Biblia Inasemaje kuhusu Mafundisho ya Injili ya Mafanikio?

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Kutokana na ongezeko la madhehebu ya Kikristo hapa nchini na duniani kwa ujumla, kumekuwa pia na ongezeko la mafundisho ya kila aina kuhusu masuala mbalimbali ya imani ikiwemo suala la mafanikio ya kiuchumi. Baadhi ya wahubiri wamekuwa na ujumbe rahisi: Mungu anataka kukubariki, na ushahidi wa baraka hiyo ni kuwa na mali nyingi. Kwa maneno mengine, kama wewe ni mwaminifu kwa Mungu, Mungu atakupatia utajiri wa kutosha au afya nzuri.  Dhana hii ndiyo inaitwa Injili ya mafanikio au Injili ya utajirisho (prosperity gospel).  Kwa Injili hii, ukimwamini Yesu, anakufanya kuwa tajiri wa vitu na atakupatia afya njema.

Preacher icon. Vector illustration

Injili ya mafanikio inaonekana kushamiri sana hasa katika makanisa yanayojiita “makanisa ya kiroho”. Msingi wa Injili hii si kumwamini Yesu tu bali ni katika utoaji wa zaka na sadaka. Injili ya mafanikio inawataka waumini kutoa zaka na sadaka ili waweze kupata mafanikio ya kiuchumi na wasipotoa hawawezi kupata mafanikio hayo. Kwa maneno mengine, mafanikio ya kifedha  na kiafya yanategemea utoaji wako.

Wahubiri wengi wa makanisa ya kiroho wamejipatia utajiri wa kutisha kwa kuwahamasisha waumini wao kutoa zaka na sadaka kwa ahadi kwamba wataweza kupata mafanikio ya kifedha baada ya kutoa. Mara nyingi sehemu kubwa ya zaka na sadaka zinazotolewa huwa zinatumiwa na wahubiri hao kwa mambo yao binafsi. Baadhi ya mafungu ya Biblia  yanayotumiwa na wahubiri hao ni “Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi ; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la” (Malaki 3 :10). Kwa kutumia mafungu ya Biblia, wahubiri hawa wamekuwa wakiwaambia waumini wao kwamba wanaweza hata wakachagua aina ya baraka wanayotaka kuipata kutoka kwa Mungu. Baadhi ya baraka hizo ni pamoja na gari, kazi, fedha, kupona ugonjwa, aina ya biashara na kadhalika. Yote haya waumini wanaambiwa kuwa wanaweza kuyapata kwa kumjaribu Mungu kupitia utoaji. Ikitokea muumini ametoa zaka na sadaka halafu asipate mafanikio aliyotarajia, lawama humwangukia yeye mwenyewe kuwa hana imani ya kutosha.

Wasemavyo Wahubiri wa Injili ya Mafanikio 

Hebu tuangalie baadhi ya maneno ya baadhi ya viongozi wa makanisa yanayohubiri Injili ya mafanikio. Mwanzilishi wa kanisa la Universal Church of the Kingdom of God lenye makao makuu mjini Sao Paulo, Brazil Askofu Edir Macedo anaeleza kuwa zaka na sadaka ni njia nzuri ya uwekezaji wa kifedha. Katika kitabu chake alichoandika kwa lugha ya kireno kiitwacho Vida Com Abundância (Maisha Tele) uk.79, Macedo anadai kuwa “Kwa mujibu wa Biblia, kulipa zaka maana yake ni kuwa mtaradhia wa mibaraka ya kimwili, kiroho na kifedha isiyo na kikomo. Tunapolipa zaka kwa Mungu, anakuwa na deni (kwa sababu aliahidi) la kutimiza Neno lake, kukemea mapepo mabaya yanayoharibu maisha ya mwanadamu na kuleta magonjwa, ajali, uraibu, mmomonyoko wa kijamii katika nyanja zote za shughuli za binadamu ambazo zinamfanya ateseke milele. Tunapokuwa waaminifu katika zaka zetu, zaidi ya kuachiliwa kutoka katika mateso hayo, pia tunaanza kufurahia uzima duniani, tukiwa na Mungu upande wetu akitubariki katika kila kitu’’.

Katika kitabu chake kingine kiitwacho “O Poder Sobrenatural da Fé” (Nguvu kuu ya imani) uk. 145 na 147, Macedo anaeleza “ Ni wazi pia kwamba wale walio waaminifu katika zaka zao wana upendeleo wa kudai kutoka kwa Mungu utimizwaji wa ahadi yake katika maisha yao na ni lazima Bwana atimize. Mimi binafsi, ninachukulia kuwa tunapata zaidi ya kile tunachostahili, iwe katika zaka au sadaka, kwa sababu tukitoa zaidi Mungu ataturudishia zaidi’’.

Kwa upande wake aliyekuwa kiongozi na mwanzilishi wa kanisa moja huko Marekani liitwalo Word of Faith Movement marehemuKenneth E. Hagin (1917–2003) anadai kuwa alifunuliwa na Mungu juu ya mafanikio. Katika kijarida chake (pamphlet) kiitwacho How God Taught Me About Prosperity (Namna Mungu alivyonifundisha kuhusu mafanikio) uk.1. Hagin anaeleza kuwa “Bwana mwenyewe alinifundisha kuhusu mafanikio. Sikuwahi kusoma juu ya mafanikio katika kitabu. Nilipata moja kwa moja kutoka mbinguni”.

Mtu mwingine aliyewahi kueleza kuhusu Injili ya mafanikio ni Dkt. Bill Hamon, mwanzilishi wa kanisa la moja la Marekani liitwalo Christian International Ministries. Katika kitabu chake kiitwacho Prophets and Personal Prophecy. Uk.124 na 126, Dkt. Bill Hamon anaeleza kuwa “Roho Mtakatifu ameweka wazi kuwa sasa ni wakati kwa jeshi la Bwana kuinuka na kumiliki utajiri wa ulimwengu”. Kwa mujibu wa kiongozi huyo, “utajiri huu unaweza kupatikana kwa msaada wa manabii wa leo ambao wanaweza kuwaonesha watu juu ya matatizo yanayokwamisha biashara zao, mwelekeo mpya, shughuli na malengo yao. Wafanyabiashara wengi, wanatafuta nabii ili awape uthibitisho kabla ya kufanya maamuzi makubwa katika mambo yao”.

Je, mafundisho haya ni sahihi

Kuna mgawanyiko mkubwa miongoni mwa Wakristo na hata wasio Wakristo kuhusu mafundisho ya injili ya mafanikio. Wapo wanaoyaamini na wengine hawayaamini. Je, nani yuko sahihi kati ya makundi haya mawili? Kujibu swali hili kwa usahihi ni lazima tuiulize Biblia.

Jibu fupi kwa swali hili ni kwamba, injili ya mafanikio ni fundisho la Biblia lakini limepotoshwa sana. Ni kwa namna gani limepotoshwa, endelea kufuatilia makala katika mtandao huu. Mtandao umesheheni makala nzuri  kuhusu masuala mbalimbali kama vile mahusiano (uchumba na ndoa), malezi ya watoto, fedha, biashara na uwekezaji.

Ili usikose makala kutoka katika mtandao huu, unaweza kujiunga na mtandao huu ili uweze kupata makala hizo moja kwa moja kwenye email yako kila zinapowekwa mtandaoni.

Ili kujiunga na mtandao huu , jaza fomu iliyoko hapa chini.

1 comment / Add your comment below

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *