Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
“Mungu haangalii nje bali anaangalia ndani ya moyo” ni kauli maarufu sana inayotokana na dhana kwamba namna mtu anavyoonekana kwa watu wengine si muhimu ili mradi tu ndani ya moyo wake yuko safi.
Watu wanaotoa kauli hiyo huenda mbali zaidi hata kuithibitisha kwa kutumia maandiko matakatifu kama vile “…… Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo” (1 Samueli 16:7). Kwa bahati mbaya sana, fungu hili limekuwa likitafsiriwa nje ya muktadha wake ili watu waweze kuhalalisha mwonekano wao wa nje usiompendeza Mungu.
Ni kweli Mungu haangalii kama wanadamu wanavyoangalia, lakini hii haimanishi kwamba hajali mwonekano wetu wa nje. Mwonekano wa nje ni muhimu sana kwa Mungu kwa kuwa unadhihirisha utukufu na uwezo Wake wa uumbaji. Katika makala haya, nitakushirikisha visa vichache kutoka katika Biblia vinavyoonesha kuwa Mungu anajali sana mwonekano wetu wa nje na pia visa hivyo inaonesha uhusiano uliopo kati ya mwonekano wa nje na hali ya kiroho ya mtu.
Kujua namna gani Mungu anajali mwonekano wetu soma hapa
Katika kitabu cha Mwanzo sura ya 34 na 35 tunakutana na kisa ambacho kinaweza kutusaidia kuelewa uhusiano wa mwonekano wa nje na mambo ya kiroho. Mwanzo sura ya 34 inaonesha kuwa watoto wa Yakobo walikuwa wametenda dhambi kubwa na sasa baba yao Yakobo ilibidi afanye upatanisho kwa ajili yao na familia nzima.
Ili kufanya upatanisho huo, Mungu alimwelekeza Yakobo na familia yake kwenda Betheli kumfanyia madhabahu. Betheli ni mahali pale pale ambapo Mungu alimtokea Yakobo wakati akiwa safarini kumkimbia Esau (Mwanzo 28:10-19). Hivyo, Betheli palikuwa ni mahali patakatifu kwa Yakobo.
Ili upatanisho ufanikiwe, ilibidi maandalizi yafanyike. Katika maandalizi hayo, Yakobo aliwaambia watu wa nyumba yake na wote waliokuwa pamoja naye kuiondolea mbali miungu ya kigeni iliyokuwa katikati yao ambayo ilihusisha miungu migeni yote iliyokuwa mikononi mwao, na pete zilizokuwa masikioni mwao (Mwanzo 35:1-4). Miungu hii waliyoambiwa waiondolee mbali huenda ni ile ambayo Raheli aliichukua kwa baba yake (Mwanzo 31:19) pamoja na ile ambayo wana wa Yakobo walikuwa wameichukua mateka katika nyumba ya Shekemu (Mwanzo 34:27-29).
Kisa hiki kinatupatia fundisho kwa wakristo wa leo kwamba kuna uhusiano kati ya utakaso wa nje na utakaso wa ndani. Kama tunahitaji kupata utakaso wa ndani ya moyo dhidi ya dhambi zetu inabidi kuondoa vitu vya nje vinavyoweza kuwa vizuizi kwa utakaso wa ndani. Vitu hivyo ni pamoja na mapambo ambayo huvaliwa kwa ajili ya uzuri wetu badala ya utukufu wa Mungu. Ili kuhakikisha kuwa hatujaribiwi kuyatumia tena mapambo hayo, yafaa tuyaondolee mbali kabisa kama walivyofanya familia ya Yakobo.
Tukio linalofanana na la Betheli, linaelezwa katika kitabu cha Kutoka 33:1-6. Tukio hili linafuatia uasi mkubwa ulioelezwa katika Kutoka sura ya 32. Uasi huo ulitokea wakati Musa akiwa katika mlima wa Sinai kupokea Amri Kumi za Mungu.
Wakati wanasubiri ujio wa Musa kutoka mlimani, wana wa Israeli walileta kwa Haruni pete za dhahabu zilizokuwa nazo katika masikio na kumwomba awafanyizie miungu itakayoenda mbele yao kwa kuwa Musa alichelewa kurudi na hawakujua nini kilikuwa kimemtokea. Haruni akapokea pete hizo na akatumia patasi kutengeneza sanamu ya ndama kwa kuziyeyusha. Wana wa Israeli walianza kuiabudu na kuitolea dhabihu sanamu hiyo (Kutoka 32:2-4).
Baada ya Haruni kutengeneza ndama wa dhahabu, Mungu alimwambia Musa ashuke haraka kutoka mlimani ili kuona kilichotokea. Musa aliposhuka chini na kuona kilichotokea alikasirika sana na akazivunja zile mbao za mawe zenye amri kumi alizopewa na Mungu. Bwana alikasirishwa sana na kitendo hicho na “akawapiga hao watu, kwa walivyoifanya ile ndama ambayo Haruni aliifanya”. Tukio hilo lilimuhuzunisha Musa na kuwasihi watu kujiweka wakfu kwa Bwana ili awape baraka (Kutoka 32:29).
Katika sura ya 33, Bwana alinena na Musa na kumwambia aende katika nchi ya Kanaani na watu wake na kwamba Mungu asingeenda kati yao ili asiwaangamize njiani kwa maana ni watu wenye shingo ngumu. Habari za kwamba Mungu asingeenda kati ya wana wa Israeli katika safari yao zilikuwa ni habari mbaya kwao. “Watu waliposikia habari hizo mbaya wakaomboleza wala hapana mtu aliyevaa vyombo vyake vya uzuri” (Kutoka 33:4).
Ili asiwaangamize, Mungu alinena na Musa na kumwambia kuwa “basi sasa vueni vyombo vyenu vya uzuri ili nipate kujua nitakalowatenda” (Kutoka 33: 5). “Basi wana wa Israeli wakavua vyombo vyao vyote vya uzuri, tangu mlima wa Horebu na mbele” (Kutoka 33: 6). Kisa hiki kinaonesha dhahiri kuwa mapambo yalikuwa kizuizi kwa watu kujiweka wakfu kwa Mungu ili kujitoa kwao kuweze kukubaliwa na Mungu ilibidi wavue mapambo yote waliyokuwa nayo.
Kupitia visa hivi, mtazamo wa Mungu kuhusu uvaaji wa mapambo uko wazi. Mungu asiyebadilika, aliwaambia kuondolea mbali mapambo yao ili waende mbele zake kwa ajili ya utakaso.
Vilevile, maelekezo ya kuondoa mapambo yanahusiana na kuingia kwao katika nchi ya ahadi. Wana wa Israeli walitakiwa kuondoa mapambo yao yote ili wafae kuingia katika nchi ya ahadi. Je, hili lina uhusiano gani na maisha yetu ya leo?
Tunapaswa kujifunza kitu kutoka katika visa hivi kama Mtume Paulo anavyotushauri: “Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani” (1 Wakorintho 10:11). Tunapaswa kujifunza kutokana na yaliyowapata wenzetu. Mungu aliwataka waondoe mapambo yote ili waweze kuingia Kanaani, nchi ya ahadi. Sisi nasi tu wasafiri wa kwenda Kanaani ya mbinguni na hivyo nasi twapaswa kutupilia mbali mapambo yote yasiyomtukuza Mungu kabla ya kuingia katika Kanaani ya mbinguni.
Pengine, unaweza kujiuliza swali, mapambo yasiyomtukuza Mungu ni mapambo yapi na nitayajuaje? Kama unataka kujifunza zaidi kuhusu mapambo yanayomtukuza Mungu ni yapi na yapi yanamtukuza Mungu, unaweza kusoma Biblia na vitabu vingine vya kitaalam kuhusu mada hii.
Kwa kuwa biblia ina mada nyingi na kwa kuwa unaweza usipate vitabu kuhusu mada hiyo, kipo kitabu kizuri kinachochambua kwa kina mada hii kwa kitumia Biblia na vitabu vingine vya wataalam wa afya na wengineo.
Kitabu hicho kinaitwa “Mwonekano wa Mkristo: Kanuni Zinazokubalika Kibiblia, Kiafya na Kijamii Kuhusu Mavazi, Mapambo Na Vipodozi”. Kupata maelezo zaidi kuhusu kitabu hiki bonyeza hapa.
Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.
Je, Unataka Kupata Mafunzo Endelevu Kuhusu Mafanikio Kwa Mkristo?
Kama unataka kuendelea kujifunza kuhusu masuala mbalimbali juu ya mafanikio kwa mkristo unaweza kujiunga na mtandao huu wa Mkristo na Masiha ya Mafanikio ili uweze kupata makala mbalimbali kuhusu masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), maisha ya kikristo, malezi ya watoto na mengine mengi. Kwa kufanya hivyo, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa katika mtandao huu.
Ili kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini.
1 comment / Add your comment below