Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuepuka Kazi yako Kugeuka kuwa Ibada ya Sanamu

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Je, Unaelewa nini kuhusu kuabudu sanamu? Je, Unahusika katika ibada ya sanamu? Je, Wapagani ndio waabudu sanamu tu?

Watu wengi, hasa wa kizazi hiki, ni wanaabudu sanamu lakini hawajui kuwa ni waabudu sanamu. Leo nitakushirikisha namna moja tu kati ya nyingi  ambavyo unaweza kuwa unaabudu sanamu bila wewe kufahamu. Nitakushirikisha pia namna unavyoweza kuepuka ibada hiyo.

Ili tujenge msingi wa kile kinachoenda kukushirikisha, hebu tuone kwanza maana ya sanamu na ibada ya sanamu.  Sanamu inaweza kuelezewa kama kitu cha kuchongwa au uwakilishi wa kitu chochote kinachoabudiwa kama mungu. Kwa maneno mengine, sanamu inaweza kuwa mbao iliyochongwa, jiwe au kitu chochote, mawazo, wazo, pesa au mali nyingine yoyote ambayo inawakilisha mungu au kitu cha kuabudiwa.

Kwa maneno mengine, tunaweza kusema kuwa chochote unachokipa kipaumbele mbele za Mungu Mwenyezi, kukifanya kipaumbele chako cha juu zaidi, hicho ni sanamu. Wengi wanaoitwa wakristo huitumikia miungu mingine kando ya Mungu. Muumbaji wetu anadai ibada yetu kamili, utii wetu wa kwanza. Kitu chochote kinachoelekea kupunguza upendo wetu kwa Mungu, au kuvuruga utumishi ambao ni stahili yake, kwa sababu hii kinakuwa sanamu

Mojawapo ya kitu kizuri na muhimu lakini kimegeuka kuwa sanamu kwa baadhi ya watu ni kazi. Kutokana na watu wengi kufanya kazi kwa bidii, kuna hatari kubwa ya kumsahau Mungu katika ratiba zetu za kazi na pumziko. Tusipoangalia tunaweza tukafanikiwa kufanya kazi vizuri na pia tukapata muda wa kupumzika lakini tukamsahau Mungu.

Kipimo kimoja kizuri kinachoweza kutusaidi kujua kama  kazi zetu zimegeuka kuwa sanamu ni kama hatumpi Mungu nafasi katika kazi na pumziko. Hebu hapo ulipo jaribu kujiuliza mwenyewe ni muda gani unautumia kufikiria masuala ya kazi wakati tukiwa hauko kazini? Kama muda wetu mwingi tunautumia kufanya kazi na kuwaza kuhusu kazi kuliko tunavyoutumia kumuwaza Mungu, basi tujue kuwa hicho ni kiashria kuwa kazi zetu zimegeuka kuwa sananmu.

Mfano mzuri wa matokeo ya kumuacha Mungu katika kazi zetu ni kisa cha Martha na Mariamu. Kisa hiki kimeelezwa katika suara ya 10 ya kitabu cha Luka Sehamu ya kisa hiki inasema “Ikawa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake.  Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie. Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa” (Luka 10: 38-42).

Wakristo wa leo, mara nyingi tunafanana na Martha kuliko Mariamu. Tuna shughulika zaidi na “utumishi mwingi” huku tukisahau kabisa kwamba tunahitaji pia kukaa miguuni mwa Yesu. Kama tutaruhusu kazi zetu zichukue nafasi ya Mungu, basi kazi zetu zitageuka kuwa ibada ya sanamu. Pamoja na umuhimu wa kazi zetu, hatuna budi kufuata kielelezo cha Mariamu na kutenga muda wa kutosha ili kukaa chini ya miguuni ya Yesu na kwa kufanya hivyo tutakuwa “tumechagua fungu lililo jema”, ambalo hatutaondolewa.

Kama tutaamua kuchagua fungu lililo jema tutaamua kutenga muda wa kutosha kwa ajili ya kusoma Neno la Mungu, maombi ya familia na ya mtu mmoja mmoja, ibada na maombi ya pamoja kanisani au mahali pengine, kutoa huduma kwa jamii wakiwemo wahitaji, kufanya shughuli za kanisa na kufanya uinjilisti kwa njia mbalimbali. Sambamba na haya yote hatutasahau kumrudishia Mungu zaka na kumtolea Sadaka kwa kila mali tunayoipata baada ya kufanya kazi. Kama tutashindwa kufanya haya, tujue wazi kwamba tuko katika hatari ya kugeuza kazi zetu kuwa ibada ya sanamu.

Unawezaje kupata muda na Mungu?

Kwa kawaida watu wenye mafanikio kiuchumi wana shughuli nyingi kiasi kwamba wanaweza kukosa muda wa kuwasiliana na Mungu kwa njia ya ibada na kusoma au kusikiliza Neno la Mungu. Matokeo ya kukosa muda na Mungu ni kuwa mtu unayetegemea vitu vingine kwa ajili ya mafaniko yako badala ya kumtegemea Mungu. Hii ni hatari sana kwa mkristo.

 Ili kuepuka hatari hii, unapaswa kumfanya Mungu kuwa wa kwanza kwa vitendo.  Hilo linawezekana kwa kuiga mfano wa Yesu ambaye alikuwa na kawaida ya kuanza siku yake kwa maombi. Biblia inaeleza kuwa “Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko” (Marko 1:35). Lakini pia unaweza kutafuta muda katikati  ya shughuli zako na kuwasiliana na Mungu, kusoma na kusikiliza Neno lake. Kwa mfano ukiwa kazini unaweza kusikiliza vipindi vya Radio au televisheni vinavyohusiana na mambo ya kiroho. Vilevile, unaweza kufuatilia mambo ya kiroho kutoka kwenye mitandao kama vile you tube, facebook na mitandao mingine ya kijamii. Kwa kuanza siku na Mungu kabla ya shughuli zako zote na kuendelea kufuatilia mambo ya kiroho siku nzima, mibaraka na ulinzi wa Mungu vitaambatana nawe siku nzima katika shughuli zako.

Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mafanikio?

Basi jipatie kitabu chetu kinachoitwa Siri za Mafanikio ya kifedha kwa Mkristo: Elimu isiyofundishwa Shuleni. Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

Je, unataka kupata mafunzo endelevu kuhusu mafanikio kwa mkristo?

Kama unataka kuendelea kujifunza kuhusu masuala mbalimbali juu ya mafanikio kwa mkristo unaweza kujiunga na mtandao huu ili uweze kupata makala mbalimbali. Kwa kufanya hivyo, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa katika mtandao huu.

Ili kujiunga jaza fomu iliyoko hapa chini.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *