Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Zipo sababu nyingi zinazochangia kuharibika na hata kuvunjika kwa mahusiano katika ndoa. Sababu mojawapo ni sababu iliyowafanya wanandoa kuingia katika ndoa. Zipo sababu sahihi na zisizo sahihi za watu kuingia katika ndoa. Ukiingia katika ndoa kwa sababu sahihi, ndoa yako ina uwezekano mkubwa wa kuwa na amani, upendo na furaha. Lakini ukiingia kwa sababu isiyo sahihi, ndoa yako ina uwezekano mkubwa wa kutokuwa na amani, furaha na upendo.
Sababu zisizo sahihi za kuingia katika ndoa
Katika makala hii, naenda kukushirikisha baadhi ya sababu zisizo sahihi za kuingia kwenye mahusiano ya ndoa. Kama uko kwenye mchakato wa kuingia kwenye ndoa na kama sababu hizi ndizo zinakusukuma kuingia katika ndoa hauna budi kujitafakari na kufanya uamuzi upya. Sababu hizo ni kama ifuatavyo:
1. Kuingia katika ndoa kwa sababu ya fedha
Baadhi ya watu huangalia uwezo wa mtu kifedha kama kigezo muhimu cha kuingia naye katika mahusiano. Kinachowapeleka watu katika mahusiano hayo ni maisha mazuri na si kitu kingine. Hapa wengine wamewageuza wapenzi wao kuwa chanzo cha mapato ya kuwainua kimaisha pamoja na ndugu zao.
Katika penzi la namna hii, kinachowaunganisha ni pesa tu na si mguso wa upendo baina yao. Ikitokea hicho kilichowaunganisha, yaani pesa, hakipo tena hata ndoa nayo itafikia mwisho. Wanandoa walioingia katika mahusiano kwa kusukumwa na pesa wana uwezekano wa kutokuwa waaminifu katika ndoa kwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa zao ili kutafuta upendo ambao hauko katika ndoa yao. Vilevile, kwa kuwa hakuna gundi ya upendo baina yao, ndoa za aina hii huwa hazina amani na furaha ya kweli.
2. Hofu ya umri mkubwa
Wapo baadhi ya watu, hasa wanawake, ambao kwa sababu moja ama nyingine, walichelewa kuolewa hadi wakafikia umri ambao wanawake wengi wa rika lao wanakuwa wameshaolewa. Kwa sababu ya kudhani kuwa watakosa wenzi wa ndoa kwa sababu ya umri, wengi huwa wanaolewa na mtu yeyote bila kujali kama wanampenda au wanaendana naye kitabia. Ndoa nyingi za aina hii zimeishia kwenye migogoro na hatimaye talaka au kutengana.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wanawake wenye kiu ya kupata watoto, na wameogopeshwa na habari kwamba wana weza wasipate watoto kwa sababu ya umri wao, wamekuwa wakijirahisisha kwa mwanaume yeyote ilimradi tu waolewe au wazae naye. Wanawake hawa wameishia kujuta baada ya kugundua kuwa mtu waliyezaa naye hakuwa baba bali mwanaume tu au mtu waliyeoana naye hakuwa mume bali mwanaume tu. Matokeo yake, wanawake hawa wameishia kulea watoto peke yao au kuishi ndani ya ndoa wakiwa sawa na wanawake wasio na ndoa. Changamoto hii inawaathiri si wanawake hao tu bali hata watoto wao. Kwa wale wanaokimbilia kuolewa ili wakazae watoto, niwakumbushe kuwa si kila anayeolewa hupata watoto maana wapo wanawake wengi na wanaume wengi walio kwenye ndoa lakin, kwa sababu zilizo njie ya uwezo wao, hawana watoto. Hivi fikiria, umeingia kwenye ndoa ili upate mtoto halafu kwa sababu zilizo nje ya uwezo wako ukakosa mtoto. Je, utavunja ndoa?
3. Kuoana kwa sababu mmepeana mimba
Kuoana na mtu eti tu kwa sababu mlikuwa naye katika mahusiano ya kimapenzi na mkapata mtoto ni sababu nyingine isiyo sahihi ya kuingia kwenye ndoa. Mara nyingi, watu hujikuta wanapeana mimba tu bila hata kupanga kupata mimba achilia mbali kupanga kuoana. Kama hamkuwa na wazo la kuoana kabla ya kupeana mimba, hampaswi kupanga kuoana kwa sababu tu ya mimba. Kwa watu ambao tayari wako katika mahusiano ya kimapenzi kama hawa, wanaweza kuoana tu ikiwa wanapendana kwa dhati na wamefahamiana vya kutosha kiasi cha kujiridhisha kuwa wanaendana kihaiba na katika mambo mengine.
Kama hamkuwa mmepanga kuoana kabla ya kupeana mimba ni udhihirisho kuwa hamkutakiwa kuwa pamoja bali mmelazimishwa tu na mimba. Kinachofuatia hapo ni kufungulia mlango ili kupata mapenzi ya kweli nje ya ndoa au kufanya mkakati wa kusitisha mahusiano yenu ili kuitafuta furaha ya kweli sehemu nyingine. Si vema vijana kuanza mapenzi kabla ya ndoa bali yawapasa kuwa waminifu ili msipate mimba kabla ya ndoa na kulazimika kuoana kwa sababu tu ya mimba.
4. Kuingia kwenye ndoa kwa sababu ya upweke
Mara nyingi mtu anapokuwa peke yake (single) huwaza kuwa ndoa ndiyo inayoweza kuwa suluhisho la upweke wake. Ni kweli kabisa, siyo kitu chema mtu kukaa peke yake bila mwenzi wa ndoa maana hata Biblia inasema “Sio vema mtu awe peke yake…” (Mwanzo 2 :18). Lakini ni vema ukatofautisha kuwa peke yako na kuwa mpweke. Kuwa pekee yako inamaanisha kukosa mtu wa kuwa naye pamoja au kukosa ukaribu na watu wengine. Kwa upande mwingine, upweke (loneliness) inahusisha nafsi, akili na hisia. Kuwa na upweke ni hali ya kujihisi kutengwa, hali ambayo ni vigumu kuishughulikia. Hivyo unaweza ukawa hauko kwenye ndoa lakini usiwe mpweke au ukawa kwenye ndoa lakini ukawa mpweke. Ni afadhali kukaa pekee yako bila upweke kuliko kuwa kwenye mahusiano ya ndoa lakini ukawa upweke.
Kuna watu waliingia kwenye mahusiano ya ndoa wakidhani kuwa watapata suluhisho la upweke lakini walipoingia kwenye ndoa mawasiliano baina yao na wenzi wao yakawa si mazuri na matokeo yake wakakomaza upekee waliokuwa nao na ukageuka kuwa upweke. Yaani, wakawa wawili lakini wapweke. Hivyo, mtu yeyote anayedhani ataondoa upweke kwa kuwa katika ndoa, anapaswa kutafakari upya.
5. Shinikizo la wazazi, ndugu, jamaa na marafiki
Wakati mwingine, watu hujikuta wanaoana kwa shinikizo la kihisia au kihalisia kutoka kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki. Mashinikizo ya kihisia hutokea pale ambapo watu wanakushawishi mara kwa mara kuoa au kuolewa kwa sababu mbalimbali kama vile umri, hitaji la kupata watoto, kupata heshima katika jamii na kadhalika. Unaweza ukawa hujihisi kama unalazimishwa lakini kule tu kukumbushwa mara kwa mara, kunaathiri hisia zako na kuweza kukufanya uingie katika ndoa ambayo hukuipanga.
Shinikizo la kihalisia ni pale wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wanapokulazimisha kuoa au kuoana na mtu fulani kwa sababu tu ni rafiki yao au kwa sababu ya kulinda maslahi na matarajio yoyote binafsi. Kabla ya kuingia kwenye ndoa ya aina hii yakupasa uelewe kuwa ndoa hiyo ni kati yako wewe na si ya wazazi, ndugu, jamaa au rafiki anayekushinikiza. Kama itakuwa ni ndoa yenye amani , wewe ndiye utapata hiyo amani lakini kama itakuwa ndoa isiyo na amani, wewe ndiye utaishi maisha yasiyo na amani. Hivyo, usikubali kuingia katika ndoa na mtu asiye wa chaguo lako.
6. Kupata uhuru
Baadhi ya watu huamua kuingia katika ndoa ili kupata uhuru binafsi. Kwa mfano, ikiwa mtu anaishi na wazazi na wazazi hao wanambana kiasi kwamba hawezi kufanya baadhi ya mambo kwa uhuru, basi mtu anaweza kuamua kuoa au kuolewa ili aondoke nyumbani na kuwa huru kufanya mambo ambayo alikuwa hawezi kuyafanya akiwa nyumbani.
Hizi ni baadhi tu ya sababu zisizo sahihi za kuingia kwenye mahusiano ya ndoa. Kama unapanga kuingia kwenye mahusiano ya ndoa kwa sababu hizi, basi tafakari upya uamuzi wako ili usije kujuta baadaye.
Je, unapenda kupata masomo endelevu kuhusu mahusiano?
Kama unapenda kupata masomo endelevu kuhusu mahusiano na masuala mengine ya mafanikio kwa muktadha wa kikristo, unaweza kujiunga na mtandao wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio. Kwa kufanya hivyo, utaweza kupata makala kupitia email yako kila zinapowekwa kwenye mtandao huu. Katika mtandao huu utapata maarifa mazuri katika maeneo ya mahusiano (uchumba na ndoa) na maeneo mengine ya maisha kama vile fedha, biashara, uwekezaji, malezi ya watoto na mambo mengine mengi.
Kujiunga na mtandao huu jaza fomu hii hapa chini.