Hivi Ndivyo Mawasiliano Yanavyoweza Kujenga Au Kubomoa Ndoa Yako

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo

“Mimi sielewi nini kimetokea katika ndoa yetu,’’ alisema Kelvin (siyo jina lake halisi) huku akiwa na msongo kubwa wa mawazo. Kabla hatujaoana tulikuwa na mambo mengi ya kuongea. Sasa hatuongei. Kwa upande wa Esta (siyo jina lake halisi) ambaye ni mke wa Kelvin anasema “huwa simwambii chochote, na hivyo hana kitu cha kusikiliza. Havutiwi tena na chochote kinachonivutia mimi”. Hii si changamoto ya ndoa ya Kelvin pekee bali ni hali halisi inayozikabili ndoa nyingi.

Wataalamu wa mambo ya familia hudai kuwa mojawapo ya mambo makubwa yanayochangia wanandoa kugombana na hata kufikia kutengana ni suala zima la mawasiliano katika ndoa. Usahihi wa mawasiliano ni suala moja lakini kupungua au kutokuwepo kwa mawasiliano kabisa ni suala jingine linalopelekea changamoto katika ndoa nyingi.

Mawasiliano ni mchakato wa kupeleka na kupokea ujumbe kupitia njia za maneno au zisizo za maneno ikiwa ni pamoja na mawasiliano ya mdomo, kuandika au mawasiliano ya maandishi, ishara na tabia. Kwa kifupi tunawez kusema, mawasilaino ni mabadishano ya maana. Kuna wakati mtu anaweza kusikiliza lakini asielewe kile kilichokusudiwa na hivyo kupelekea mawasiliano kutokukamilika. Ikimbukwe kuwa mawasiliano hukamilika kwa njia zingine zaidi ya kuongea na kusikiliza kwani mwonekano, matendo, ishara, hisia na kadhalika huweza kufikisha ujumbe kwa mlengwa.

Kwa kawaida tukiwa macho tunatumia takribani 70% ya muda wetu kuwasiliana kwa kuongea, kusikiliza, kuandika na kusoma. Katika muda huu, 33% hutumika katika kuongea na asilimia zingine hubakia kwa mambo mengine. Hivyo, mazungumzo ni muhimu sana katika kuelezea hisia na kuwaleta watu karibu katika mahusiano. Mawasiliano ya kuongea husaidia kufafanua fikra zetu, kuimarisha mawazo, kufahamiana na watu, kuondoa msongo, kutoa maoni na kujenga mahusiano thabiti.

Mawasiliano katika ndoa huweza kukamilika ikiwa wanandoa watazingatia kanuni kuu tatu za mawasiliano kama zinavyopendekezwa na mwandishi Nancy Van Pelt, katika kitabu chake kiitwacho To Have and to Hold. Nancy anasema, mawasiliano katika ndoa huweza kukamilika pale:

  • Yanapozingatia sanaa ya kusikiliza na kuongea kwa usahihi
  • Yanapoweza kutatua matatizo kwa njia za kujenga zaidi kuliko kubomoa
  • Yanapotumika kila siku kuelezea hisia ya mapenzi na ukaribu kati ya wenzi.

Kanuni hizi ni za msingi sana ili kuhakikisha uhai na furaha katika mahusiano ya ndoa.

Vizuizi katika mawasiliano ya kuzungumza

Wakati mwingine mazungumzo huweza kupata vizuizi mbalimbali hata kupelekea mawasiliano kukatika. Vizuizi hivi ni pamoja na matumizi ya maneno yenye kushurutisha. Kama vile toka hapa, fanya haraka.  Mfano mwingine ni matumizi ya maonyo na vitisho. Kwa mfano,  ukirudia kufanya hivyo tena…; Ina maana hujui… na kadhalika. Matumizi ya maneno haya pamoja na ukosoaji usio wenye kujenga, lawama na maneno ya kejeli au dharau huvunja mnyororo wa mawasiliano kwa kiwango kikubwa sana. Haya humfanya mwenzi kuwa duni na kujiona hafai kabisa. Matokeo yake, mwenzi huyo anaweza kuamua kukaa kimya tu na kuyaacha maisha yajiendee tu.

Vizuizi katika kusikiliza

Kwa mujibu wa wanasaikolojia, udhaifu katika kusikiliza ni mojawapo ya kikwazo kikubwa katika changamoto za mawasiliano kwa wanandoa. Hata kama kuna mbinu bora kiasi gani zinazoweza kutumika kutafuta suluhu, kuleta maridhiano kihisia na kuondoa kutokuelewana, ikiwa zitakumbana na msikilizaji mbovu haziwezi kuleta ufanisi.

Ili kudumisha maelewano katika ndoa, wanandoa wanapaswa kuzingatai ushauri ufuatao kutoka katika Neno la Mungu: “Hayo mnayajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika; kwa maana hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu (Yakobo 1: 19 – 20).

Ushauri huu ni wa muhimu kwa sababu wengi wetu hupenda kuongea kuliko kusikiliza na kuelezea hisia zetu na kutoa mawazo na matamanio yetu bila kujali kupokea kutoka kwa wengine. Watu wa aina hii wanapokutana na mtu mwenye mtazamo tofauti na wao mabishano na malumbano yanaweza kutokea maana hawawezi kumsikiliza ili kuelewa bali husikiliza ili kujibu hoja.  Watu wa aina hii ni wasikilizaji wabovu.

Je, ungependa kujifunza zaidi kuhusu mada hii?

Kama unataka kuendelea kujifunza zaidi kuhusu mada hii, unaweza kujiunga na mtandao huu wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio ili uweze kupata makala mbalimbali zitakazokusaidia kuboresha mahusiano yako iwe mahusiano ya ndoa au uchumba au mahusiano mengine katika familia, maeneo ya kazi na katika jamii kwa ujumla.

Zaidi ya kujifunza kuhusu mahusiano, utapata pia makala juu ya masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, maisha ya kikristo, malezi ya watoto na mengine mengi. Kwa juinga na mtandao huu, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa.

Ili kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini.

About Devotha Shimbe

Devotha Shimbe ni Mwalimu na mwanasaikolojia. Amepata pia mafunzo ya Theolojia. Devotha amejitoa kumtumikia Mungu katika maisha yake yote na amekuwa akifundisha na kutoa semina mbalimbali kuhusu mahusiano na maisha ya kiroho kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *