Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Karibu tena katika mfululizo wa makala kuhusu injili ya mafanikio. Hii ni injili maarufu sana na inayopendwa na watu wengi siku hizi. Injili hii inawafundisha watu kuwa ukimwamini Yesu na ukawa mwaminifu kwake utapata mafanikio katika maisha yako. Mafanikio hayo ni pamoja na utajiri wa mali, afya njema na mambo yako kukuendelea vizuri kwa kila jambo unalolifanya. Pamoja na mambo mengine, ili uweze kupata mafanikio, injili hii inasisitiza utoaji wa zaka na sadaka kwa wingi na usipotoa zaka na sadaka utapata laana na hivyo hutaweza kupata mafanikio.
Katika mfululizo wa makala haya tumekuwa tukiangalia injili ya mafanikio ina ukweli kiasi gani kulingana na Bibalia na tumekuwa tukijibu swali hili :Biblia inasemaje kuhusu injili ya mafanikio? Katika makala haya, tunaenda kuangalia namna ambavyo injili ya mafanikio inavyopingana na mafundisho ya Yesu na mitume. Yote haya tutayapata katika Biblia. Karibu tujifunze pamoja.
Kupata makala za nyuma kuhusu mada hii, soma hapa
Mafundisho ya Yesu yanakazia uongofu unaopelekea kujikana nafsi na kujisalimisha kikamilifu kwa Yesu (Mathayo 16:24; Marko 8:34; Luka 9:23). Katika uzoefu huo, wanadamu wadhambi ambao kwa asili ni wabinafsi, wanabadilishwa na kuwa si wabinafsi ambao wanamtanguliza Mungu. Akieleza uzoefu wake binafsi, Mtume Paulo anasema “Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu yeyote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi. Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia. Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani” (Wafilipi 3:4–9).
Wahubiri wa Injili ya mafanikio hujifanya kuhubiri ujumbe unaowataka waumini wao kuishi maisha ya kujitoa na yasiyo ya kibinafsi kwa kutoa zaka na sadaka kwa uaminifu. Kwa juu juu, fundisho la utoaji linaweza kuonekana kama ni fundisho linalolenga kuwafanya waumini wasiwe watu wanaopenda fedha kuliko kumpenda Mungu. Hata hivyo, ukweli ni kwamba, fundisho hili linawafanya waumini kuwa wapenda fedha maana wengi wanatoa si kwa sababu ni wajibu wao kutoa bali wanatoa ili wapate mafanikio kwa kuwa wanaahidiwa kuwa wakitoa watabarikiwa na kupata mafanikio ya kila aina yakiwemo mafanikio ya kifedha.
Zaidi ya kuwajengea ubinafsi na kupenda fedha, Injili ya mafanikio inawajengea waumini tabia ya kujionesha na kujiinua. Hii inatokana na ukweli kwamba wahubiri wa injili hii huhamasisha waumini wao kutoa ushuhuda hadharani juu ya mafanikio waliyoyapata kama matokeo ya utoaji wao. Shuhuda za waumini hao kwa kawaida huelezea kwanza walitoa nini na wakapata mafanikio gani. Mara nyingi, shuhuda hizi hutolewa kupitia televisheni, radio au mikutano ya hadhara.
Hata kama shuhuda hizi zinafanyika kwa nia njema, lakini zinapingana na fundisho la Yesu alilolitoa kupitia kisa cha sadaka ya mwanamke mjane (Marko 12:41–44; Luka 21:1–4) na katika mfano wa farisayo na mtoza ushuru (Luke 18:9–14). Kupitia visa hivi, ni wazi kuwa Yesu hakubaliani na ushuhuda wa kujionesha kwa watu juu ya nini ulichomfanyia Mungu. Badala yake alisistiza usiri na unyenyekevu katika matoleo maana alisema “Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi (Mathayo 6:2–4).
Baadhi ya wahubiri huenda mbali zaidi hata kuwapangia waumini wao aina ya mafanikio yatakayopatikana baada ya kutoa zaka na sadaka na kuwataka wachague aina ya mafanikio wanayoyaka kwa kutoa kiasi cha fedha kinachoendana na mafanikio wanayoyataka. Kama fundisho hili ni la kweli maana yake ni kwamba waumini walio matajiri wataendelea kuwa matajiri na walio maskini wataendelea kuwa maskini. Hii ni kwa sababu matajiri wataweza kutoa fedha nyingi na hivyo kupokea baraka ya fedha nyingi kulingana na utoaji wao wakati maskini watatoa kidogo kulingana na uwezo wao na hivyo kupokea baraka kidogo zinazoendana na fedha waliyotoa. Fundisho hili linamfanya Mungu aonekane anajali matajiri kuliko maskini. Kwa vyovyote vile, Mungu wa aina hii si Mungu aliyeelezwa kwenye Biblia. Mungu tunayemsoma kwenye Biblia ni Mungu mwenye upendo na asiyependelea mtu yeyote kwa sababu yoyote ile (Matendo 10:34).
Endelea kufuatilia mtandao huu ili tuendelee kujifunza pamoja juu ya mtazamo wa Biblia kuhusu funidsho la injili ya mafanikio.
Je, unapenda kupata mafunzo endelevu kutoka katika mtandao huu?
Ili uweze kupata makala kuhusu mada hii na mada zingine kuhusu mafanikio, jiunge na mtandao huu. Kwa kufanya hivyo, utaweza kupata makala hizo moja kwa moja kwenye email yako kila zinapowekwa mtandaoni. Mtandao huu unatoa mafunzo endelevu kuhusu mafanikio hususani kuhusu masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), malezi ya watoto na mambo mengine mengi ya kiroho.
Ili uweze kujiunga, jaza fomu iliyoko hapa chini.
1 comment / Add your comment below