Hii ni aina nyingine ya Uwekezaji Ambao Mtu Wa Kisasa Kama Wewe Anapaswa Kuwa Nao

Rafiki yangu mpendwa ,

Katika makala yangu iliyopita nilikushirikisha  juu ya aina ya uwekezaji wa kisasa ambao mtu wa kisasa kama wewe ni muhimu kuwa nao. Aina hiyo ya Uwekezaji huo ni uwekezaji katika masoko ya dhamana. Katika makala hayo, nilikueleza kuwa uwekezaji katika masoko ya dhamana si uwekezaji mpya duniani lakini ni uwekezaji mpya hapa nchini na ndiyo maana nikauita uwekezaji wa kisasa.

Katika makala hayo, nilikushirikisha aina moja tu ya uwekezaji katika masoko ya dhamana. Aina hiyo ni uwekezaji katika hisa . Hata hivyo, hisa ni aina moja tu ya dhamana lakini kuna aina zingine.

Kusoma makala juu ya uwekezaji katika Masoko ya Dhamana bonyeza hapa

Katika makala ya leo, naomba nikushirikishe aina nyingine ya uwekezaji. Aina hiyo ni uwekezaji katika vipande.

Vipande ni uwekezaji wa aina gani?

Uwekezaji kwenye vipande ni aina ya uwekezaji wa pamoja ambapo fedha hukusanywa kwa pamoja na baadaye kuwekezwa kwenye biashara kwa lengo la kupata faida. Vipande ni uwiano wa umiliki wa wawekezaji kwenye mfuko wa uwekezaji wa pamoja. Kila mwekezaji kwenye vipande anawekeza kulingana na uwezo wake na malengo yake. Tofauti na hisa, vipande vinajumuisha mseto wa uwekezaji wa vitega uchumi mbalimbali ambavyo fedha zilizokusanywa kwa ajili ya uwekezaji wa pamoja zinawekezwa.

Mifuko ya uwekezaji wa pamoja ni aina ya uwekezaji ambayo inaruhusu wawekezaji walio na malengo sawa kuwekeza fedha zao kwa pamoja. Wawekezaji (wenye vipande) hawamiliki dhamana hizo za mfuko moja kwa moja. Umiliki wa mfuko umegawanywa katika umiliki wa vipande. Kadiri mfuko unavyoongezeka au kupungua kwa thamani ndivyo thamani ya kipande huongezeka au kupungua pia. Idadi ya vipande inategemea bei ya ununuzi wa kipande, wakati wa uwekezaji na kiwango cha pesa kilichowekezwa.

Usimamizi wa Mifuko ya Uwekezaji nchini Tanzania

Uwekezaji katika mifuko ya pamoja nchini Tanzania unasimamiwa na Kampuni ya Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja ambayo kwa Kiingereza inaitwa Unit Trust of Tanzania – Asset Management and Investor Services (UTT-AMIS). Hii ni taasisi ya serikali iliyo chini ya wizara yenye dhamana ya masuala ya fedha nchini.

UTT-AMIS ilianzishwa mwaka 2013 kuchukua majukumu ya usimamizi wa Mifuko ya Uwekezaji wa pamoja kutoka kwa Dhamana ya Uwekezaji Tanzania (UTT) kufuatia maamuzi ya wamiliki kubadilisha muundo. Zaidi ya kusimamia Mifuko ya uwekezaji wa pamoja, kampuni ya UTT-AMIS inatoa huduma ya usimamizi wa mali za kifedha kukidhi mahitaji maalum kwa wawekezaji binafsi wa kipato cha kati na cha juu pamoja na taasisi. UTT-AMIS inaendeshwa na Bodi ya Wakurugenzi inayoundwa na wataalamu wenye taaluma mbalimbali na uzoefu kwenye masoko ya fedha na mitaji.

Faida za uwekezaji katika vipande

Kupata gawio: Kama ilivyo kwenye uwekezaji katika hisa, kwa kawaida, faida ya uwekezaji katika vipande hupatikana kupitia gawio la mapato na kukua kwa mtaji kutokana na uwekezaji uliofanywa na mfuko. Kila kipande hugawiwa  mapato sawa yaliyotokana na kiwango kilichowekezwa kama mtaji katika kipindi fulani. Kwa kawaida, gawio hili ni kubwa kuliko riba inayotolewa na mabenki ya biashara na taaisi za fedha.

Uwekezaji mseto: Kila uwekezaji una hatari zake. Ili kupunguza hatari hizo na kuongeza mapato, mifuko ya uwekezaji wa pamoja hutawanya uwekezaji. Kwa mifuko ya uwekezaji iliyopo nchini kwa sasa, hakuna kikomo kwa idadi ya wawekezaji ambao wanaweza kumiliki vipande kwenye mfuko wowote. Kuwepo kwa wawekezaji wengi zaidi katika mfuko ndivyo rasilimali zaidi na faida inavyopatikana kwa uwekezaji mseto katika mfuko.

Weledi wa wasimamizi wa mifuko ya uwekezaji: Mifuko ya uwekezaji huendeshwa na watalaam waliobobea katika masuala ya uwekezaji. Kwa hiyo, uwekezaji huu huhamisha utaalam wote wa uwekezaji kwa wale wenye uwezo wa kusimamia masuala ya uwekezaji. Kwa kuwa na wasimamizi bora wa mifuko kuna uwezekano mkubwa wa  kuongeza kipato cha mwekezaji.

Usalama wa uwekezaji: Kwa hapa nchini, mifuko ya uwekezaji wa Pamoja husimamiwa kisheria chini ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA). Sheria hii ina lengo la kumlinda mwekezaji na hivyo kuna  usalama wa kutosha katika uwekezaji huu.

Masharti rahisi ya uwekezaji:  Mwekezaji ana hiari ya kuwekeza kwa muda mrefu au mfupi kwa kuwa hakuna kipindi maalum cha uwekezaji kilichowekwa. Vilevile, ni rahisi kuuza na kununua vipande vya mifuko ya uwekezaji wa pamoja. Ni rahisi pia kwa mwekezaji kubadilisha uwekezaji wake kutoka uwekezaji wa msingi wa hisa na kuwa dhamana ya mapato ya moja kwa moja (dhamana za serikali za muda mfupi na za muda mrefu) au mchanganyiko wa aina yoyote utakaohitajika kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa kwenye waraka wa toleo wa mfuko husika.

Ukwasi: Mwekezaji anaweza kuwekeza kwa muda mrefu au mfupi kulingana na sifa za mfuko. Mwekezaji ana uwezo wa kuamua wakati anaotaka kuuza vipande pia kupata pesa za mauzo ya vipande kwa muda mfupi. Kwa kuwa uwekezaji ni kitu cha muda mrefu, wawekezaji wanashauriwa kuwa na mtazamo wa muda mrefu ili kunufaika zaidi na uwekezaji katika mifuko ya pamoja.

Uhamishaji: Kwa mifuko ya uwekezaji wa pamoja inayoendeshwa na Dhamana ya uwekezaji Tanzania uhamishaji wa vipande kutoka kwenye mfuko mmoja kwenda mwingine unaruhusiwa. Uhamishaji huu utatumia thamani halisi ya kipande kwa wakati huo bila gharama yoyote. Uhamishaji huo hufanyika kwa mauzo ya vipande kutoka kwenye mfuko mmoja na kuviwekeza kwa kanuni za vipande kwenye mfuko mwingine, ilimradi sifa za kuwekeza kwenye mfuko mwingine zimezingatiwa.

Ungependa kujifunza zaidi kuhusu uwekezaji katika vipande?

Hapa nimekushirikisha kwa kifupi sana kuhusu uwekezaji katika vipande. Kama unapenda kujifunza zaidi aina hii ya uwekezaji, basi endelea kufuatilia makala katika mtandao huu.

Je, unataka kupata mafunzo endelevu kuhusu mafanikio kwa mkristo?

Kama unataka kuendelea kujifunza kuhusu masuala mbalimbali juu ya mafanikio kwa mkristo unaweza kujiunga na mtandao huu ili uweze kupata makala mbalimbali kuhusu masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), maisha ya kikristo, malezi ya watoto na mengine mengi. Kwa kujiunga na matandao huu, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa katika mtandao huu.

 Ili kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *