Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuandaa Kichwa Kizuri cha Hubiri Lako

Rafiki yangu Mpendwa Katika Kristo,

Kichwa cha hubiri ni kitu muhimu sana katika hubiri. Pamoja na kuwa muhimu, baadhi ya wahubiri wa injili wana mtazamo kuwa kichwa cha hubiri siyo kitu cha msingi sana katika maandalizi ya hubiri. Ndiyo maana baadhi ya wahubiri huwa hawana kichwa cha hubiri.

Kwa nini kichwa cha hubiri ni muhimu?

Kichwa cha hubiri ni muhimu katika kulitambulisha hubiri.

Kichwa cha hubiri husaidia kuliuza hubiri lako na kinaweza kuwafanya watu wavutiwe au wasivutiwe na hubiri mwanzoni kabisa mwa hubiri lako. 

Kuhubiri bila kuwa na kichwa cha hubiri ni sawa na kuandika kitabu bila kuwa na jina la kitabu!

Kwa umuhimu huu, kichwa cha hubiri, siyo kitu cha kupuuza. Hivyo, kila mhubiri anapaswa kuelewa namna anavyoweza kuwa na kichwa kizuri cha hubiri.

Nini Tofauti Kati ya Mada ya Hubiri, Wazo Kuu la Hubiri na Kichwa cha Hubiri

Yapo mambo kadhaa ya kuzingatia ili uweze kuwa na kichwa kizuri cha kubiri. Lakini kabla ya kukushirikisha mambo hayo, naomba nikushirikishe kwanza mambo matatu yayotambulisha hubiri lako.Mambo hayo ambayo unahitaji kuyafahamu na kuyatofautisha ni mada ya hubiri, wazo kuu la hubiri na kichwa cha hubiri

Mada ya Hubiri ni somo kwa ujumla, yaani hubiri linahusu jambo gani. Kichwa cha Hubiri ni jina unalolipatia hubiri lako.

Wazo Kuu katika hubiri ni kile unachoenda kusema kuhusu somo lako. Kwa maneno mengine, ni kile unachohubiri kama ukikieleza kwa sentensi moja.

Wazo kuu ndicho hadhira yako wanachotoka nacho au kukumbuka baada ya hubiri. Unaweza kupata wazo kuu wakati unajifunza fungu au  mafungu ya hubiri, si kabla au baada ya hapo.

Mfano wa mada, wazo kuu na kichwa cha hubiri ni kama ifuatavyoi:

Mada: Kusaidia wahitaji

Wazo kuu: Kuwa mkristo ni kuwa tayari kusaidia wahitaji

Kichwa cha hubiri: Yuko wapi msamaria wa leo?

Mambo ya kuzingatia katika kuchagua kichwa cha hubiri

Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia unapochagua kichwa cha hubiri:

  1. Kichwa cha hubiri lazima kivute usikivu wa hadhira. Kichwa cha hubiri ni hubiri lililofunikwa wakati hubiri ni kichwa cha hubiri kilichofunuliwa. Chagua kichwa kitakachowafanya hadhira wavutiwe na hubiri lako.
  2. Sisitiza maandiko: Tunapaswa kuhubiri maandiko, siyo mawazo yetu. Hivyo ujumbe wa hubiri, ikiwa pamoja na kichwa chake, lazima vitoe kipaumbele kwenye maandiko. Kichwa cha hubiri kitokane na maandiko na siyo mawazo yetu.Hivyo,chagua kichwa cha hubiri kutoka kwenye maandiko utakayotumia. Usichague maandiko utakayotumia kutoka kwenye kichwa cha hubiri.
  3. Kichwa cha hubiri kiwe rahisi kueleweka kwa hadhira. Kichwa cha hubiri ni kwa ajili ya hadhira na siyo kwa ajili yako. Hivyo chagua kichwa kinachoeleweka kwao na si kwako pekee. Usitumie maneno magumu bila sababu ya msingi. Kumbuka wasipolewa kichwa cha hubiri unaweza kuwa ndiyo mwanzo wa kupoteza usikivu wa hadhira yako.
  4. Kiwe kifupi. Kwa kawaida, kinatakiwa kisizidi maneno saba. Hata hivyo, kisiwe kifupi sana kiasi cha kupoteza mwelekeo wa ujumbe unaokusudiwa. Kwa mfano, kichwa cha hubiri chenye neno moja hakifai.
  5. Tumia maneno yenye staha. Epuka kutumia maneno yasiyo rasmi au yasiyo ya staha. Kwa mfano, niliwahi kumsikia mhubiri mmoja kanisani, akisema kichwa cha hubiri lake ni “Bro Yesu na masela wake walipokula Pasaka”. Neno masela alilitumia kumaanisha wanafunzi wa Yesu 12 na neno Bro lilimaanisha kifupincha bother, yaani kaka . Neno “masela” na masela ni Kiswahili cha mtaani, siyo neno rasmi. Si vema kutumia maneno kama hayo kwenye hubiri lako.
  6. Tumia muundo wa aina mbalimbali (hasa kama una hubiri mara kwa mara). Mifano ya miundo unayoweza kutumia ni kama ifuatavyo:
  • Swali: Uko tayari kukutana na Bwana?
  • Tangazo au tamko: Jiandae kukutana na Bwana.
  • Mshangao: Kumbe Yesu anajali kiasi hiki!
  • Matumizi maishani: Namna ya Kushinda Majaribu
  • Nukuu za Biblia. Kwa mfano:
  • “Chagueni hivi leo mtakayemtumikia” (Yoshua 24:15),
  • “Siku ya wokovu ni sasa” (2 Wakorintho 6:2),
  • “Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini?”(1 Waf. 18:21)
  • “Mjue sana Mungu ili uwe na Amani” (Ayubu 22:21)
  • Mchanganyiko. Kwa mfano:
  • Maisha ya Kikristo: Changamoto na uzuri wake,
  • Siku ya hukumu: Je, unaisubiriaje?

Je, Ungependa Kujifunza Zaidi Kuhusu Mada hii?

Haya ndiyo baadhi ya mambo ya kuzingatia unapoandaa kichwa cha hubiri yako. Kama unataka kwa kina kuhusu mada hii na mambo mengijen kuhusu  namna ya kuandaa na kuwasilisha mahubiri kwa yenye mvuto kwa hadhira, unaweza kujipatia kitabu kizuri kiitwacho Homilia kwa Walei: Ustadi wa Kuandaa na Kuwasilisha Mahubiri.

Kitabu hiki kimeandikwa kwa namna ambayo ni rahisi kueleweka kwa kila mtu kikimlenga hasa yule asiye na elimu ya Teolojia. Kitabu hiki kinawafaa watu wote wanaohubiri Neno la Mungu katika maeneo mbalimbali kama vile katika ibada ya kawaida kanisani, ibada maalum za kanisani kama vile ibada ya maombi katikati ya juma, mikutano ya uamsho na majuma ya maombi, mahubiri ya hadhara na matukio mengine ambapo mahubiri hutolewa.

Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na Email: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

Je, unataka kupata mafunzo endelevu kuhusu mafaniko kwa mkristo?

Kama unataka kuendelea kujifunza kuhusu masuala mbalimbali juu ya mafanikio kwa mkristo unaweza kujiunga na mtandao huu ili uweze kupata makala mbalimbali. Kwa kufanya hivyo, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa katika mtandao huu.

Ili kujiunga, jaza fomu iliyoko hapa chini.

About Devotha Shimbe

Devotha Shimbe ni Mwalimu na mwanasaikolojia. Amepata pia mafunzo ya Theolojia. Devotha amejitoa kumtumikia Mungu katika maisha yake yote na amekuwa akifundisha na kutoa semina mbalimbali kuhusu mahusiano na maisha ya kiroho kwa ujumla.

1 comment / Add your comment below

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *