Hivi Ndivyo Unavyoweza Kufundisha na Kuhubiri Watoto kwa kutumia Visa

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Zipo njia nyingi zinazotumika katika kufundisha na kuhubiri watoto wa umri mbalimbali kanisani, nyumbani na katika vipindi vya dini mashuleni. Kati ya njia hizo visa na hadithi ni njia ambayo inatumiwa na walimu na wahubiri wengi wa watoto pengine kuliko njia nyingine zote.

Yesu Kristo mwenyewe alitumia sana visa  kufikisha kwa urahisi ujumbe aliokusudia. Wakati njia zingine za kufundisha zimekuwa zikiibuka na kutoweka, njia ya visa imedumu kwa muda mrefu na haionekani kama inaweza kupitwa na wakati.  Njia ya visa, inaweza kufanyika katika namna mbalimbali kama vile kuigiza kisa cha Biblia, kusimulia kisa cha Biblia, kusimulia kisa kutoka nje ya biblia kama kielelezo cha fungu au mafungu ya Biblia, kusimulia kisa chako kinachokuhusu.

Kwa nini matumizi ya visa ni muhimu katika kufundisha na kuhubiri ?

Kufundisha na kuhubiri kwa njia ya visa, ni njia yenye umuhimu wa pekee katika kuwasaidia watoto kukua katika maadili mazuri. Baadhi ya faida za kutumia visa na  katika kufundisha watoto ni kama ifuatavyo :

  • Hushika na kudumisha usikivu ;
  • Hugusa mihemko ya watoto na kuchochea hisia zao za kina ;
  • Huchochea fikra;
  • Husaidia kumbukumbu;
  • Husaidia darasa kuwa na mtazamo mzuri kiakili;
  • Hufanya ukweli dhahania uwe thabiti na wa kufaa

 Kama mwalimu au mhubiri wa watoto, ni lazima ujue namna ya kuandaa na kusimulia kisa ili kivute usikivu wa watoto.

Namna ya kuandaa na kusimulia kisa

Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia wakati unapoandaa na kutoa kisa kwa watoto:

  1. Chagua kisa: Uchaguzi wa kisa utategemea somo unalotaka kufundisha kwa watoto. Kisa unachokichagua lazima kilenge kuwapa fundisho maalum watoto. Kwa hiyo, kabla ya kuchagua kisa, chagua kwanza somo unalotaka kufundisha. Je, visa utavipata wapi? Visa vizuri unaweza kuvipata kutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na visa vinavyokuhusu wewe mwenyewe. Vyanzo vingine ni Biblia, vitabu mbalimbali maalum kwa ajili ya visa vya watoto, magazeti, kusimuliwa na watu wengine, viumbe vya asili, matukio unayokutana nayo kila siku. Kama kisa chako hakitoki kwenye Biblia, ni lazima usome fungu la Biblia linaloendana na kisa hicho. Kisa kutoka nje ya Biblia kitumike tu kama kielelezo cha fungu au kulifanya fungu lieleweke zaidi na kamwe kisisimame pekee yake. Hata hivyo, kama kisa chako kinatokana na Biblia, kisa hicho kinaweza kusimama chenyewe na si lazima uwe na fungu jingine la kuambatana na kisa hicho.

Ukiwa mwalimu au mhubiri wa watoto, ni vizuri ukajenga utamaduni wa kutembelea maduka ya vitabu vya kikristo au kuwatafuta wauzaji wa vitabu vya kikristo walio katika eneo lako ili uweze kununua vitabu vyenye visa vya kufundishia au kuhubiria watoto. Katika zama hizi, mtandao wa kompyuta unaweza kuwa chanzo kizuri cha visa vya watoto, japo utalazimika kufanya kazi kubwa ya kuvichuja ili upate visa vinavyofaa kwa mafundisho ya kiroho. Unaweza kuwa na daftari maalum kwa ajili ya kuandika visa mbalimbali unavyovipata kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya rejea baadaye.

Kwa kawaida, kisa kizuri huwa kina taarifa za kutosha zinazosaidia kieleweke vizuri na taarifa hizo lazima zijibu maswali sita au baadhi yake. Maswali hayo ni: nini, nani, lini, wapi, kwa nini na kwa namna gani? Maswali haya yanajulikana kama 5W+1H (W tano na H moja), yaani what (nini), who (nani), when (lini), where (wapi), why (kwa nini) na How (kwa namna gani).

Inashauriwa kuwa kila mwalimu au mhubiri wa watoto awe na visa vya akiba ili inapotokea dharura na ikabidi ahubiri au afundishe watoto basi awe tayari kufanya hivyo bila kuathiri ubora wa hubiri au somo. Kwa maneno mengine, mhubiri wa watoto anashauriwa kuwa tayari kila wakati kuhubiri au kufundisha watoto. Kama utaombwa kuhubiri au kufundisha watoto wakati hujajiandaa ni heri ukatae kuliko kukubali halafu ukafundisha au kuhubiri kwa kulipua.

  • Jifunze vizuri kisa ulichokichagua: Kama kisa ulichochagua kimeandikwa, kisome vizuri zaidi ya mara moja ili ukielewe vizuri. Kama hakijaandikwa jaribu kukumbuka vitu muhimu vilivyomo katika kisa hicho kwa mfuatano wake na unaweza kukiandika kwa kifupi. Usikariri maneno yaliyomo kwenye kisa hicho bali kumbuka mtiririko wa kisa ili wakati wa kusimulia utumie maneno yako mwenyewe. Panga mapema utaanzaje kisa na utasimuliaje kila hatua ya kisa na utamalizaje. Kama unadhani unaweza kusahau, andika vitu vichache vya kukusaidia kukumbuka lakini usisome neno kwa neno bali angalia kidogo tu na kisha endelea kusimulia.
  • Fanyia mazoezi kisa kabla ya kukitoa: Kama hauna uzoefu wa kusimulia visa, inashauriwa kufanya zoezi kabla ya kwenda kusimulia kisa ulichokichagua. Fanya zoezi kwa kusimulia watoto wa nyumbani kwako au wa jirani au unaweza kufanya zoezi mbele ya kioo ili ujione unavyofanya. Unaweza pia ukajirekodi na baadaye ukajisikiliza na/au kujiona na kusahihisha makosa utakayoyagundua mapema badala ya kwenda kufanya makosa hayo mbele ya watoto.
  • Kumbuka kuomba: Kwa kuwa kisa chako kitahusisha usomaji wa neno la Mungu, ni muhimu kuomba kabla ya kuanza na baada ya kumaliza somo ili Mungu aweze kukuongoza wewe kuwasilisha ujumbe utakaogusa maisha ya watoto na pia kuwaongoza watoto kuelewa na kupokea ujumbe huo kwa ajili ya kuutumia maishani.
  • Kila mtoto akuone unapotoa kisa: Wakati wa kusimulia kisa, simama au kaa mahali ambapo kila mtoto atakuona na uongee kwa sauti ambayo kila mtoto atakusikia lakini sauti isiwe ya juu kiasi cha kuwakera watoto. Kama utatumia kipaza sauti, hakikisha unajifunza namna ya kukitumia kwa usahihi.  Kwa kadri inavyowezekana, tumia vielelezo vya kufundishia katika kusimulia kisa na itafaa zaidi vielelezo viwe vile vinavyopatikana katika mazingira ya watoto. Hivyo ndivyo Yesu alifanya; alitumia vielelezo vinavyopatikana katika mazingira ya wasikilizaji wake kufikisha ujumbe. Hata kama itabidi kutumia vielelezo visivyopatikana katika mazingira yenu, jiridhishe kuwa vinafahamika kwa watoto au hazitakuwa kikwazo katika kuelewa somo.

Kwa leo naishia hapa. Endelea kufuatilia mtandao huu kwa makala zaidi kuhusu mada hii. Unaweza kujiunga na mtandao huu ili uwe na uhakika wa kupata makala kila zinapowekwa kwenye mtandao huu. Kujiunga, jaza fomu iliyoko chini ya makala haya.

Ungependa Kujifunza zaidi Juu ya Mada hii?

Rafiki yangu mpendwa, huenda bado una maswali mengi kuhusu namna unavyoweza kutumia visa kufundisha na kuhubiri watoto na ungependa kujifunza zaidi. Usiwe na wasiwasi, tuna kitabu mahususi kuhusu mada hii pamoja na mada zingine kuhusu kufundisha na kuhubiri watoto. Kitabu hicho kinaitwa Ustadi wa Kufundisha na Kuhubiri Watoto.

Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

About Devotha Shimbe

Devotha Shimbe ni Mwalimu na mwanasaikolojia. Amepata pia mafunzo ya Theolojia. Devotha amejitoa kumtumikia Mungu katika maisha yake yote na amekuwa akifundisha na kutoa semina mbalimbali kuhusu mahusiano na maisha ya kiroho kwa ujumla.

1 comment / Add your comment below

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *