Kama Unataka Usife Mapema Baada ya Kustaafu, Soma Hapa

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Hivi umeshawahi kujiuliza, ikitokea umestaafu na ukacheleweshewa mafao yako kwa muda wa miezi sita au zaidi, maisha yako na ya familia yako yatakuwaje?

Swali jingine, ambalo nakuomba ujiulize ni hili: Unajua kwamba pensheni utakayokuwa unalipwa kila mwezi baada ya kustaafu ni ndogo kuliko mshahara wako wa sasa? Kama unajua, je, uko tayari kuishi kwa kipato kidogo baada ya kustaafu kuliko kipato chako cha sasa? Je, umeandaa njia mbadala ya kukabiliana na kushuka kwa kipato baada ya kustaafu? Kwa uliyejiajiri, unajua kuwa na wewe kuna siku utapaswa kustaafu?

Watu wengi ambao hawajawahi kujiuliza maswali haya au wamejiuliza lakini wakapuuza kufanyia kazi majibu yao, wamekuwa wakijuta baada ya kustaafu baada ya kukutana na maisha magumu baada ya kustaafu. Kwa sababu ya changamoto zinazowakuta wastaafu, wengi wao hufa miaka michache tu baada ya kustaafu. Kama utajiuliza maswali haya na kufanyia kazi majibu yake, utaepuka changamoto hizo za wastaafu na utaepuka kifo kisicho cha lazima baada ya kustaafu. Kama ulikuwa hujajiuliza maswali haya au umewahi kujiuliza lakini hukuchukua hatua yoyote, fuatana nami katika makala haya ili nikukumbushe mambo kadhaa kuhusu maisha baada ya kustaafu.

Kustaafu Kunamhusu Nani?

Kustaafu ni hatua ambayo mtu anafikia ukomo wa uwezo wa kufanya kazi au anakoma kuwa mfanyakazi wa muda wote wa kazi. Watu hustaafu kutokana na muda stahiki wa kustaafu kutimia, uamuzi wa hiari, maradhi au kuachishwa kazi na ukakosa fursa ya kuajiriwa tena.

Ni vema ieleweka hapa kuwa suala la kustaafu haliwahusu walioajiriwa tu bali hata waliojiajiri au wanaofanya shughuli zao binafsi kama vile biashara, kilimo, ufugaji na uvuvi. Bila kujali umeajiriwa au umejiajiri, kuna siku utakuwa na umri ambao hautaweza kufanya kazi na itabidi upumzike kufanya kazi. Hata kama hautapumzika kufanya kazi lakini nguvu zitapungua na utashindwa kufanya baadhi ya majukumu yako kama kawaida. Hivyo, kustaafu ni kitu ambacho hakiepukiki na kwa sababu hiyo kila mtu ni vyema kuwa na mpango wa kustaafu katika shughuli yoyote anayoifanya.

Kwa yule aliyeajiriwa, baada kustaafu anastahili kupewa mafao ambayo hujumuisha stahili mbalimbali ikiwemo pensheni. Pensheni ni malipo maalum anayolipwa mtu kipindi anastaafu. Malipo hayo hutokana na michango yake kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii aliyochangia wakati akiwa kazini na kiasi kingine huchangiwa na mwajiri wake. Malipo hayo hulipwa kwa mstaafu kama Pensheni kulingana na muda aliotumikia na kiwango cha mshahara kipindi anapostaafu. Kwa mtu aliyejiajiri, hapati mafao yoyote ya kustaafu.

Iwe umeajiriwa au umejiajiri, kustaafu kunaweza kuambatana na kushuka kwa kipato. Kwa sababu hiyo kuna kila sababu ya kujiandaa kwa ajili ya kustaafu ili uweze kuendelea na maisha yaleyale au maisha bora zaidi kuliko uliyokuwa unaishi kabla ya kustaafu. Bila kujali umeajiriwa au umejiajiri, ni vema kuwa na mpango wako binafsi wa kustaafu.

Kwa wale walioajiriwa, ni muhimu kuwa na mpango wako binafsi wa kustaafu badala ya kutegemea kulipwa mafao. Mpango wako binafsi wa kustaafu unaweza kukusaidia kutoshuka kwa kipato chako baada ya kustaafu maana zaidi ya mafao unayolipwa utakuwa pia na kipato kingine kutoka kwenye mpango wako wa kustaafu. Mpango huu utakusaidia pia kuepuka changamoto zinazoikumba mifuko ya hifadhi za jamii kwa sasa na kushindwa kumudu gharama za maisha utakapostaafu. Tumeshuhudia katika siku za hivi karibuni, mifuko ya hifadhi ya jamii inakumbwa na changamoto nyingi na kusababisha wastaafu kucheleweshewa mafao yao. Changamoto hii inasababishwa na mambo mengi ikiwa pamoja na faida ya uwekezaji uliofanywa na mifuko kuwa ndogo kuliko mahitaji ya mafao kwa watu waliostaafu. Pia idadi ya watu wanaostaafu ni kubwa ukilinganisha na uwezo wa mifuko hiyo wa kuwalipa. Hata kama utalipwa mafao yako kwa muda, bado mafao hayo hayakuwezeshi kuishi katika ubora wa maisha uleule uliokuwa nao kabla ya kustaafu. Kutokana na changamoto hizi ni muhimu kuwa na mpango wako binafsi wa kustaafu.

Kustaafu si Tukio ni Mchakato

Isivyo bahati, watu wengi wanachukulia suala la kustaafu kama tukio la siku moja, yaani, ni tukio la siku unapoagwa na wafanyakazi wenzako baada ya kufikia umri wa kustaafu. Na kwa mtazamo huu, watu wengi huanza kujipanga na maisha ya kustaafu baada ya tukio hili. Matokeo yake ndiyo yanawakuta ya mzee Nyanda. Kwa mtu makini anayeona mbali, kustaafu siyo tukio bali ni mchakato unaohusisha mtu kujiandaa kuachana na maisha ya ajira au shughuli zake nyingine za sasa na kuanzisha maisha binafsi, yanayotarajiwa kuwa yenye staha na mafanikio.

Maandalizi ya Kustaafu Huanza Siku Unapoanza Kazi

Kila mmoja anahitaji kupanga kustaafu mapema kadiri iwezekanavyo. Ni muhimu kujiuliza mwenyewe ni kiasi gani cha kipato ungehitaji wakati wa kustaafu ili kuweza kumudu gharama za maisha na familia yako. Kama upo katika mpango wa pensheni itakuwa nyongeza nzuri kwako katika kustaafu au kipato cha kustaafu. Kupanga mapema kwa kuweka akiba, kufanya biashara na kuwekeza kwa busara kutakuwezesha kutimiza mahitaji yako wakati ukiwa mstaafu.

Maandalizi ya kustaafu yanapaswa kuanza mara tu mtu anapoanza kazi yake iwe ya kuajiriwa au ya kujiajiri. Mara tu unapoanza kazi, unapaswa kujua kuwa kuna siku utastaafu na hivyo unaanza kupanga unataka uwe na maisha ya aina gani baada ya kustaafu. Zaidi ya kupanga aina ya maisha unayopaswa kuwa nayo, unapaswa kupanga unataka kustaafu ukiwa na umri gani.

Kwa kawaida, umri wa kustaafu kwa walioajiriwa unatajwa na sheria za nchi au sera na taratibu za mwajiri. Kwa mfano, hapa Tanzania, umri wa kustaafu kwa watumishi wa serikali ni miaka 55 kwa hiari na miaka 60 kwa lazima. Hata hivyo, wataalam wachache kama vile wahadhiri waandamizi na maprofesa wa taasisi za elimu ya juu na madaktari bingwa umri wao wa kustaafu ni miaka 60 kwa hiari na miaka 65 kwa lazima. Hii haimaanishi kuwa ni lazima kustaafu kwa mujibu wa sheria au taratibu hizo. Unaweza kuamua kustaafu katika umri wowote utakaochagua wewe.

Baada ya kuamua unataka ustaafu ukiwa na umri gani, ndipo sasa unapanga mambo yako vizuri ili kufikia umri huo uwe na aina gani ya maisha na unaanza maandalizi mara moja bila kusubiri. Usipojiandaa vizuri, utatamani siku ya kustaafu isifike ili usidhalilike. Lakini ukijiandaa vizuri utatamani siku hiyo ifike mapema ili ukafurahie maisha uliyoyaandaa. Ukijiandaa vizuri utakuwa na ujasiri wa kustaafu hata kabla ya umri wa kustaafu kisheria. Lakini kama hukujiandaa, utasubiri ufikishe umri wa kisheria ndipo ustaafu na wapo wengine ambao hudiriki hata kudanganya umri ili mradi tu waendelee na ajira.

Ungependa Kujifunza zaidi Juu ya Namna Unavyoweza Kuijandaa Kustaafu?

Rafiki yangu mpendwa, huenda bado una maswali mengi kuhusu namna unavyoweza kujiandaa kustaafu maana hapa nimekudokezea kidogo tu. Kama ndivyo, nakushauri upate vitabu vyetu kuhusu fedha ili uweze kupata maarifa haya kwa kina.

Vitabu hivyo ni kama ifuatavyo:

  1. Siri za Mafanikio ya kifedha kwa Wakristo: Elimu ya Fedha isiyofundishwa Shuleni.

Katika kitabu hiki utajifunza mengi kuhusu fedha, biashara na uwekezaji. Maarifa haya yatakusaidia kumfundisha motto wako elimu ya fedha.

2. Siri za Mafanikio ya Kifedha Katika Ndoa na Familia: Kanuni za Kibiblia na Kiuchumi za Kukabiliana na Changamoto na Migogoro ya Kifedha Katika Ndoa na Familia.

Kitabu hiki kina mambo mengi ya msingi kuhusu elimu ya fedha kwa wana ndoa na wanafamilia likiwemo saula la kujiandaa kustaafu.

Ili kupata vitabu hivi, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

Je, Unataka Kupata Mafunzo Endelevu Kuhusu Mafanikio kwa Mkristo?

Kama unataka kuendelea kujifunza kuhusu masuala mbalimbali juu ya mafanikio kwa mkristo unaweza kujiunga na mtandao huu wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio ili uweze kupata makala mbalimbali kuhusu masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), maisha ya kikristo, malezi ya watoto na mengine mengi. Kwa kufanya hivyo, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa katika mtandao huu.

Ili kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *