binti Farao. Pamoja na kunyonyeshwa, alipewa elimu bora ya kiroho iliyomsaidia katika maisha yake yote.
Wakati Musa alipotimiza umri wa miaka 12, kilikuwa kipindi kigumu sana kwake na kwa mama yake maana ndicho kipindi ambacho alitakiwa kuchukuliwa kwenda kuishi ikulu. Kuanzia hapo Musa alienda kuwa chini ya malezi ya mama mwingine, mama mpagani na asiyemjua Mungu wa kweli. Musa angeweza kuasi na kuwa kinyume na mfumo mzima wa maisha yake mapya, lakini hakufanya hivyo na aliyatumia vizuri mazingira aliyokuwa akiishi kwa ajili ya kujiandaa kuwakomboa ndugu zake kutoka utumwani.
Akiwa katika mazingira ambayo hakuna uwezekano wa mama yake kuendelea kumpatia malezi yampasayo, Musa alikuwa katika hatari ya kujiingiza katika uovu wa kipagani huko Misri. Musa alikuwa amezungukwa na waabudu sanamu, wapagani na uovu wa kila aina. Lakini, kwa bahati nzuri mama yake Musa alimwandaa mtoto wake kusimama mwenyewe badala ya kumtegemea mama yake kila wakati. Hivi ndiyo akina mama wa leo wanapaswa kuwandaa watoto wao.
Watoto wanapokutana na majaribu na changamoto mbalimbali za kiroho hawapaswi kusema ngoja nikamuulize mama, bali wanapaswa kuamua kuutetea ukweli bila kumuuliza mama yao maana wanaujua kwa kuwa mama yao amewafundisha.
Baada ya kuwa ameachana na mama yake, Musa aliendelea kupokea kile ambacho tunaweza kukiita elimu ya kikristo, elimu iliyomwelekeza mapenzi ya Mungu ni yapi kwa maisha. Malaika wa Mungu waliendeleza kazi nzuri iliyoanzishwa na mama yake.
Hapa somo la kujifunza ni kuwa ukimlea mtoto katika njia impasayo, hataiacha hata atakapokuwa mzee. Musa hakuiacha.
Akina mama wanapaswa kujifunza somo hapa. Kama una mtoto ambaye pengine ameamua kumuasi Mungu, usikate tamaa. Mungu hakati tamaa, hutuma malaika ambao huendeleza kazi nzuri uliyoianza ya kuwafundisha watoto hao. Hata kama hautapata fursa tena ya kuendelea kuwapatia malezi bora ya kiroho, malaika wataendeleza mafundisho yako.
Katika Waebrania 11:24, 25, Mtume Paulo anatueleza kuwa “Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo”.Wakati anachukua uamuzi huu, alikuwa ametimiza umri wa miaka 40.
Neno la Mungu linatumbia kuwa akiwa Misri, Musa alipata elimu nzuri ya kidunia juu ya mambo mengi. “Musa akafundishwa hekima yote ya wamisri akawa hodari wa maneno na matendo” (Matendo 7:22). Mwandiihi maarufu wa vitabu vya kikristo katika kitabu chake cha Patriarchs and Prophets uk. 246 anaeleza kuwa “ Uwezo wake wa akili ulikuwa juu sana kuliko watu maarufu wa zama zote. Kama mwanahistoria, mwanafalsafa, mshairi, jemedari wa majeshi na mtunga sheria hakuna wa kumlinganisha naye”.
Huyo ndiye Musa. Mwandishi wa vitabu sita vya Biblia. Mwalimu wake wa kwanza alikuwa mtu wa kawaida tu: Mwanamke mcha Mungu, mwenye maombi, anayeamini Neno la Mungu na aliyepata elimu yake nyumbani. Baadaye, Musa alikuja kuwa kiongozi mwenye busara na uwezo mkubwa hadi akaaminiwa na Mungu kupewa jukumu zito la kwenda kuwakomboa wana wa Israeli kutoka utumwani Misri.
Uamuzi wa Musa wa kuwa tayari kupata mateso na watu wa Mungu unatukumbusha uamuzi wa Yesu. Yesu alikuwa na kila kitu mbinguni lakini aliamua kuja duniani kuteseka kwa ajili ya wokovu wetu. Hiki ndicho Musa alichochagua pia. Siku moja, Musa alipokuwa mtu mzima alitoka kwenda kuwaangalia ndugu zake ili aone maisha yao. Ndipo alipokutana na mwebrania anapigana na Mmisri. Musa alishikwa na hasira akampiga na kumuua Mmisri na kumuokoa ndugu yake. Habari hizi zilienea kwa waebrania na Wamisri hadi kwa Farao.
Farao alipopata habari hizi alitaka kumuua, lakini Musa alikimbilia nchi ya Midiani. Unaweza ukafikiri kuwa Musa alikimbilia Midiani ili kuokoa maisha yake lakini hii haikuwa sababu ya kukimbia kwake maana hakumwogopa mfalme. Tunaambiwa katika Waebrania 11:27: “Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme, maana alistahimili, kama amwonaye yeye asiyeonekana”.
Sasa kwa nini alikimbia? Musa alikuwa ameazimia moyoni mwake kuwakomboa ndugu zake kutoka utumwani lakini alihitaji kujiandaa ili kutimiza jukumu lake hilo. Alihitaji kujitenga na mambo ya kipagani ya wamisri ili apate muda wa kukaa na Mungu ili ampe uwezo wa kuwakomboa ndugu zake. Alihitaji kupata uwezo huo kutoka kwa Mungu badala ya kutegemea uwezo wake na elimu yake aliyopata kutoka Misri. Mahali pazuri alipoona panafaa kujiandaa kwa jukumu hilo zito ni Midiani.
Akiwa Midiani, kwa muda wa miaka 40 alijifunza mengi akiwa kama mchungaji wa kondoo. Kazi yake ya uchungaji ilimfundisha kuwa kiongozi mnyenyekevu, mwenye huruma na mvumilivu. Ellen G.White anatupatia maelezo ya kuvutia sana katika Patriarchs and Prophets uk. 248.“Muda, kubadilisha mazingira na ushirika na Mungu vingeweza kuondoa mvuto hasi wa Wamisri kutoka kwa Musa”.
Kwa kukaa katika sehemu tulivu ya Midiani, Musa alipata muda wa kutosha wa kumtafuta na hivyo kuwa karibu na Mungu kila siku. Kwa kufanya hivyo mivuto ya kipagani ya wamisri ilitoka na maisha yake yalibadilika. Hivyo ndivyo, tunavyobadilishwa. Bila kupata muda wa kutosha wa kumtafuta Mungu na kujitenga na mivuto isiyofaa, maisha ya mtu hayawezi kubadilika.
Juhudi za Musa kumtafuta Mungu katika jangwa la Midiani zilizaa matunda maana aligeuka kutoka kuwa mwenye hasira na muuaji na kuwa mpole kuliko watu wote duniani (Hesabu 12:3).
Yapo mengi ya kujifunza kutoka kwa Musa. Mwisho wa yote, Musa aliona ukweli wa Mathayo 6: 33 “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa”.Kwa ujumla, Musa alikuwa na mustakabali au mwisho mzuri. Lakini yote hayo yanatokana na kazi nzuri iliyofanywa na mama yake akiwa katika umri mdogo. Akina mama wa leo wanaweza kujifunza kitu kutoka kwa mama yake Musa.
Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu malezi ya watoto?
Kama unataka kujifunza zaidi kuhusu malezi ya Watoto, naweza kujipatia kitabu chetu kiitwacho Ustadi wa Kufundisha na Kuhubiri Watoto. Kitabu hiki kina mbinu zote kwa ajili ya kumfundisha mtoto wa siku hizi. Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.
Vilevile, kama unapenda kupata masomo endelevu kuhusu malezi na masuala mengine ya mafanikio kwa muktadha wa kikristo, unaweza kujiunga na mtandao wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio ili uweze kupata makala mbalimbali kupitia e-mail yako. Katika mtandao huu utapata maarifa katika maeneo ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), malezi ya watoto na mambo mengine mengi.
Kujiunga na mtandao huu jaza fomu iliyoko hapa chini.