Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Naomba nikukaribishe katika mwendelezo wa makala kuhusu matumizi ya visa katika kufundisha na kuhubiri watoto. Katika sehemu iliyopita, tuliona mambo muhimu matano ya kuzingatia unapofunidsha au kuhubiri kwa kutumia visa.
Kusoma makala iliyotangulia, bonyeza hapa
Leo, naomba nikushirikishe mambo mengine muhimu. Mambo hayo ni kama ifuatavyo:
- Fahamu hadhira yako: Kwa kuwa kisa kinawalenga watoto, ni lazima kiwe kisa cha watoto kweli na siyo kisa cha watu wazima kinachosimuliwa kwa watoto. Kwa hiyo, kisa kisimiliwe kwa kuzingatia ukweli kuwa uwezo wa watoto kuelewa mambo ni tofauti na watu wazima. Unaposimulia kisa kwa watoto mahali ambapo kuna watu wazima pia, jielekeze kwa watoto moja kwa moja. Ongea na watoto badala ya kuongea na watu wazima. Tumia lugha rahisi kueleweka kwa watoto. Kama utalazimika kutumia maneno magumu, hakikisha unayafafanua ili yaeleweke. Elezea kwa ufasaha wahusika wa kisa kama vile mwonekano wao, nguo zao, mambo wanayofanya. Simulia matukio katika visa kana kwamba unayaona matukio hayo yakitokea.
- Vuta usikivu wa watoto tangu mwanzo: Wakati wa kusimulia hakikisha unavuta usikivu wa watoto mwanzoni tu wa kisa chako na kuwafanya watamani kuendelea kukusikiliza.Uwe mbunifu kwa kutafuta namna nzuri ya kuanza kisa chako. Kwa mfano, unaweza kuanza kisa chako kwa swali au kwa kufanya kitu cha kushangaza na kuvutia au kuanza na sentensi inayovuta usikivu kama vile….Nilipokuwa mdogo kama ninyi….
Tumia uso wako kuonyesha picha ya kisa. Kama kisa ni cha huzuni, onesha uso wa huzuni na kama kisa ni cha furaha onesha furaha. Ili usionekane unalazimisha kuvaa uhusika, fanya mazoezi kabla. Unaweza kufanya mazoezi kwa kutumia kioo au kujirekodi kwa kutumia kamera ya video au simu.
Unaweza ukavaa kofia, kanzu, skafu, joho, mshipi au vitu vingine ili kuwafanya watoto wapate picha ya wahusika wa kisa unachosimulia. Kwa kadri utakavyoona inafaa unaweza ukatumia vifaa vingine katika kuongeza hisia ya uhalisia wa kisa. Kama unataka kuigiza mavazi ya mhusika katika Biblia, ni vizuri ukasoma vizuri biblia uone alikuwa anavaa mavazi gani katika sehemu ya kisa unachosimulia ili kuepusha kuchanganya mavazi na matukio.
Watoto wa rika zote, kwa kawaida, huvutiwa zaidi na vipindi au ufundishaji ambao nao watashirikishwa. Kwa kulijua hilo, mwalimu inabidi aone namna ya kuwashirikisha katika kusimulia kisa ambapo wanaweza kushiriki katika kuigiza vitendo vya wahusika wa visa. Kwa kufanya hivyo, wataelewa kwa urahisi zaidi na somo litakaa katika kumbukumbu zao kwa muda mrefu zaidi.
- Simulia kisa kwa mtiririko sahihi: Unaposimulia kisa, epuka kueleza vitu visivyo vya lazima. Nenda moja kwa moja kwenye vitu muhimu na uelezee matukio ya visa kwa kufuata mtiririko wake. Kanuni ni hii: Kwa kadri watoto wanavyokuwa wadogo zaidi ndivyo maelezo mengi yanavyokuwa hayahitajiki katika kisa. Watoto wadogo wanahitaji uende moja kwa moja kwenye kisa chenyewe bila kuwa na maelezo mengi yasiyo ya lazima. Hii ni kwa sababu watoto wadogo hawawezi kuchuja kipi cha muhimu na kipi si cha muhimu. Wewe ndiye unapaswa uchuje kwa ajili yao.
- Uwe makini na matumizi ya lugha ya picha: Biblia imejaa lugha zaa picha ambapo neno fulani linaweza kutumika kumaanisha kitu tofauti na maana ya kawaida ya neno hilo. Maneno hayo ni kama vile chumvi ya ulimwengu, nuru ya ulimwengu, kutoa moyo, kumfuata Yesu, mnyama na malaika akiruka angani. Watu wazima wanaweza kuelewa lugha hizi lakini kwa watoto inaweza kuwa vigumu. Kwa hiyo, kama unataka watoto wakuelewe, waambie moja kwa moja maneno hayo yanamaanisha nini badala ya kuwaacha wao wenyewe watafakari nini kinawakilishwa katika lugha hiyo ya picha. Kama unataka kuwafundisha namna ya kuonesha wema kwa rafiki zao, waambie moja kwa moja ni namna gani wanaweza kufanya hivyo. Kama unataka kuwafundisha kuwa mfano wa kuigwa, usiwaambie tu kwamba “uwe nuru ya dunia” badala yake waonyeshe namna gani wanavyoweza kuwa mfano wa kuigwa. Hii haimaanishi kuwa usitumie hata kidogo lugha ya picha. La hasha, unaweza kutumia pale inapobidi lakini hakikisha unaitafsiri vizuri lugha hiyo ili iwe wazi kwa kila watoto.
- Tumia lugha ya mwili kwa usahihi: Tafiti zinaonyesha kuwa 40% ya kile tunachojifunza kinatokana na mawasiliano yasiyo ya mdomo kutoka kwa yule anayefundisha. Mawasiliano yasiyo ya mdomo ni pamoja na lugha ya mwili, mavazi, mtindo wa nywele na kadhalika. Kwa hiyo, ni muhimu kutumia vizuri mawasiliano yasiyo ya mdomo. Kitu cha kwanza unachopaswa kufanya ni kuhakikisha kuwa unakutanisha macho na watoto na kwa kufanya hivyo kila mtoto atajisikia kuwa unazungumza naye. Lugha ya mwili lazima iwe halisia na iendane na kisa unachosimulia. Kwa mfano, kwa kutumia ishara za mikono unaweza ukaishiria mambo mengi kama vile tahadhari, hasira, kukataa, kugawanya, kupokea, kutoa kitu na kuonyesha (kusonda). Ishara zingine ni ishara za kichwa, mabega na uso. Zote hizi ni lazima uzifanyie mazoezi ili ziwe sehemu muhimu ya kisa unachosimulia.
- Msisitizo wa kisa uwe upande wa chanya zaidi: Pamoja na ukweli kwamba tunaweza kujifunza kutokana na matokeo mabaya ya kutokuwa watii lakini tunaweza pia kujifunza kutokana na matokeo mazuri ya kuwa watii. Unapotoa kisa, lengo lisiwe kuwatisha au kuwaogopesha watoto ili wawe na tabia nzuri ya utii. Kufanya hivyo hakuwapi watoto motisha ya kumfuata Yesu kwa sababu wanampenda bali kwa sababu ya kuogopa matokeo ya kutokumfuata. Msisitizo wa kisa chako uwe upande wa chanya zaidi na upande hasi uwe kidogo. Kumbuka “Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo”(1Yohana 4:18).
Kitu kingine cha kuepeuka ni matumizi ya kupita kiasi ya neno “usi…” Badala yake tumia lugha ya kuelekeza. Kwa mfano, badala ya kusema usizini, sema uwe mwaminifu, badala ya kusema “usiseme uongo” mwambie “sema ukweli” na badala ya kusema “usimchukie” mwenzako, sema “mpende” mwenzako.
- Washirikishe watoto kujadili kisa: Kisa kinaweza kuwa na mguso mkubwa kwa watoto ikiwa watashirikishwa kukijadili baada ya kuwa mwalimu amekisimulia. Wakipewa fursa ya kujadili kisa, wanaweza kukumbuka kwa urahisi mambo muhimu katika kisa hicho. Hata watoto wadogo kabisa wanaweza kuzungumzia kisa ili mradi tu wanajua kuongea na wamekisikiliza. Mwalimu au mhubiri anaweza kuwashirikisha watoto kwa kuwauliza maswali kuhusu kisa yanayowafanya wafikiri. Kwa hiyo, toa fursa kwa watoto kujadilia kisa kama mazingira na muda unaruhusu. Kwa maelezo zaidi juu ya namna mwalimu anavyoweza kuwafanya watoto waongee endelea kufuatilia makala katika mtandao huu, tutaendelea kushirikishana.
- Baada ya kisa sikiliza maoni ya kujenga. Baada ya kutoa kisa, ni vizuri ukajijengea utaratibu wa kupata maoni kutoka kwa watu wazima na watoto juu ya kisa chako na namna ulivyokitoa. Unaweza kupata maoni juu ya mambo mengi ikiwa pamoja na yafuatayo: urefu wa kisa? Ulitumia maneno rahisi au magumu kwa watoto? Kisa kilikuwa nje ya uelewa au uzoefu wa watoto? Kisa kilikuwa kizuri? Ni mambo gani unapaswa kuyabadilisha kama utapata nafasi ya kukisimulia tena? Kama kweli unataka kuboresha ufundishaji wako, uwe tayari kukubali kukosolewa na usijisikie vibaya unapokosolewa. Hata hivyo, si kila mtu anaweza kukupa ushauri wa kujenga. Vilevile, si kila mtu anaweza kukuambia kwa uwazi mapungufu aliyoyabaini maana wengine ni wanafiki. Kwa hiyo, uwe makini na watu unawaomba maoni. Chagua tu wale ambao una imani nao. Ndugu na marafiki wa karibu wanaweza kuwa msaada katika hili. Kwa wanandoa, mume au mke wako anaweza kuwa mtu sahihi wa kukupa maoni.
- Urefu wa kisa uendane na umri wa watoto: Moja ya mambo yanayowafanya watoto wasipate kitu kutoka kwenye kisa, ni kutozingatia muda. Kwa bahati mbaya sana watu wengi hawafahamu kuwa uwezo wa watoto kutulia na kusikiliza kitu mfululizo ni mfupi sana na unaendana na umri wa mtoto. Kwa kutolijua hilo, wengi wamejikuta wakisimulia kisa kwa muda mrefu na kujikuta watoto wote hawasikilizi. Wataalam wa elimu wanakadiria kuwa muda (dakika) wa mtoto kusikiliza kwa makini ni sawa na umri wake kujumlisha moja. Kwa mfano, mtoto wa umri wa miaka mitatu anaweza kutulia na kusikiliza kwa dakika zisizozidi nne tu na mtoto wa miaka minne anaweza kutulia na kusikiliza kwa muda usiozidi dakika tano tu. Kwa hiyo, ili upate usikivu kutoka kwa watoto, jitahidi kuzingatia mwongozo huu. Ukizisha ujue kuwa unapoteza muda wako bure maana hakuna mtoto anayekusikiliza. Jedwali lifuatalo linatoa mwongozo juu ya muda wa kufundisha na kuhubiri watoto, mada na mtindo wa ufundishaji.
Ungependa Kujifunza zaidi Juu ya Mada hii?
Rafiki yangu mpendwa, huenda bado una maswali mengi kuhusu namna unavyoweza kutumia visa kufundisha na kuhubiri watoto na ungependa kujifunza zaidi. Usiwe na wasiwasi, tuna kitabu mahususi kuhusu mada hii pamoja na mada zingine kuhusu kufundisha na kuhubiri watoto. Kitabu hicho kinaitwa Ustadi wa Kufundisha na Kuhubiri Watoto.
Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.