Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuwafundisha Watoto Wako Elimu ya Fedha

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Watoto ni zawadi, thawabu na urithi kutoka kwa Mungu (Zaburi 127:3). Baada ya wana wa Israeli kutoka katika nchi ya Misri, Mungu aliwapa maelekezo mahususi tena kwa kurudiarudia kuhusu kuwafundisha watoto wao kile alichokuwa amewafundisha (Kumbukumbu la Torati 4:9-10, 40; 5:29; 6:2-9; 11:18-21). Bila shaka, Mungu alitaka mafanikio yanayotokana na kuzingatia mafundisho ya Mungu yasiishie kwao tu bali yarithishwe katika vizazi na vizazi. Sisi kama wana wa Israeli wa kiroho, maelekezo waliyopewa wana wa Israeli yanatuhusu pia.

Fedha ni kitu muhimu sana katika maisha ya mwanadamu yeyote. Kwa kuwa fedha ni muhimu, wanadamu wanapaswa kuwa na elimu sahihi kuhusu fedha ili waweze kuitafuta, kuitumia na kuiongeza kwa namna iliyo sahihi, inayomtukuza Mungu na hivyo kuepuka changamoto za kifedha. Pamoja na umuhimu huu, elimu ya fedha haifundishwi ipasavyo shuleni, nyumbani na kanisani kwa usahihi wake na kuna wasomi wasio na elimu ya fedha. Hali hii imesababisha hali mbaya ya kifedha kwa watu wengi wakiwemo wasomi.

Kutokana elimu ya fedha kutofundishwa nyumbani, shuleni na makanisani, kuna haja kubwa ya kurekebisha hali hii kwa mzazi kuchukua jukumu hili yeye mwenyewe na kuwafundisha watoto wake. Si vibaya kuwapeleka watoto shule lakini tutambue kuwa elimu ya shuleni haiwaandai watoto kwa ajili ya maisha halisi katika ukamilifu wake baada ya masomo bali inawaandaa kwa kitu kimoja tu, yaani kuajiriwa. Nje ya ajira, elimu ya darasani ina msaada kidogo sana kuhusiana na masuala ya kifedha. Kwa kuwa elimu ya darasani inawaandaa wahitimu kwa sehemu kubwa kuajiriwa, wazazi, walezi, walimu na jamii kwa ujumla tumekuwa tukiwaambia watoto kwenda shule, wasome kwa bidii ili wafaulu na kupata kazi nzuri itakayowawezesha kuishi maisha mazuri. Matokeo yake, wengi wa wahitimu wa elimu katika ngazi yoyote, wameshindwa kabisa kuhusisha ufaulu wao wa darasani na mafanikio yao baada ya kumaliza shule.

Mungu katika neno lake anaelekeza “Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako” (Mithali 4:13). Kama kuna elimu muhimu katika maisha ya duniani na ambayo ni lazima tuikamate  sana ni elimu ya fedha. Bila kujali utasoma fani gani katika elimu ya darasani, bila kujali ulifaulu kiasi gani katika fani yako, bila elimu ya fedha huwezi kupata mafanikio ya kifedha. Unaweza ukapata fedha lakini usiwe na mafanikio ya kifedha. Ili ufikie utajiri na uhuru wa kifedha, lazima uwe na elimu sahihi ya fedha.

Baadhi ya migogoro ya kifedha katika ndoa na familia husababishwa na mtazamo tofauti au mitazamo isiyo sahihi kuhusu fedha. Kuwafundisha watoto elimu ya fedha wakiwa wadogo, kutawasaidia kuepuka migogoro hiyo na kuwa na ndoa zenye amani na mafanikio ya katika Nyanja mbalimbali ikiwemo eneo la fedha.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa kile unachowapa watoto wako katika umri mdogo ndicho kitakuwa maisha yao ya baadaye ya kiroho, kijamii, kimwili na kadhalika. Kwa sababu hiyo, yatupasa kuwekeza nguvu zetu katika kuwajengea watoto msingi mzuri wa mambo mbalimbali ikiwemo elimu ya fedha. Kama tutasubiri wawe watu wazima ndiyo tuwafundishe elimu ya fedha, tutakuwa tumechelewa.

Umri gani Tuanze Kuwafundisha Watoto Elimu ya Fedha?

Hakuna umri mahususi ambao umethibitishwa kuwa mtoto anaweza kuanza kufundishwa elimu ya fedha. Kwa sababu hiyo, ni wajibu wa mzazi kuamua ni katika umri upi aanze kumfundisha mtoto wake masuala ya fedha kutegemeana na uelewa wa mtoto huyo na namna anavyoendesha maisha yake. Baadhi ya wataalam hushauri kuwa mtoto anaweza kuanza kufundishwa masuala ya fedha pale atakapojua fedha na kuzitofautisha fedha au sarafu moja na nyingine. Kwa upande wa wanasaikolojia, wao wanatueleza kuwa kuna umri fulani wa mtoto ambapo unapaswa kumjengea mtoto wako msingi muhimu wa maisha iwe misingi ya imani ya dini na mambo mengine. Kipindi hicho, kwa mujibu wa wanasaikolojia ni kuanzia miaka 9 mpaka miaka 15 kwa watoto wa kiume lakini kwa watoto wa kike ni chini ya umri huo kwa sababu wao wanakua haraka zaidi kiakili kuliko watoto wa kiume. Elimu ya msingi kuhusu fedha kwa watoto inapaswa kuwa imeshaanza kwenye umri huo.

Namna ya Kuwafundisha Watoto Elimu ya Fedha

Kufundisha watoto masuala ya fedha ni kazi rahisi sana na ya kuvutia kuliko ambavyo inaweza kufikiriwa. Kazi hii inaweza kufanyika kwa kuwashirikisha watoto masuala mbalimbali kuhusu fedha. Hili linaweza kufanyika katika maisha ya kila siku kupitia mazungumzo na vitendo kwa kutumia kanuni za kibiblia na zisizo za kibiblia zisizopingana na misingi ya Biblia.

Mambo Gani Tuwafundishe Watoto Kuhusu Fedha?

Baadhi ya mambo muhimu ambayo watoto wanapaswa kufundishwa tangu utoto ili kuwajengea msingi imara wa namna ya kusimamia fedha ni pamoja na ukweli kwamba Fedha na mali zingine ni vya Bwana. Mambo mengine  ni kufanya kazi, utoaji (zaka na  sadaka Mungu, misaada na michango kwa ndugu jamaa, marafiki na jamii na kodi kwa serikali), upangaji wa bajeti na mtazamo chanya kuhusu fedha. Mambo mengine ni biashara na uwekezaji,  uwekaji wa akiba, Nidhamu ya matumizi ya fedha, uwekaji wa malengo (kuishi kwa malengo) na mambo mengine mengi.

Ungependa Kujifunza Zaidi Juu ya Namna ya Kuwafundisha Watoto Elimu ya Fedha?

Rafiki yangu mpendwa, huenda bado una maswali mengi kuhusu namna unavyoweza kuwafundisha watoto elimu ya fedha maana hapa nimekudokezea kidogo tu. Kama ndivyo, nakushauri upate vitabu vyetu kuhusu fedha ili uweze kupata maarifa haya kwa kina.

Vitabu hivyo ni kama ifuatavyo:

  1. Siri za Mafanikio ya kifedha kwa wakristo: Elimu ya Fedha isiyofundishwa Shuleni. Katika kitabu hiki utajifunza mengi kuhusu fedha, biashara na uwekezaji. Maarifa haya yatakusaidia kumfundisha motto wako elimu ya fedha.
  2. Siri za Mafanikio ya kifedha Katika Ndoa na Familia: Kanuni za Kibiblia na Kiuchumi za Kukabiliana na Changamoto na Migogoro ya Kifedha Katika Ndoa na Familia. Kitabu hiki kina mambo mengi ya msingi kuhusu elimu ya fedha kwa wana ndoa na wanafamilia wakiwemo watoto. Kitabu hiki kimeeleza kwa kina namna unavyoweza kuwafundisha watoto wako elimu ya fedha.

Ili kupata vitabu hivi, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

Je, unataka kupata mafunzo endelevu kuhusu mafanikio kwa mkristo?

Kama unataka kuendelea kujifunza kuhusu masuala mbalimbali juu ya mafanikio kwa mkristo unaweza kujiunga na mtandao huu ili uweze kupata makala mbalimbali kuhusu masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), maisha ya kikristo, malezi ya watoto na mengine mengi. Kwa kufanya hivyo, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa katika mtandao huu.

Ili kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini.

About Devotha Shimbe

Devotha Shimbe ni Mwalimu na mwanasaikolojia. Amepata pia mafunzo ya Theolojia. Devotha amejitoa kumtumikia Mungu katika maisha yake yote na amekuwa akifundisha na kutoa semina mbalimbali kuhusu mahusiano na maisha ya kiroho kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *