Biblia inasemanaje kuhusu Injili ya Mafanikio? – 5

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Karibu tena katika mfulululizo wa makala kuhusu injili ya mafanikio. Hadi sasa tumeshambua mafungu mengi yanayobainisha kuwa injili ya mafanikio kama inavyofundishwa na wahubiri wengi inavyopingana na Biblia.

Katika makala haya ya mwisho katika mfulululizo huu tutaangalia namna ambavyo injili ya mafanikio inavyopotosha dhana nzima ya utii wa wanadamu kwa Mungu hususani utii kuhusu utoaji wa zaka na sadaka. Vilevile tutaangalia namna injili ya mafanikio isivyoendana na mwelekeo wa utume katika Agano jipya.

Kupata makala za nyuma soma hapa

Injili ya Mafanikio Inapotoshwa Dhana ya Utii kwa Mungu

Kitabu cha Malaki na Kumbukumbu la Torati sura ya 11 na ya 28, zinazungumzia baraka zinazoendana na uaminifu kwa Mungu. Hata hivyo, ni vizuri ieleweke kuwa baraka hizi si kwa watu waaminifu katika matoleo tu bali kwa wale ambao ni waaminifu kwa Mungu katika mambo yote. Yesu alizungumzia ukweli huu na kusema “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. “Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu” (Mathayo 7:21-23).

Biblia inasisitiza kuwa ni bora kutoa kuliko kupokea. Katika hali ya kawaida  wahubiri wa Injili ya mafanikio wanafundisha kuwa ni vizuri kupokea kuliko kutoa japo hawasemi hili waziwazi. Hii ni kwa sababu wanawaambia waumini wao watoe ili wapate mafanikio. Kwa maneno mengine, msukumo wa utoaji kwa waumini wa Injiili ya mafanikio ni kupokea mafanikio na si vinginevyo. Wahubiri hawa hawajali sana kama waumini wana “mikono safi na moyo mweupe” (Zaburi 24:3-5) au wanaishi “kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu” (Mathayo 4:4), au kama wamemruhusu “Roho wa kweli” awaongoze na kuwatia “kwenye kweli yote” (Yohana 16:13; 1 Yohana 4:1; Matendo 5:32).

Mara nyingi, wahubiri hawa wanataka zaidi kuona waumini wao kama wananena kwa lugha, wanapitia katika uzoefu wa miujiza na kupata mafanikio ya kiuchumi na kimwili.  Kwa mfano, wanataka waumini wao wapate uponyaji wa magonjwa badala ya kuishi kwa kuzingatia kanuni za afya kama biblia inavyotaka. Injili hii ni kama biashara ambayo lengo lake ni kuongeza idadi ya waumini ili wahubiri wapate mapato mengi kupitia zaka na sadaka (1 Wakorintho 3:16, 17; 6:19, 20) na wanahubiri mafanikio ya kitambo badala ya kuhubiri watu waache dhambi ili wapate uzima wa milele (Wakolosai 1:12). Misisitizo wa wahubiri hawa ni “simama uende” badala ya “enenda zako; wala usitende dhambi tena” (Yohana 8:11; 5:14).

injili ya Mafanikio Haiendani na Mwelekeo wa Utume Katika Agano Jipya

Kuna tofauti ya mwelekeo wa kiutume kati ya kanisa la agano la kale na ule wa kanisa la Agano jipya. Katika kanisa la Agano la kale, Mungu alimchagua Ibrahimu na uzao wake ili awafanye taifa kubwa na kuwabariki ili kuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengine. Ilitarajiwa kuwa mataifa mengine wangevutwa kuja kumwabudu Mungu wa Ibrahimu (Mwanzo 12:1–3; 15:13, 14; 22:16–18). Taifa la Israeli walikaribia kufikia hadhi hii wakati wa mfalme Daudi na mfalme Sulemani ambapo mafanikio yao ya kiuchumi na kiroho yaliwafanya wawe kielelezo cha kuigwa na mataifa mengine (1 Wafalme 4 na 10). Hata hivyo, mafanikio haya yalitoweka baada ya uasi na ibada ya sanamu iliyopelekea katika kugawanyika kwa taifa la Israeli kati ya taifa la Kaskazini na taifa la kusini (2 Wafalme 25; 2 Mambo ya Nyakati 36:17–21; Yeremia 39, 52).

Katika Agano jipya, mwelekeo wa utume uligeuka ambapo Wakristo (Waisreli wa kiroho) walitakiwa kutoka na kuwafuata watu wasiomjua Mungu na kuwahubiri Injili (Mathayo 24:14; 28:18–20; Marko 16:15, 16; Luka 24:45–49; Matendo 1:8). Mfumo huu una uhusiano gani na Injili ya mafanikio? Mfumo huu una changamoto kubwa maana mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache (Mathayo 9:37; Luka 10:2). Hivyo, utoaji wa zaka na sadaka unahitajika ili kufanikisha mipango ya utume. Katika Injili ya mafanikio, utoaji unahitajika ili kufanikisha mafanikio ya kiuchumi kwa waumini.

Yesu alisema “Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako (Mathayo 6:19-21). Pamoja na wahubiri wa Injili ya mafanikio kuwahamasisha waumini wao kutokujiwekea hazina duniani na badala yake wajiwekee hazina mbinguni kwa kuwa watoaji lakini kwa upande mwingine ni kama wanawahamasisha waumini hao kujiwekea hazina duniani kwa kuwaahidi baraka za mafanikio ya kila aina katika dunia hii kutokana na utoaji.

Kwa kuhitimisha, ni vizuri ifahamike kuwa tajiri na kupata mafanikio mengine ya kimwili ni mpango wa Mungu (3 Yohana 2). Hata hivyo, mafanikio haya ni lazima yapatikane katika njia zinazoendana na Neno la Mungu. Njia halali ya kujipatia kipato kwa mujibu wa Biblia ni kufanya kazi. Hakuna njia nyingine zaidi ya hii. Muujiza wowote  unaofanyika ili kujipatia fedha na mali zingine ni lazima uhusishe kazi. Muujiza huo usipohusisha kazi basi huo haupatani na Neno la Mungu.

Ili kufanikiwa ni lazima uweke kazi kwa kutumia maarifa, bidii, ubunifu. Usipofanya kazi kwa bidii ,weledi na ubunifu huwezi kupata mafanikio yoyote kwa kutegemea muujiza kupitia mafuta ya upako, maombezi, kunyunyuziwa maji ya baraka, kupanda mbegu kwa kutoa fungu la kumi na sadaka kubwa na vitu kama hivyo. Kama unabisha jaribu kukaa bila kazi halafu uone kama utapata hayo mafanikio. Yaani kazi yako iwe kula, kuomba na kulala tu kisha upate mafuta ya upako, unyunyizwe maji ya baraka, ukemewe kila aina ya mapepo na utimize kwa uaminifu kila aina ya masharti (yasiyohusisha kufanya kazi) unayopewa na kiongozi wako wa dini . Jaribu kufanya hivyo kwa mwezi mzima halafu unishirikishe ushuhuda wa mafanikio uliyopata.  Nina hakika hakuna atakayekuja na ushuhuda wa mafanikio.

Rafiki yangu mpendwa, nimalizie kwa kusema kuwa pamoja na kutafuta mafanikio ya kifedha na kimwili, mafanikio muhimu kuliko yote ambayo Mkristo anatakiwa yawe kipaumbele chake ni kuupata ufalme wa Mungu (Mathayo 6:33) “Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?” (Marko 8:36). “Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa” (Mithali 1:7). Kama tunataka mafanikio, hatuna budi kutafuta maarifa, kufanya kazi kwa bidii, weledi na ubunifu na kasha tumwabudu BWANA katika Roho na kweli. Kwa kufanya hivyo hakuna namna utakosa mafanikio katika mambo yetu ikiwa pamoja na mafanikio ya kiuchumi.

Je, unapenda kupata mafunzo endelevu kutoka katika mtandao huu?

Ili uweze kupata makala kuhusu mada hii na mada zingine kuhusu mafanikio, jiunge na mtandao huu. Kwa kufanya hivyo, utaweza  kupata makala hizo moja kwa moja kwenye email yako kila zinapowekwa mtandaoni. Mtandao huu unatoa mafunzo endelevu kuhusu mafanikio hususani kuhusu masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), malezi ya watoto na mambo mengine mengi ya kiroho.

Ili uweze kujiunga, jaza fomu iliyoko hapa chini.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *