Rafiki yangu mpendwa,
Mara nyingi tunaposikia suala la deni la taifa au mikopo kwa serikali, mawazo yetu yanakimbia moja kwa moja katika nchi zilizoendelea pamoja na mashirika ya kimataifa kama vile Shirika la Fedha Duniani, Benki ya Dunia na mengine mengi. Hawa ndio wakopeshaji wakuu wa Serikali.
Ndiyo, hawa ndiyo wakopeshaji wakubwa wa Serikali, lakini kuna wakopeshaji wengine ambao hawajulikani sana kwa hapa Tanzania. Kwa sababu hawajulikani, hata kwenye mjadala juu ya mikopo ya Serikali hawatajwi sana. Kwa mfano, mara kadhaa kumekuwa kukiibuka mjadala hapa nchini kuhusu deni la taifa, yaani kiasi cha fedha ambacho Serikali inadaiwa kutokana na mikopo. Kinachokuwa kinajadiliwa na wengi ni mikopo kutoka kwa wakopeshaji wakuu wa Serikali niliowataja hapo juu. Huwa hatusikii sana wakopeshaji wengine wakijadiliwa.
Katika makala haya, sikusudii kabisa kusema chochote kuhusiana na deni la taifa na kama Serikali iendelee kukopa au la. Ninachotaka kukushirikisha tu ni kwamba, tunapozungumzia Serikali kukopa si lazima iwe mikopo ya nje bali kuna mikopo ya ndani pia. Na mikopo hiyo ya ndani si lazima Serikali ikope katika mabenki ya biashara bali inaweza kukopa hata kwa watu binafsi. Huenda hujanielewa. Ninamaanisha kuwa hata wewe unaweza kuikopesha Serikali. Ninaposema wewe, ninamaanisha wewe unayesoma makala haya.
Huenda ulikuwa hujui kuwa hata wewe unaweza kuikopesha Serikali. Kama hivyo ndivyo, fuatana nami katika makala haya nikueleze habari hiyo ambayo ni moja ya fursa ambazo zinaweza kukutajirisha kwa kukupatia kipato cha uhakika.
Kwa Namna Gani Unaweza Kuikopesha Serikali?
Serikali ina vyanzo vingi vya mapato ikiwa pamoja na kodi, ushuru na tozo za aina mbalimbali, misaada na mikopo ya ndani ya nje ya nchi. Kwa upande wa mikopo ya ndani ya nchi, serikali kupitia benki kuu hukopa fedha kwa ama taasisi au mwananchi mmoja mmoja kupitia dhamana za Serikali.
Serikali inapochukua mkopo (kupitia dhamana za Serikali) usiozidi mwaka mmoja (si zaidi ya siku 365), mikopo hii inaitwa hatifungani au dhamana za serikali za muda mfupi (treasury bills) na mikopo inayozidi mwaka mmoja (zaidi ya siku 365) inaitwa dhamana za serikali za muda mrefu (treasury bonds). Kwa kawaida, riba (coupon rate) ya dhamana za serikali za muda mfupi ni 3.24%, 5.21% na 9.17% wakati riba za dhamana za serikali za muda mrefu huwa ni 7.82%, 9.18%, 10.08%, 11.44%,13.5% na 15.49% kulingana na muda wake.
Dhamana za Serikali za muda mfupi (hati fungani) kwa kiwango kikubwa huiwezesha Serikali kugharamia kwa muda nakisi katika bajeti yake inayosababishwa na upungufu wa mapato ukilinganisha na matumizi ya Serikali.
Dhamana za Serikali za muda mrefu kwa kiwango kikubwa huiwezesha Serikali kugharamia mahitaji ya miradi ya maendeleo. Dhamana zimegawanyika katika makundi matatu kulingana na mtoaji. Makundi hayo ni dhamana za serikali, dhamana za makampuni na dhamana za manispaa.
Dhamana za Serikali huuzwa kwenye soko la awali kwa njia ya ushindani kupitia minada. Soko la awali ni pale ambapo Benki Kuu huuza dhamana hizi kwa umma kwa mara ya kwanza. Mnada hufanyika mara mbili kwa mwezi. Uuzaji na Ununuzi wa dhamana hizo baada ya hapo hufanywa kwenye soko la upili, yaani Soko la Hisa la Dar es salaam (Dar es salaam Stock Exchange). Mkazi yeyote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anaruhusiwa kushiriki katika mnada wa Dhamana za Serikali.
Kwa mujibu wa Miongozo ya Benki Kuu juu ya Namna ya kushiriki katika Soko la Awali na la Upili la Dhamana za Serikali wa mwaka 2015,wakala au mwekezaji mwenye kiwango cha kuanzia shilingi laki tano (500,000) tu anaruhusiwa kushiriki katika mnada wa Dhamana za Serikali za muda mfupi na kwa dhamana za serikali za muda mrefu kiwango cha kuanzia ni shilingi milioni moja (1,000,000) tu.
Dhamana za serikali za muda mfupi zipo katika makundi manne kutegemea na muda zitakapoiva. Makundi hayo ni ya siku 35, siku 91, siku 182 na siku 364. Kwa upande wa Dhamana za Serikali za muda mrefu zipo za muda wa miaka 2, 5, 7, 10,15, 20 na miaka 25.
Faida za kuwekeza kwenye dhamana za Serikali ni zipi?
Uwekezaji katika dhamana za serikali una faida nyingi. Baadhi ya faida hizo ni hizi zifuatazo:
- Ni uwezekezaji usio na hatari (risk free investement). Kuwekeza katika Dhamana za Serikali ni salama kwani Serikali haitarajiwi kukiuka mategemeo ya wadai wake wakati wa malipo.
- Dhamana za Serikali zinahamishika, hivyo mwekezaji anaweza kuziuza kabla ya muda wake wa kuiva endapo itakuwa ni lazima afanye hivyo.
- Dhamana za Serikali zinaweza kutolewa kama Dhamana kwa ajili ya mkopo.
- Dhamana za Serikali zina kiwango cha faida kikubwa kuliko riba unayoipata kwa kuweka fedha benki.
Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mada hii ?
Hapa nimekushirikisha kwa kifupi sana kuhusu uwekezaji katika dhamana za serikali. Huenda umebaki na maswali mengi yasiyo na majibu. Basi endelea kufuatilia mtandao huu ili uzidi kupata elimu zaidi kuhusu uwekezaji huu na aina nyingine za uwekezaji.
Je, unapenda kupata masomo endelevu kuhusu mafanikio?
Kama unapenda kupata masomo endelevu kuhusu fedha na masuala mengine ya mafanikio kwa muktadha wa kikristo, unaweza kujiunga na mtandao wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio. Katika mtandao huu utapata maarifa mazuri katika maeneo ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), malezi ya watoto na mambo mengine mengi.
Kujiunga na mtandao huu jaza fomu hii hapa chini.
1 comment / Add your comment below