Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Katika Biblia, matumizi ya vipodozi yanaonekana kwa mara ya kwanza katika 2 Wafalme 9:30 ambapo tunaelezwa namna Yezebeli alivyojipamba machoni na kichwani. “Hata Yehu alipofika Yezreeli, Yezebeli akapata habari; akatia uwanja machoni mwake, akapamba kichwa chake, akachungulia dirishani”.
Kisa hiki kilitokea wakati mfalme Yehu alipowasili Yezreeli baada ya kuwa amemuua Yoramu mfalme wa Israeli ambaye alikuwa mtoto wa Yezebeli na Ahazia mfalme wa Yuda aliyekuwa mjukuu wa Yezebeli.
Habari za matukio hayo zilimfikia Yezebeli na alijua wazi kuwa naye angeuawa. Ili kuepuka kifo kilichokuwa kinamkabili, ilibidi abuni mbinu itakayompumbaza Yehu asimuue. Mbinu hiyo ilikuwa ni kujipamba midomo na kichwa ili amvutie Yehu kimapenzi na kuachana na mpango wa kumuangamiza. Hata hivyo, Yehu hakushawishika na vipodozi vya Yezebeli bali aliendelea na mpango wake wa kumuua ambapo aliwaamuru matowashi wamshushe chini; na damu yake ikamwagika nyingine juu ya ukuta, na nyingine juu ya farasi, naye akamkanyaga-kanyaga na kufa. Mwonekano wa Yezebeli uliolenga kumshawishi Yehu asimuue, unaendana na maisha yake ambapo alifanya kila jitihada za kuwaingiza wana wa Israeli katika ibada ya miungu.
Katika Ezekieli 23, tunakutana na mfano unaoonesha matumizi mabaya ya vipodozi. Kisa hiki kinahusu wanawake wawili binti za mama mmoja. Binti mkubwa anaitwa Ohola na mdogo anaitwa Oholiba. Katika kisa hiki, Mungu anatumia lugha ya picha ambapo wanawake hawa wametumika kuwakilisha miji ya Samaria na Yerusalemu. Vilevile, mume wa wanawake hawa ametumika kumwakilisha Mungu. Ohola anawakilisha Samaria na Oholiba anawakilisha Yerusalemu. Samaria na Yerusalemu ilikuwa miji mikuu ya falme mbili za Israeli baada ya kugawanyika kwa taifa la Israeli kati ya ufalme wa Kaskazini na ufalme wa Kusini. Samaria ulikuwa mji mkuu wa ufalme wa Yuda ambao ulikuwa ni ufalme wa Kaskazini na Yerusalemu ulikuwa ni mji mkuu wa ufalme wa Yuda ambao ulikuwa ni ufalme wa kusini.
Ohola na Oholiba wanaelezwa kuwa ni makahaba ambao hawaridhiki na mume wao, yaani, Mungu na wanafanya uzinzi na wanaume wengine, yaani miungu wa uongo. “Tena mmewatuma watu kuwaita watokao mbali; ambao mjumbe alitumwa kwao, na tazama, wakaja; nawe ulijiosha kwa ajili yao, ulitia rangi macho yako, na kujipamba vyombo vya uzuri; ukaketi juu ya kitanda cha enzi, na meza imeandikwa tayari mbele yake, ambayo juu yake uliweka uvumba wangu na mafuta yangu. Na sauti za wingi wa watu wenye hali ya raha zilikuwa pamoja naye; na pamoja na watu wasio na adabu, waliletwa walevi toka jangwani; wakawatia vikuku mikononi, na taji nzuri juu ya vichwa vyao. Ndipo nikasema, Huyo aliye mkongwe atafanya uzinzi! Sasa hao watazini naye, naam, na yeye! Wakamwingilia kama watu wamwingiliavyo kahaba; ndivyo walivyowaingilia Ohola na Oholiba, wanawake wale waasherati. Basi watu wenye haki watawahukumu, kwa hukumu iwapasayo wazinzi, na kwa hukumu iwapasayo wanawake wamwagao damu; kwa sababu wao ndio wazinzi, na mikononi mwao mna damu” (Ezekieli 23:40-45).
Katika mfano huu, Ohola na Oholiba ni kielelezo cha namna wanawake wanavyotumia mapambo na vipodozi kuwavutia kingono wanaume. Kama ilivyo kwa Yezebeli, Ohola na Oholiba walijipodoa macho yao na kuvaa mapambo ili kuwavutia wanaume wafanye nao ngono. Katika kielelezo hiki, ni dhahiri kwamba lengo la kutumia vipodozi na mapambo ni kuwashawishi watu wa jinsia tofauti ili wafanye dhambi ya uzinzi. Mungu alikasirishwa na vitendo vya Ohola na Oholiba na kutamka hukumu yao.
Katika kielelezo kinachofanana na kile cha Ezekieli 23, katika kitabu cha Yeremia, tunakutana na mwanamke mwingine mwenye mavazi mekundu na mapambo ya dhahabu aliyejitia wanja machoni. Mwanamke huyu anawakilisha taifa la Israeli lililokataliwa. Kujipamba ilikuwa ni njia ya kuwavutia mataifa mengine yaweze kushirikiana na taifa hilo. “Na wewe, utakapotekwa, utafanyaje? Ujapojivika mavazi mekundu, ujapojipamba mapambo ya dhahabu, ujapojitia wanja machoni, unajifanya kuwa mzuri bure tu; wapenzi wako wanakudharau; wanakutafuta roho yako” (Yeremia 4:30).
Visa na mifano michache iliyoelezwa hapa ya wanawake waliotumia vipodozi inaonesha dhahiri kuwa matumizi ya vipodozi yalilenga kuwavutia wanaume ili kufanya nao ngono. Wanawake hawa hawakuridhika na waume zao. Kwa maneno mengine, wanawake hawa walitumia vipodozi ili kuwashawishi wanaume wafanye dhambi. Hawakuwa nia yoyote nzuri zaidi ya kuweka mazingira mazuri ya kushawishi kufanya ngono.
Pamoja na nia mbaya katika matumizi ya vipodozi kwa wanawake hawa, hii haimanishi kuwa Biblia inapinga matumizi ya vipodozi vya aina yoyote na kwa kiasi chochote. Matumizi ya vipodozi hayana tatizo kabisa ili mradi tu vipodozi hivyo viwe salama kwa afya. Tatizo ni sababu ya kutumia vipodozi hivyo. Kama vipodozi vitatumiwa kwa nia ya kuwavutia wanaume au wanawake ili kufanya ngono au hata kama si ngono bali kutaka kuonekana bora zaidi na kutafuta sifa, basi hapo ndipo ubaya wa matumizi ya vipodozi unapokuja. Vinginevyo, hakuna ubaya wa kutumia vipodozi.
Kujua uhusiano wa mwonekano wa nje na hali ya kiroho ya mtu, soma hapa
Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mada hii?
Rafiki yangu mpendwa, huenda bado una maswali mengi kuhusu mada hii. Kama ndivyo, nakushauri ununue kitabuchetu kinachoitwa Mwonekano wa Mkristo: Kanuni Zinazokubalika Kibiblia, Kiafya na Kijamii Kuhusu Mavazi, Mapambo na Vipodozi. Katika kitabu hiki utapata majibu yote ya maswali yako kuhusu vipodozi na mwonekano wa mkritoso kwa ujumla (mavazi na mapambo).
Ili kupata maelezo zaidi kuhusu kitabu hiki kitabu hiki,bonyeza hapa
Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mpango wa Mungu kuhusu mafanikio yako?
Basi jiunge na mtandao wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio. Mtandao huu umeanzishwa kwa kusudi la kuwapatia maarifa ya msingi katika nyanja mbalimbali za maisha. Katika mtandao huu utapata maarifa katika maeneo ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano, malezi ya watoto na mambo mengine ya kiroho kupitia email yako kila zinapowekwa kwenye mtandao huu.
Kujiunga na mtandao huu, jaza fomu hii hapa chini.