Hivi Ndivyo Unavyoweza Kukwepa Gharama za Miamala ya Fedha ya Kielektroniki bila Kuvunja Sheria

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Kutokana na maendeleo ya Sayansi na teknolojia yaliyopo, siku hizi utunzaji na uhamishaji wa fedha umekuwa rahisi sana. Unaweza kutunza fedha kwa namna nyingi kama vile kwenye akaunti ya benki na kwenye simu za mikononi kupitia akaunti ya M-pesa, Tigo-Pesa, Airtel Money, Halopesa, Esy-Pesa na T-Pesa. Siku hizi unaweza kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya benki kwenda kwenye akaunti nyingine ya benki hiyohiyo au benki nyingine. Vilevile unaweza kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya benki kwenda kwenye akaunti ya simu au kutoka kwenye akaunti ya simu kwenda kwenye akaunti ya benki.

Kwenye utoaji wa fedha, unaweza kutoa fedha kwenye akaunti ya benki au kwenye simu kupitia kwa wakala wa huduma za kifedha au kupitia kwenye mashine za kutolea fedha zinajiendesha zenyewe ziitwazo Automated Teller Machine (ATM). Uhamishaji na utoaji wa fedha wa aina hii ndiyo unaitwa miamala ya fedha ya kieletroniki.

Huduma hizi zimeturahisishia maisha na tunazifurahia lakini tunasahau kwamba zina gharama zake. Kwa kawaida, kuweka fedha kwenye akaunti ya benki au simu ni bure lakini kuhamisha au kutoa fedha taslimu kuna gharama zake. Kwa upande wa benki, hauhitaji kuhamisha au kutoa fedha taslimu ndipo ukate bali akaunti nyingi zina makato ya kila mwezi na kila mwaka hata kama hujatoa au kuhamisha fedha yoyote.

Tangu kuanza kwa miamala ya fedha ya kieletroniki kumekuwa na makato ambayo yalikuwa yanakatwa na benki zenyewe au kampuni za simu. Lakini tangu Julai 15 mwaka jana, Serikali ilianzisha tozo za miamala ya fedha za kielekroniki kupitia mitandao ya simu. Hali hii iliongeza gharama za miamala hiyo. Kwa mujibu wa Kanuni za tozo ya miamala ya fedha ya kielektroniki, za mwaka 2021 zilizoanza kutumika Julai 15, 2021, mteja alikuwa anakatwa kati ya shilingi 10 hadi 10,000 kulingana na kiasi cha fedha cha muamala husika.

Baada ya wananchi kulalamika sana juu ya tozo hizo, Serikali ilipunguza viwango vya tozo vya maiamala hiyo kwa asilimia 30 kuanzia terehe 1 Septemba, 2021. Katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, Serikali imepunguza zaidi viwango hizo. Hata hivyo, Serikali imeongeza wigo wa tozo  na sasa tozo hizo zinahusisha miamala yote ya fedha ya kielektroniki inayopitia mfumo wa malipo iliyopewa leseni zikwemo fedha za kieletroniki kupitia benki. Marekebisho hayo yaliyoanza kutumika mwezi Julai, 2022 yamefanywa na Serikali kupitia marekebisho kwenye Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa kwa kupunguza tozo ya miamala kutoka kiwango kisichozidi shilingi 7,000 hadi kiwango kisichozidi shilingi 4,000 katika kila muamala wa kutuma au kutoa pesa. Punguzo hili ni sawa na asilimia 43 ya kiwango cha sasa.

Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba aliyoyatoa wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya mwaka 2022/23 bungeni mjini Dodoma Juni, 2022, lengo la hatua hii ni kupunguza makali ya maisha kwa mtanzania hasa katika kipindi hiki cha changamoto kubwa ya kiuchumi na kuweka usawa katika utozaji wa tozo hiyo. Pamoja na maelezo hayo ya Waziri wa Fedha, wananchi wengi wamelalamikia tozo hizo kuwa zinaongeza ukali wa maisha hasa kwa wananchi wa kipato cha chini.

Rafiki yangu mpendwa, tozo hizi zipo kwa mujibu wa Sheria na tunapaswa kutii sheria bila shuruti kwa kulipa tozo hizo. Isivyo bahati ni kwamba, utozaji wa tozo hizi unafanyika kielektroni ambapo hakuna namna ya kukwepa maana zinakatwa moja kwa moja kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu. Hata hivyo, kuna namna ambayo unaweza kufanya ili kukwepa tozo hizo bila kuvunja sheria. Unaweza kupunguza gharama za miamala ya fedha ya kielektroniki kwa kutumia njia zifuatazo:

  • Kabla ya kwenda kuroa fedha panga kwanza bajeti ya matumizi ya fedha zako kwa muda fulani kama vile mwezi mmoja. Katika kufanya hivyo, usitoe fedha kidogo kidogo na mara kwa mara badala yake toa fedha mara moja na ujijengee nidhamu ya kukaa na fedha. Kwa mfano, baada ya kuwa umeandaa bajeti yako na kujua mahitaji yako kwa mwezi au kwa kipindi fulani utakachoamua wewe mwenyewe, unaweza kutoa fedha benki au kwenye akaunti ya simu zinazotosha mahitaji yako yote kwa kipindi hicho hata kama hauhitaji fedha zote siku hiyo. Tunza fedha hizo nyumbani na uwe unachukua kidogo kidogo kulingana na mahitaji ya siku kwa siku badala ya kwenda kuchukua kidogo kidogo kwenye akaunti ya benki au ya simu. Hapa utakatwa gharama mara moja tu badala ya kukatwa kila unapoenda kuchukua. Hivyo utapunguza makato hayo. Cha muhimu ni kuwa tu na nidhamu ya matumizi kwa kuzingatia bajeti uliyopanga.
  • Kila unapotaka kuchukua fedha benki au kwenye simu, chagua njia nafuu kuliko zote. Kwa mfano badala ya kuchukua fedha nyingi kwenye ATM ambapo utalazimika kuchukua kwa mikupuo mingi na kila mkupuo unakatwa fedha, unaweza kwenda kuchukua kwenye kaunta ya benki. Lakini pia unapaswa kuzingatia gharama za usafiri na muda unaopoteza kwenda benki. Fanya ulinganisho wa gharama na kisha uamue njia iliyo na gharama nafuu. Kwa kadiri inavyowezekana epuka matumizi ya ATM yasiyo ya lazima maana makato yake yanaweza kuwa makubwa ukilinganisha na kuchukulia fedha kwenye kaunta ya benki. Ndiyo maana ATM zimepewa jina la utani kama Automated Theft Machine (ATM) likimaanisha Mashine zinazojiendesha zenyewe zinazoiba fedha. Hivyo, epuka kuibiwa!
  • Kuna watu siku hizi wanalipa vitu vingi moja kwa moja kupitia simu au kupitia akaunti ya benki. Kwa mfano, mtu akitaka kununua umeme, kununua vocha, kulipa ada ya shule, kulipa deni kwa rafiki yake na kadhalika anafanya hivyo kwa kutumia akaunti ya simu au akaunti ya benki. Hii inasababisha apoteze fedha nyingi bila kujua. Pale inapowezekana, nakushauri ulipe fedha taslimu badala ya kulipa kwa simu au kulipa kutoka kwenye akaunti ya benki au kulipa kwa kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti moja ya benki au ya simu kwenda kwenye akaunti nyingine ya benki au ya simu. Kwa kufanya hivi utaepuka tozo kihalali.

Kwa kuzingatia haya utaweza kuepuka gharama zisizo za lazima. Unaweza kupuuza gharama hizi na kuziona ni ndogo lakini baada ya muda fualni ukikaa chini na kupiga hesabu unaweza kushangaa umepoteza pesa nyingi. Sasa kwa nini upoteze fedha hizo wakati unaweza kuiokoa kwa kuwa na nidhamu kidogo tu.

Je unataka kujau fedha zako huwa zinaenda wapi? Bonyeza hapa hapa

Je, ungependa kujifunza kwa undani juu ya nidhamu ya matumizi ya fedha?

Kama unapenda kujifunza zaidi juu ya nidhamu ya matumizi ya fedha, basi soma katika kitabu kiitwacho:SIRI ZA MAFANIKIO YA KIFEDHA KATIKA NDOA NA FAMILIA: Kanuni za Kibiblia na Kiuchumi na Kukabiliana na Migogoro na Changamoto za Kifedha Katika Ndoa na Familia.

Zaidi ya kujifunza nidhamu ya matumizi ya fedha, kitabu hiki kina mambo mengine mengi kuhusu elimu ya fedha, hasa elimu ambayo huwezi kuipata darasani. Ili kupata maelezo zaidi kuhusu kitabu kitabu bonyeza hapa.

Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mpango wa Mungu kuhusu mafanikio yako?

Basi jiunge na mtandao wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio. Mtandao huu umeanzishwa kwa kusudi la kuwapatia maarifa ya msingi katika nyanja mbalimbali za maisha. Katika mtandao huu utapata maarifa katika maeneo ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano, malezi ya watoto na mambo mengine ya kiroho kupitia email yako kila zinapowekwa kwenye mtandao huu.

Kujiunga na mtandao huu, jaza fomu hii hapa chini.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *