Hii Ndiyo Sababu Kwa Nini Unapaswa Kutoa Zaka

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Watu wengi wakiwemo wakristo, hutafuta mafanikio ya kifedha ili wafaidike wao wenyewe na familia zao tu. Lakini haipaswi kuwa hivyo, badala yake fedha unapoipata, kabla ya hata hujaanza kuitumia yakupasa kumpatia Mungu kilicho chake kama Neno la Mungu linavyosema “Yesu akajibu, akawaambia, Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya Mungu mpeni Mungu. Wakamstaajabia sana” (Marko 12:17).

Baada ya kumpatia Mungu kilicho chake, kiasi kinachobaki hupaswi kitumia wewe pekee yako bali una wajibu pia wa kuisadia jamii inayokuzunguka. Kwa kifupi, fedha au mali ya aina nyingine unayopata, unapaswa kuigawanya katika makundi matatu. Kundi la kwanza ni kwa Mungu, yaani zaka na sadaka, kundi la pili ni kwa ajili yako na kundi la tatu ni misaada kwa jamii.

Njia ya kumpatia Mungu kilicho chake ni kupitia zaka na sadaka. Katika makala haya, nitakushirikisha kwa kifupi dhana ya utoaji wa zaka ili uweze kufahamu kwanini mimi na wewe tunapaswa kutoa zaka.

Zaka ni nini na ni kiasi gani?          

Zipo dhana mbalimbali na zinazotofautiana baina ya wakristo kuhusu zaka. Kwa uelewa wa baadhi ya watu zaka ni kiasi cha fedha ambacho mtu anaamua kutoa ili kutegemeza kazi ya Mungu kulingana na baraka ambazo anaamini Mungu amempatia. Kwa wengine, zaka ni kiasi cha fedha ambacho mtu anapangiwa kutoa na uongozi wa kanisa ili kutegemeza kazi ya Mungu. Wapo wanaotoa kila wanapopata fedha, lakini wengine hutoa kila wanapoenda kwenye ibada na wengine hutoa kila baada ya kipindi fulani kama vile mwezi, mwaka na kadhalika.

Pamoja na kutofautina kwa mitazamo ya watu kuhusiana na zaka, maelekezo ya Biblia yako wazi.Kwa kifupi, zakani moja ya kumi ya mapato yako au ya mali yako yote uliyopata katika kipindi fulani. Mapato hayo yanaweza kuwa ya siku, wiki, mwezi, msimu au mwaka kutegemeana na shughuli unayoifanya. Kwa maneno, mengine, zaka hutolewa kila unapopata fedha au mali nyingine kama vile mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi (Mwanzo 14:17-20).

Katika Biblia, utoaji wa zaka unatajwa unatajwa kwa mara ya kwanza wakati Abramu alipomtolea kuhani Melkizedeki wa Salemu zaka ya vitu vyake vyote (Mwanzo 14:17-20, Waebrania 7:1-4). Baada ya hapo, Biblia inarudiarudia agizo la Mungu la kutoa zaka kwa wana wa Israeli. “Usiache kutoa zaka ya fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokayo shamba mwaka baada ya mwaka” (Kumbukumbu la Torati 14:22). “Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya Bwana; ni takatifu kwa Bwana…. Tena zaka yote ya ng’ombe, au ya kondoo, kila apitaye chini ya fimbo; sehemu ya kumi watakuwa ni watakatifu kwa Bwana…. Haya ndiyo maagizo, Bwana aliyomwagiza Musa kwa ajili ya wana wa Israeli katika mlima Sinai” (Walawi 27: 30, 32, 34).

Tunapotoa zaka, Mungu anatarajia kuwa tutaleta iliyokamilika kulingana na maelekezo yake. “Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la” (Malaki 3:10). Mungu anaruhusu tumjaribu katika swala hili la utoaji wa zaka. Anajua siku tutakapojaribu hatutaacha kutoa. Tutagundua kuwa “. . . Ni heri kutoa kuliko kupokea” (Matendo 20:35).

 Wale wanaozuia zaka na sadaka Mungu anawaita wezi na waliolaaniwa “Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote” (Malaki 3: 8-9).

Kuzuia zaka ya Mungu ni zaidi ya kuiba bali ni kumnyang’anya Mungu. Ni wanyang’anyi kwa kuwa kwa kawaida, wizi ni kitendo kinachofanyika kwa siri wakati ambapo mwenye mali hana habari. Lakini, unapozuia zaka, Mungu anakuona maana hakuna kitu ambacho mwanadamu anaweza kufanya wakati wowote halafu Mungu asijue.

Utoaji wa zaka ni kitendo cha utii na utambuzi wa kwamba yeye ni mmiliki wa mali na maisha yetu kwa kuwa “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake (Zaburi 24:1). Ni ukweli ulio wazi kuwa mali tulizo nazo tumezipata kwa kutumia nguvu, maarifa, na muda ambavyo vyote tumepewa na Mungu.

Kwa mantiki hiyo, basi Mungu ndiye mwenye mchango mkubwa katika mali tulizo nazo. Hivyo, yatupasa kumkumbuka Mungu kama neno linavyoelekeza “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo” (Kumbukumbu la Torati 8:18).

Pamoja na Mungu kuwa mbia mkubwa katika mali zetu, lakini anatuachia sisi tuchukue sehemu kubwa ya mali hizo.  Kwa hali ya kawaida, unapofanya shughuli ya ubia, faida inayopatikana inagawanywa kulingana na mchango wa kila mtu. Anayechangia kidogo anapata kidogo na anayechangia kikubwa anapata kikubwa. Huo ndiyo ubia wa hapa duniani. Lakini ubia wa Mungu na mwanadamu ni tofauti, anayechangia kidogo anapewa kingi! Lakini cha ajabu ni kwamba linapokuja suala la utoaji wa zaka, wengi wetu tunataka tuchukue asilimia zote wakati tumechangia kidogo!

Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu dhana ya utoaji wa zaka?

Hapa nimekueleza kwa kifupi sana kuhusu fundisho la Biblia juu ya utoaji zaka. Yapo mambo mengi ya kujifunza kuhusu fundisho hili. Baadhi ya mambo hayo ni kama vile zaka inatofautianaje na sadaka? zaka inatolewa wapi na kwa nani? Je, kwa waaajiriwa, zaka inatolewa kwenye mshahara wote kabla ya makato (gross salary) au baada ya makato (net salary)? Kwa wafanyabiashara je, zaka inatolewa kwenye faida au kwenye mapato  yote kabla ya faida? Je, zaka inatumiwaje?

Jambo jingine linalofundishwa na wengi kuhusu zaka na matoleo mengine kama vile sadaka ni kwamba ukitoa zaka au sadaka unabarikiwa na usipotoa unalaaniwa. Hata hivyo, fundisho hili lina ukweli kiasi tu lakini kwa sehemu kubwa ni fundisho potofu na haliungwi mkono na Biblia.

Majibu ya maswali yote haya na mengineyo yamechambuliwa kwa kina kwenye kitabu kiitwacho Siri za Mafanikio ya kifedha kwa Mkristo: Elimu isiyofundishwa Shuleni.

Kwa nini usijipatie nakala ya kitabu hiki? Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

Vilevile, kama unapenda kupata mafunzo endelevu kuhusu fedha na masuala mengine ya mafanikio kwa muktadha wa kikristo, unaweza kujiunga na mtandao wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio. Katika mtandao huu utapata maarifa mazuri katika maeneo ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), malezi ya watoto na mambo mengine mengi.

Kujiunga na mtandao huu jaza fomu hii hapa chini.

About Devotha Shimbe

Devotha Shimbe ni Mwalimu na mwanasaikolojia. Amepata pia mafunzo ya Theolojia. Devotha amejitoa kumtumikia Mungu katika maisha yake yote na amekuwa akifundisha na kutoa semina mbalimbali kuhusu mahusiano na maisha ya kiroho kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *