Hivi Ndivyo Unavyoweza Kufanya ili  Kuitikia Maelekezo ya Yesu Aliposema “Waacheni Watoto wadogo Waje Kwangu…

Rafiki yangu mpendwa Katika Kristo,

Neno la Mungu linaeleza kuwa Basi wakamletea watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni, Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia” (Marko 10:13 -16).

Ni siku nyingine ya kazi kwa Yesu. Akiwa amekaa ndani ya nyumba akiongea na wanafunzi wake, mara kundi la wazazi wakaja wakiwa na watoto wao wakitaka wawalete kwake. Wazazi hawa walihitaji Yesu awaguse watoto wao.

Mtu anaweza kufikiria kuwa wazazi hawa walikuwa ni watu wanaotukuza na kuabudu watu maarufu na ndiyo maana waliwaleta watoto wao kwa Yesu, mtu maarufu, ili awaguse. Wazazi hawa walikuwa hawatafuti kitu kama hicho bali walikuwa wanatafuta mguso wa Yesu ili ubadilishe maisha ya watoto wao.

Mguso ni njia ya kuleta baraka na Yesu alitumia njia hiyo mara nyingi kuwabariki na kuwaponya watu. Yeyote aliyepata bahati ya kumgusa au kuguswa na Yesu hakubaki kama alivyo, alikuwa mtu tofauti kabisa. Fikiria mama yule aliyekuwa akitokwa damu kwa muda wa miaka 12 alipomgusa Yesu tu akapona (Luka 8: 43 – 44). Fikiria pia mtu yule aliyezaliwa kipofu lakini alipoguswa tu na Yesu akaanza kuona (Yohana 9:6 -7)

Miaka mingi baada ya tukio la watoto kupelekwa kwa Yesu, wataalam wamegundua kuwa mguso unaotokana na kukumbatiwa au kushikwa ni muhimu sana. Chuo kikuu cha Purdue kilichoko Indiana, Marekani kiliwahi kufanya utafiti unaohusiana na mguso na matokeo ya utafiti huo ni ya kushangaza sana.

Utafiti huo ulifanywa kwa wakutubi wa chuo. Nusu ya wakutubi waliombwa kuwagusa watu wote walioingia katika maktaba ya chuo kuazima vitabu,  kurudisha vitabu  walivyokuwa wameazima au kupata huduma yoyote ya maktaba. Nusu nyingine ya wakutubi waliombwa kuendelea na utaratibu wa kawaida, yaani, kutoa huduma bila kuwagusa wateja wao.

Matokeo ya utafiti huo yalionesha kuwa wale watu waliokuwa wakiguswa walionyesha heshima kubwa sana kwa wakutubi na waliheshimu sana sheria na taratibu za maktaba. Kundi la wale waliopewa huduma bila kuguswa hawakuonyesha tabia hizi.

Utafiti huu, unadhihirisha kuwa mguso una matokeo chanya katika tabia na mwenendo wa mtu. Tafiti zimeonesha kuwa watu wamekuwa wakijisikia vizuri na hata kupata uponyaji kutokana na mguso wa wanyama kama vile mbwa na paka. Kama mguso wa mwanadamu na wanyama unaweza kuwa na matokeo chanya kiasi hiki, mguso wa Mungu si utakuwa zaidi!

Kama watu wanahitaji mguso wa wanadamu na wanyama ili kujisikia vizuri na hata kupata uponyaji wa kiafya, ni kitu cha kushangaza kuona wanafunzi kuwazuia wazazi walipowapeleka watoto kwa Yesu!

Inaonekana wanafunzi walikuwa hawajui umuhimu wa mguso. Wanafunzi walimuona Yesu kuwa ni mtu maarufu sana na kama ilivyo kwa mtu maarufu yeyote ana ratiba iliyojaa na hivyo hawezi kupoteza muda kuonana na watu wadogo , yaani , watoto ambao wakati mwingine huwa ni wasumbufu!

Huenda wanafunzi wa Yesu waliwazuia wazazi ili Yesu apate muda wa kushughulikia masuala mengine ya muhimu zaidi. Kwa mtazamo wa wanafunzi, watoto si muhimu na hivyo hawahitaji kuguswa na Yesu. Kwa mtazamo wao, Yesu ni wa watu wazima tu!

Hivi ndivyo tunavyofanya hata sisi wanafunzi wa leo, tunadhani Yesu ni wa watu wazima tu na tunafanya mambo ambayo yanawafanya watoto wasiende kwa Yesu kwa kudhani kuwa wataenda kwa Yesu watakapokuwa watu wazima.

Hebu kila mmoja wetu atafakari ni kwa namna gani amechangia kuwafanya watoto wasiende kwa Yesu.

Je, umeshindwa kuwafundisha neno la Mungu wakiwa nyumbani.

 Je , umewazuia wasiende kanisani badala yake waende shambani, tuisheni au kwenye biashara? Je, umewanyima fursa ya kusoma katika shule za kiadventista bila sababu ya msingi?

Je umezuilia mkono wako kutoa kwa ajili ya kuboresha uwepo wa shule za ambazo zinafundisha watoto elimu ainayoambatana na maadili ya kikristo?

Kitendo hiki cha wanafunzi wa Yesu kinashangaza, ukizingatia muda mfupi tu kabla ya hapo alikuwa amemchukua mtoto na kumkumbatia mbele ya wanafunzi hao hao na kusema “Mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma” (Marko 9: 37).

Watoto ni muhimu sana kwaYesu. Umuhimu wa watoto kwa Yesu unadhihirishwa na namna alivyowakasirikia wanafunzi katika Marko 9: 42 aliposema “na yeyote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini.

Hakika hili ni onyo kali sana. Kwa maneno mengine Yesu alikuwa anawaambia kuwa mtu yeyote anayesababisha watoto hawa wasiende kwa Yesu, kwa namna yeyote ile, adhabu yake ni kifo (maana haitegemewi mtu atapona baada ya kufungwa jiwe shingoni na kutoswa baharini).

Kumbe, chochote tunachokifanya kuwazuia watoto wetu wasiende kwa Yesu, kitatugharimu uhai wetu.!! Sijui kama tulishawahi kufikiria hili! Yesu anayajua vizuri maisha ya mwanadamu. Hakuna ajuaye maisha ya wanadamu kwa undani kuliko Yesu na ndiyo maana anawaonya wanafunzi na kupitia kwao anatuonya sisi juu ya wajibu wetu kwa watoto wadogo na waumini wengine wenye imani changa. Anajua kuwa watoto na watu wengine wenye imani changa wanaweza kupotezwa kirahisi. 

Wakati Yesu anawaonya wanafunzi wake, alisema; “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie. Kwani nini Yesu alitoa agizo hilo? Yesu anatoa jibu katika mstari unaofuata; “kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao”. Hiki ndicho kiini cha fungu hili.

Kama tunahitaji watoto hawa waingie katika ufalme wanaoahidiwa na Yesu, ni lazima tuwapeleke kwake. Ni lazima wapate elimu ya kiroha ili iwaandae kuingia katika ufalme huo. Ni lazima tuwapeleke kwa Yesu ili awaguse, kuwabariki na kuwabadilisha maisha yao kutoka ndani ya mioyo yao.

Ili uweze kuwasaidia watoto kwenda kwa Yesu, ni lazima ujue mbinu za kuwafundisha na kuwahubiri Neno la Mungu. Kwa kuwa tunaishi katika kizazi cha karne ya 21, karne yenye maendeleo makubwa ya Sayansi na Teknolojia, ni lazima ujue mbinu za kisasa kabisa za kuwafundisha watoto wa siku hizi.

Je, unapenda kujifunza kuhusu namna ya kufundisha au kuhubiri watoto wa siku hizi?

Basi pata kitabu juu ya Ustadi wa Kuhubiri na Kufundisha Watoto. Kitabu hiki kitakupatia mbinu zote kwa ajili ya kufundisha na kuhubiri watoto wa umri tofauti tofauti. Kupata kitabu hiki  na vitabu vingine unaweza kuwasiliana nasi namba za simu; +255-754-405582 (Simeon Shimbe), +255-714-606278 (Devotha Shimbe), Email:spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

Je, unataka kupata mafunzo endelevu kuhusu mafaniko kwa mkristo?

Kama unataka kuendelea kujifunza kuhusu masuala mbalimbali juu ya mafanikio kwa mkristo unaweza kujiunga na mtandao huu ili uweze kupata makala mbalimbali. Kwa kufanya hivyo, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa katika mtandao huu.

Ili kujiunga, jaza fomu niliyoko hapa chini.

About Devotha Shimbe

Devotha Shimbe ni Mwalimu na mwanasaikolojia. Amepata pia mafunzo ya Theolojia. Devotha amejitoa kumtumikia Mungu katika maisha yake yote na amekuwa akifundisha na kutoa semina mbalimbali kuhusu mahusiano na maisha ya kiroho kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *