Je, Hata Mkristo anaweza Kuandika Wosia?

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo

Kwa watu wote ambao maisha yao yanaongozwa na Biblia, wanatambua kuwa kifo ni kitu halisi kama sehemu ya hali ya sasa ya mwanadamu iliyoathiriwa na dhambi (Mwanzo 2:17; Warumi 5; Waebrania 9:27). “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu, Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa (Mhubiri 3:1-2). Kulingana na uhalisia huu, wakati Wakristo wanamsubiri Yesu, inaweza ikatokea kuwa wakapatwa na umauti. Kwa sababu hiyo kuna haja ya kujiandaa kwa umauti.

Kujiandaa kwa mauti kunaweza kufanyika kwa njia mbili. Kwanza kujiandaa kiroho kwa kuweka sawa uhusiano wetu na Mungu ili tukifa basi tufe katika tumaini la kuokolewa Yesu anaporudi. Pili, kujiandaa kwa kuweka vizuri mambo yetu ili mali zetu ambazo Mungu ametupatia zigawiwe au zitumike sawasawa na sisi tunavyopenda. Hili la pili linaweza kufanyika kwa kuandika wosia.

Wosia ni kitu gani?

Wosia ni tamko au maandishi anayotoa mtu wakati wa uhai wake akielezea mazishi yake yatakavyofanyika akionyesha mahali atakapozikwa au jinsi mali zake zitakavyogawiwa kwa warithi wake baada ya kifo chake.

Ni vema ifahamike kuwa wosia ni suala la kisheria. Hivyo ukiamua kuandika wosia ni vizuri kupata ushauri wa kisheria ili wosia utakaouandika uzingatie matakwa ya sheria za nchi unayoishi ili na uweze kukubalika. Bilvile ni muhimu kupta ushauri kutoka kwa viongozi wako wa dini ili wosia wako uweze kukubalika kidini pia. Hivyo, wosia wako unapswa kukubalika kisheria na kidini pia.

Ipo dhana katika jamii kwamba kuandika wosia ni uchuro, yaani kujitakia kifo chako mapema. Dhana hii imesababisha watu wengi kutoandika wosia. Ukiacha dhana ya uchuro, watu wengine wana dhana kuwa wosia unaachwa na watu wasomi, wazee hasa wanaume, watu wanaokaribia kufa, watu wanaomiliki mali nyingi kama vile fedha, nyumba, viwanja na kadhalika. Hizi zote ni dhana potofu na tunapaswa kuondokana nazo. Ukweli ni kwamba kifo kipo tu hata kama hujaandika wosia.

Kwa kuwa mtoa wosia anaweza kuendelea kupata mali zaidi baada ya kaundika wosia, mali hizo zinaweza kuwa sehemu ya wosia bila hata kuorodheshwa katika wosia huo. Lakini pia wosia wa mwanzo unaweza kufutwa au kubadilishwa na wosia mwingine. Hii inaweza kutokea hata kama kuna kipengele katika wosia kinachosema wosia huo hautabadilishwa kamwe. Mabadiliko haya yanaweza kufanywa na aliyetoa wosia kipindi cha uhai wake na sio mtu mwingine yeyote.

Ikumbukwe kuwa mtoa wosia hatakuwa hai wakati wosia wake utakapotumika ili aweze kuulizwa na kutoa ufafanuzi kuhusiana na wosia wake. Hivyo, ni vema kuandika wosia kwa lugha ya wazi inayoeleweka vizuri. Utata wowote utakaojitokeza unaweza kupelekea wosia huo kuwa batili.

Faida za Kuandika Wosia

Wosia una faida nyingi. Baadhi ya faida hizo ni kama ifuatavyo:

  1. Wosia humsaidia mtoa wosia kupanga ni namna gani mali yake itakavyosimamiwa na kugawanywa baada ya kufariki kwake. Hii itamzuia mtu asiyehusika kuingilia mali zake baada ya kufariki na hivyo kuepusha mivutano na chuki miongoni mwa ndugu wa marehemu baada ya kifo cha mzazi au ndugu yao.
  2. Husaidia mali kutumika kwa makusudi mazuri sawa sawa na utashi wa mwenye mali.
  3. Wosia huepusha warithi wa mali za marehemu kutodhulumiwa au kudhulumiana mali hizo. Tumekuwa tukishuhudia warithi wa mali za marehemu hasa wanawake na watoto wakinyang’anywa mali hizo na ndugu pale baba wa familia anapofariki bila kuacha wosia na kuwaacha wakiishi maisha ya shida. Wosia huzuia watu wenye nia mbaya ya kutumia mali za ndugu wa marehemu au kuhujumu haki za familia iliyoachwa.
  4. Huokoa fedha na kuwaepusha warithi katika kesi hasa wakati wa harakati za kutaka haki zao pale ambapo hakuna wosia ulioandaliwa.
  5. Ikiwa mtoa wosia atatoa sehemu ya mali yake kwa kanisa, wosia husaidia kanisa kupata rasilimali na uwezo wa kutekeleza huduma zake ili kutimiza utume wake. Kama hakuna wosia, kanisa haliwezi kupata chochote hata kama mwenye mali alitamani kufanya hivyo.
  6. Kwa kuwa wosia hueleza utaratibu wa namna mtoa wosia atakavyozikwa, huepusha migogoro ya familia ya kugombania mahali pa kuzikwa marehemu.
  7. Hudhihirisha tendo la imani na ujasiri wa kiroho kwa yule anayeandika au kutoa wosia, kwa kutenda jambo linalompendeza Mungu na lenye baraka kwa kanisa la masalio na jamaa yake. 

Ungependa kujifunza zaidi kuhusu masuala ya fedha katika ndoa?

Rafiki yangu mpendwa, huenda bado una maswali mengi juhusu suala la kuandika wosia. Kama ndivyo, makushauri upate kitabu kizuri kinachoitwa Siri za Mafanikio ya kifedha Katika Ndoa na Familia: Kanuni za Kibiblia na Kiuchumi za Kukabiliana na Changamoto na Migogoro ya Kifedha Katika Ndoa na Familia.

Kupata maelezo zaidi kuhusu kitabu hiki bonyeza hapa

Kitabu hiki kimeeleza kwa kina suala la wosia na mirathi kwa muktadha wa kibiblia na kisheria. Zaidi ya wosia na mirathi , kitabu hiki kina mambo mengine mengi kuhusu masuala ya fedha katika ndoa na familia. Hiki si kitabu cha kukosa kwa mtu yeyote aliye serious na ustawi wa ndoa na familia yake.

Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

Je, unataka kupata mafunzo endelevu kuhusu mafanikio kwa mkristo?

Kama unataka kuendelea kujifunza kuhusu masuala mbalimbali juu ya mafanikio kwa mkristo unaweza kujiunga na mtandao huu ili uweze kupata makala mbalimbali kuhusu masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), maisha ya kikristo, malezi ya watoto na mengine mengi. Kwa kufanya hivyo, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa katika mtandao huu.

Ili kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *