Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Wakati Mungu anaanzisha taasisi ya ndoa, alimtafutia Adamu mke wa kufanana naye kama Neno lake linavyosema “Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye” (Mwanzo 2:18). Kwa sababu hiyo, nasi hatupaswi kufanya tofauti bali kutafuta mtu wa kufanana nasi.
Kufanana kwa wanandoa kutawafanya waelewane kwa urahisi na kutofautiana kwao kutawafanya wasiwe rahisi kuelewana. Hivyo, tunapotafuta mwenzi wa maisha ni muhimu kutafuta ambaye tuna mambo mengi tunayofanana. Wakati wote tunapomfikria mtu kama anaweza kufaa kuwa mwenzi wa ndoa yapasa tujiulize swali hili: Ninafanana naye katika mambo ya msingi? Yapo mambo mengi tunayopaswa kufafana na wenzi wetu wa ndoa. Moja ya mambo hayo ni imani ya dini.
Neno la Mungu linaelekeza: “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? (2 Wakorintho. 6:14-15).
Mafungu haya yanatoa mwongozo juu ya mahusiano baina ya watu wa imani mbalimbali hususani mtu aaminiye na asiyeamini. Pamoja na kwamba tunapaswa kuwaheshimu na kuwapenda watu wa dini tofauti, yawapasa waaminio kuwa makini wanapohusiana na watu wasioamini hasa katika mambo nyeti yanayogusa mustakabali wa uzima wa umilele. Mojawapo ya mambo hayo ni mahusiano ya ndoa. Ni vema kuoana na mtu anayeamanini na kuepuka kuoana na mtu asiyeamini.
Pengine kabla hatujaendelea, ni vema tuelewe, maneno “asiyeamini” na “aaminiye” yanamaanisha nini. Awali ya yote, yatupasa tuelewe kuwa maneno haya, kama yalivyonukuliwa hapo juu, yanapatikana katika waraka wa Mtume Paulo aliowaandikia wakristo wa kanisa la Korintho. Huu ni waraka ulioandikwa kwa watu wanaomwamini Kristo. Kwa muktadha huu, Paulo anaposema “wasioamini”, anamaanisha wasiomwamini Yesu Kristo. Kwa maneno mengine, waaminio ni wakristo na wasioamini ni watu ambao si wakristo.
Katika Agano jipya, neno lililotafsiriwa kama “asiyeamini”, linatokana na neno la kiyunani apistou. Neno hili likitumika kama kivumishi na likitafsiriwa sisisi (literally) linamaanisha mtu asiyemwaminifu na hutumika kwa mtu asiyeshika vizuri imani ya kikristo au mwenye mapungufu katika imani ya kikristo. Hivyo, neno “asiyeamini” lilitumika kumwelezea mtu yeyote mwenye mwenendo unaopingana na imani ya kikristo na utauwa na kwa hivyo mkristo anayeamini au mwaminifu alitegemewa kuwa na mwenendo tofauti na asiyeamini. Kwa kuzingatia tofauti zao hizi, Paulo anawashauri “wanaoamini” kutoingia katika uhusiano na “wasioamini” ili kuepusha migongano baina yao.
Katika maana pana zaidi ya mafungu haya, mtu “asiyeaamini” si lazima awe mtu asiye na dini bali mtu yeyote asiyeamini kama wewe unavyoamini. Hata kama ni mkristo, lakini ni wa madhehebu tofauti, kwako huyo ni mtu asiyeamini kwa sababu kuna mambo mengi ambayo haamini kama wewe unavyoaamini. Ni muhimu sana kuoana watu wa madhehebu moja na siyo dini moja maana kuna tofauti kubwa sana ya mitazamo ya mambo na hata mtindo wa maisha baina ya madhehebu ndani ya dini moja.
Tofauti za mitazamo ya mambo na mitindo ya maisha baina ya watu wa madhehebu tofauti zinapunguza kufanana kwa waumini wa madhehebu hayo. Hivyo, kama wewe ni mkristo mkatoliki vi vema uoane na Mkatoliki mwenzako na kama wewe ni Mkristo Mlutheri ni vema uoane na mlutheri mwenzako na kadhalika. Hata hivyo, hii haimanishi kuwa tusishirikiane kabisa na watu wasio wa imani yetu. La hasha. Mafungu haya hayapaswi kuchukuliwa hivyo maana kama yangekuwa yanamaanisha hivyo, ingebidi kila dini au kila madhehebu wawe na dunia yao. Tunaweza kushirikiana na watu wa imani zote katika masuala ambayo hayaathiri mustakabali wa wokovu wetu. Kwa maneno mengine, tunaweza kushirikiana na mtu wa dini au imani yoyote katika namna ambayo haitathiri imani yetu na wokovu wetu.
Tukumbuke kwamba ndoa ni uhusiano wa karibu mno, ulio nyeti na mtakatifu zaidi kuliko uhusiano wa aina yoyote duniani. Ni uhusiano uliokusudiwa na Mungu kuwa baraka kwa wanadamu na wa kudumu hadi kifo kinapowatenganisha. Kuoana na mtu wa imani moja na wewe kutaleta umoja katika ndoa yenu na kutachangia kuwa na ndoa yenye furaha na mafanikio. Kutofautiana kwa wanandoa katika imani ya dini kunaweza kuchangia kupunguza furaha ya familia na kuleta machafuko, majonzi, wasiwasi na kushindwa kulea watoto katika njia mnayotaka maana kila mmoja atataka awalee kwa misingi ya imani ya dini yake.
Neno la Mungu linasema “‘Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana?’ (Amosi. 3:3). Furaha na mafanikio ya uhusiano wa ndoa vinategemea umoja wa wahusika; lakini kati ya anayeamin na asiyeamini kuna tofauti kubwa ya mambo wayapendayo, matakwa na makusudi. Wanatumikia mabwana wawili, ambao hawawezi kupatana. Hata misimamo ya mtu ikiwa safi na sahihi kiasi gani, mvuto wa mwenzi asiyeamini kama anavyoaamini yeye utakuwa na mwelekeo wa kumpeleka mbali na kile anachokiamni. Ndoa zina nafasi zaidi ya kudumu, na maisha ya ndoa kutimiza kusudi la Mungu kama mume na mke wana umoja na wameunganishwa na maadili ya kiroho na mtindo wa maisha unaofanana. Mambo ambayo yanaweza kuleta changamoto kama mtaoana na mtu wa imani tofauti ya dini ni pamoja na ibada kwa Mungu, kushika taratibu za imani, burudani, kujumuika, matumizi ya pesa, matumizi ya vyakula na vinywaji vya aina fulani na malezi watoto. Kutofautiana kwa wanandoa katika maeneo haya mara nyingi kunaweza kuleta uzorotaji wa uhusiano baina yao, kuvunjika moyo, na hata kupoteza kabisa hali ya ukristo wao.
Ungependa kujifunza zaidi kuhusu mada hii ?
Hapa nimekueleza kwa kifupi tu juu umuhimu wa kuoana na mtu wa imani yako.Makala haya yataendelea ambapo nitafafanua zaidi juu ya suala hili kwa kutumia mifano halisi. Nikusihi tu uendelee kufuatilia mtandao huu ili tuweze kujifunza zaidi juu ya mada hii.
Zaidi ya masuala ya mahusiano, mtandao huu umesheheni makala nzuri kuhusu masuala mengine kama fedha, biashara, uwekezaji, malezi ya watoto, mwenendo wa mkristo, ustadi wa kuandaa na kuwasilisha mahubiri kwa watu wazima na kwa watoto na masuala mengine mengi.
Ili usipitwe na chochote kwenye mtandao huu, unaweza kujisajili ili uweze kupata makala moja kwa moja kwenye email yako kila zinapowekwa mtandaoni.
Ili uweze kujisajili, jaza fomu iliyoko hapa chini.
Nimependa n animefurahi kujifunza