Hivi Ndivyo Unavyoweza Kujenga Msingi Bora wa Malezi kwa Mtoto Wako

Rafiki yangu Mpendwa katika Kristo,

Mojawapo ya mashujaa wa imani tunaowasoa kwenye Biblia ni Danieli na wenzake watatu. Danieli alizaliwa katika ufalme wa Yuda katika kipindi cha wasiwasi na misukosuko kutokana na kuibuka kwa Babeli kama ufalme wenye nguvu kwa wakati ule. Danieli alikuwa ni kijana mdogo tu mwenye miaka inayokadiriwa kuwa kati ya 15 na 17 alipotolewa katika mazingira aliyoyazoea, yaani,taifa lake la Yuda, familia yake, rafiki zake, sinagogi lake na jumuia yote iliyomzunguka.

Mfalme Nebukadneza wa Babeli alikuwa amevamia na kuteka jiji la Yerusalemu lililokokuwa makao makuu ya taifa la Yuda.Tukio hili lilitokea mwaka 605 K.K ambapo watu wapatao 10,000 walikamatwa mateka na kupelekwa Babeli akiwemo Danieli na wenzake watatu (Hanania,Mishaeli na Azaria).

Wakiwa uhamishoni kule Babeli, Danieli na wenzake walipelekwa, katika kile ambacho kwa leo kinaweza kuitwa, Chuo Kikuu cha Babeli. Wakiwa kule walibadilishiwa majina yao na kupewa mengine ili kupata utambulisho mpya ulioendana na mazingira ya taifa hilo la kipagani (Danieli aliitwa Belteshaza, Hanania aliitwa Shadraka, Mishaeli aliitwa Meshaki na Azaria akaitwa Abednego). Walitakiwa kujihusisha na utamaduni na mtindo mpya wa maisha ya waabudu sanamu. Walipaswa kula, kuzungumza, kuvaa na hata kufikiri kama wababeli. Utambulisho wao na dini yao ya kiebrania vilikuwa hatarini kupotea.

Baada ya kuwa wamebadilishwa majina, walipewa chakula maalum kutoka kwa mfalme. Lakini Danieli, kwa sababu ya mafundisho na malezi, elimu iliyojengwa juu ya ubora, “ aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme wala kwa divai aliyokunywa;  basi akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi” (Danieli 1:8).

Danieli na rafiki zake waliomba wasipewe chakula kingine zaidi ya mtama na maji tu. Walikataa chakula cha mfalme kwa sababu zifuatazo: Kwanza, baadhi ya vyakula hivyo vilikuwa najisi, kwa maana ya kwamba Mungu aliwakataza kula vyakula hivyo kama tunavyosoma katika Mambo ya Walawi sura ya 11. Pili, hata nyama iliyosafi ilikuwa haiandaliwi vizuri kwa jinsi Mungu alivyoelekeza, kupitia kwa Musa. Tatu, kula chakula hicho na kunywa divai hiyo lilikuwa ni tendo la ibada ya sanamu kwani chakula na vinywaji hivyo vilitolewa kwanza sadaka kwa miungu. Kwa kutambua haya, walichagua kuwa waaminifu kwa Mungu wao. 

Wakiwa wamegomea chakula cha mfalme, akina Danieli, waliomba wajaribiwe kwa siku kumi na baadaye walinganishwe na wale watakaokula chakula cha mfalme ili waone nani ana afya nzuri zaidi. Biblia inasema “hata mwisho wa zile siku kumi nyuso zao zilikuwa nzuri zaidi, na miili yao ilikuwa imenenepa zaidi, kuliko wale vijana waote waliokula chakula cha mfalme” (Danieli 1:15). Danieli na wenzake walifaulu mtihani huo ambao ulikuwa mtihani wa kwanza kwao.

Danieli na wenzake walisoma katika Chuo Kikuu cha Babeli kwa muda wa miaka mitatu. Baada ya hapo, wakiwa na wanafunzi wenzao, waliletwa mbele ya mfalme Nebukadreza ili awaone kama wamefuzu vizuri masomo yao. Huu unaweza kulinganishwa na mtihani wa mwisho wa kumaliza Chuo Kikuu. Mfalme aliwapima vijana wote akiwemo Danieli na wenzake.

Kitu cha kushangaza ni kwamba katika kila jambo la hekima na ufahamu alilowauliza mfalme, akawaona kuwa walifaa mara kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake” (Danieli 1:20). MfalmeNebukadreza alivutiwa sana na ufahamu wa Danieli na rafiki zake na akawaajiri moja kwa moja na kuwafanya kuwa maafisa waandamizi katika serikali yake na wakapangiwa kuufanya kazi katika ikulu ya mfalme.

Upo msemo wa kiingereza unaosema Charity begins at home (wema wa mtu huanzia nyumbani kwao). Mara nyingi kauli hii htumuika kumaanisha kuwa wema wa mtu unapaswa uanze kutendwa nyumbani. Lakini tunasahau kuwa huwezi kutenda wema kama hauna huo wema. Hivyo, ili uweze kutenda wema nyumbani, lazima wema huo uwe umeandaliwa nyumbani.  Hiki ndicho kilitokea kwa akina Danieli. Tabia yao nzuri ya kumpenda Mungu na kukataa upagani, japo haitajwi kama waliionesha nyumbani pia, iliandaliwa nyumbani kwao  (katika ufalme wa Yuda).

Je, tabia ya akina Danieli, iliandaliwaje na iliandaliwa na nani? Huenda, jambo la muhimu sana katika kisa hiki ni kile ambacho hakijaandikwa; yaani, kilichotokea nyuma ya pazia. Kuna mashujaa wengi ambao hawakutajwa katika kisa hiki lakini walichangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya akina Danieli wawe kama walivyokuwa. Watu hao ni pamoja na wazazi wao na walimu wao katika masinagogi  ya Yuda. Na bila shaka jumuia nzima iliyowazunguka nayo ilihusika maana katika utamaduni wa mashariki na hata Afrika ikiwemo Tanzania kwa wakati ule, jukumu la kumlea mtoto lilikuwa la kijiji kizima.

Mafanikio ya akina Danieli kule Babeli hayakuja kama bahati. Kulikuwa na miaka ya awali ya elimu na mafunzo yaliyoanzia  nyumbani kwao na baadaye katika masinagogi baada ya kufikia miaka 12. Katika sinagogi, kila mvulana wa kiebrania alifundishwa historia takatifu, torati na usomaji wa neno la Mungu. Hii ni elimu iliyojengwa juu ya ubora lakini isiyo katika mfumo rasmi wa elimu. Hii ndiyo ilkuwa siri ya mafanikio ya baadaye ya  akina Danieli waliopenda Babeli.

Naam, hiki ni kisa cha kuvutia sana. Unaweza kujiuliza, ni kitu gani kilimfanya Danieli awe na ujasiri wa kusimama imara upande wa Mungu katika mazingira ya kipagani? Ilikuwaje akawa mwanafunzi bora mara kumi zaidi ya wengine katika Chuo Kikuu cha Babeli?

Baadaye katika kipindi cha zahama akiwa ikulu kwa Nebukadreza, aliwezaje kutafsri ndoto ya mfalme?

Je, sisi kama wazazi au kanisa, tunawezaje kuandaa kizazi kijacho cha akina Danieli  ambao wataweza kutafsiri ndoto za wakuu wa nchi katika sehemu zao za kazi na katika taaluma zao?

Je, Ungependa Kujifunza Zaidi Namna Unavyoweza Kuwaanda Akina Danieli wa Leo?

Ili tuweze kuwaanda akina Danieli wa leo, ni lazima tuwe na nyenzo za kuwaandalia. Mojawapo ya nyezno hizo ni vitabu bora.

Leo naomba nikushirikishe kitabu bora kabisa kinachoweza kukupatia mbinu za kisasa kabisa kwa ajili ya kuwafundisha watoto wa siku hizi Neno la Mungu.

Kitabu hicho kinaitwa Ustadi wa Kufundisha na Kuhibiri Watoto. Kitabu hiki kitakupatia mbinu zote kwa ajili ya kufundisha na kuhubiri watoto wa umri tofauti tofauti.

Kupata kitabu hiki  na vitabu vingine unaweza kuwasiliana nasi namba za simu; +255-754-405582 (Simeon Shimbe), +255-714-606278 (Devotha Shimbe), Email:spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

Je, unataka kupata mafunzo endelevu kuhusu mafaniko kwa mkristo?

Kama unataka kuendelea kujifunza kuhusu masuala mbalimbali juu ya mafanikio kwa mkristo unaweza kujiunga na mtandao huu ili uweze kupata makala mbalimbali. Kwa kufanya hivyo, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa katika mtandao huu.

Ili kujiunga, jaza fomu niliyoko hapa chini.

About Devotha Shimbe

Devotha Shimbe ni Mwalimu na mwanasaikolojia. Amepata pia mafunzo ya Theolojia. Devotha amejitoa kumtumikia Mungu katika maisha yake yote na amekuwa akifundisha na kutoa semina mbalimbali kuhusu mahusiano na maisha ya kiroho kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *