Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Mojawapo ya mambo muhimu sana ya kuzingatia unapochagua mwenzi wa maisha (mume au ke) ni imani ya dini. Jambo hili limekuwa likipuuzwa sana na watu wengi na ni kawaida kukuta mkristo ameoana na mwislamu au mkristo ameoana na mtu asiye na dini au mkristo wa madhehebu fulani kuoana na mkristo wa madhehebu mengine.
Katika Biblia, Mungu anaonya vikali dhidi ya kuoana na watu wa imani tofauti. Kwa mfano, katika Kumbukumbu la Torati, Mungu anatoa maelekezo ya kutooana na makabila yaliyokuwa yakiishi katika nchi ya Kanaani ambao walikuwa waabudu sanamu (imani tofauti na wana wa Israeli). ‘ Bwana, Mungu wako, atakapokutia katika nchi uendayo kuimiliki, atakapoyang’oa mataifa mengi watoke mbele yako, Mhiti, na Mgirgashi, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, mataifa saba makubwa yenye nguvu kukupita wewe; wakati Bwana, Mungu wako, atakapowatoa mbele yako, nawe utawapiga; wakati huo ndipo uwaondoe kabisa; usifanye agano nao, wala kuwahurumia; wala usioane nao; binti yako usimpe mwanawe mume, wala usimtwalie mwanao mume binti yake. Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira ya Bwana juu yenu, naye atakuangamiza upesi ’ (Kumbukumbu la Torati 7 :3)
Kwa kutoa maelekezo haya, Mungu alijua kuwa kuna changamoto pale watu wa imani tofauti wanapooana. Hivyo, hatupaswi kupuuza maelekezo hayo. Wale wanaopuuza wamekuwa wakikutana na changamoto nyingi. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja matumizi ya fedha, ibada kwa Mungu, ushikaji wa taratibu za imani, masuala ya burudani na malezi ya watoto. Katika makala haya, nitakupatia mifano michache tu ya changamoto hizi.
Kujua Biblia inamaanisha nini inaposema usifungiwe nira na asiyeamini soma hapa
Matumizi ya fedha : Imani ya dini inaathiri namna unavyotumia fedha zako. Kwa mfano, kwa mujibu wa mafundisho ya baadhi ya madhehebu ya kikristo, muumini anapaswa kutoa zaka na sadaka kwa Mungu kila anapopata kipato. Kwa mafundisho hayo, zaka ni asilimia kumi ya kipato chako kabla ya makato yoyote na sadaka ni angalau asilimia kumi ya kipato chako (jumla ya zaka na sadaka ni asilimia 20 ya kipato chako au zaidi). Kwa upande mwingine, yapo madhehebu ya kikristo yanayofundisha tofauti kuhusu utoaji wa zaka na sadaka. Kwa mfano, katika baadhi ya madhehebu, zaka hutolewa mara moja tu kwa mwaka na si kwa kila kipato unachopata na unatoa kiasi unachopangiwa na kanisa na huwa chini ya asilimia 10. Kwa upande wa sadaka, baadhi ya madhehebu ya kikristo hufundisha kuwa unaweza kutoa kiasi chochote utakachojisikia.
Sasa, hebu fikiria, mkristo wa madhehebu yanayofundisha kuwa zaka na sadaka ni asilimia 20 au zaidi anaoana na mkristo wa madhehebu yanayofundisha kuwa zaka hutolewa mara moja tu kwa mwaka na sadaka ni kiasi chochote unachoamua. Hatuhitaji kuwa manabii kutabiri kuwa ndoa ya aina hii itakuwa na mgogoro mkubwa kuhusiana na matumizi ya fedha ikiwa kila mmoja atataka atoe zaka na sadaka kulingana na imani yake.
Matumizi ya vyakula na vinywaji: Yapo madhehebu ya kikristo yanayofundisha kuwa baadhi ya vyakula na vinywaji havifai kuliwa. Wakati huo huo, mafundisho ya baadhi ya madhehebu huruhusu matumizi ya vyakula na vinywaji vinavyokataliwa na madhehebu mengine. Hivi itakuwaje ikiwa watu wa madhehebu haya mawili wakioana?
Siku ya ibada na mapumziko: Lipo pia suala la siku ya mapumziko na ibada. Wapo wakristo wanaopumzika na kufanya ibada siku za Jumamosi na hawafanyi kazi yoyote siku hiyo. Lakini wapo wakristo wengine wanaopumzika na kufanya ibada siku za Jumapili. Hawa wa Jumapili, wanaweza kwenda kanisani siku hiyo na baadaye wakaenda kazini au wakaenda kazini na baadaye wakaenda kanisani lakini wanaopumzika Jumamosi, hawawezi kufanya kazi yoyote siku hiyo kabla au baada ya ibada. Fikiria watu wa madhehebu haya mawili wakioana hali itakuwaje katika familia hiyo? Lazima kutakuwa na mgogoro.
Burudani: Kwa kuwa na imani fulani ya dini hata aina ya burudani itaongozwa na imani yako. Kama wewe ni mkristo, bila shaka mojawapo ya burudani zako inaweza kuwa nyimbo za kwaya. Kwa mtu ambaye si mkristo anaweza asipende kusikiliza nyimbo za kwaya. Pia kwa baadhi ya wakristo, imani yako inawafanya wasishiriki katika baadhi ya burudani kama vile kwenda disko na katika klabu za usiku lakini kwa imani zingine zinaruhusu. Kwa kuwa na burudani tofauti kwa wanandoa, inaweza kuwapunguzia ukaribu baina yenu na hivyo mnaweza msifurahie maisha kwa pamoja kama wanandoa.
Hii ni mifano michache tu kati ya mingi inayoonesha changamoto zinazoweza kutokea ikiwa watu wa imani tofauti za dini wataoana. Pengine, nisisitize pia kuwa haitoshi tu kuchagua mtu wa imani ya dini sawa na ya kwako kuwa mume au mke wako bali chagua mtu anayeshika vizuri imani hiyo kwa kuwa si wote walio katika imani yako ya dini wanashika vizuri imani. Wengine wapo tu kwenye imani kwa sababu mbalimbali kama vile kufuata dini ya wazazi, ndugu, jamaa na marafiki na wengine wanakuja kwa sababu tu ya maslahi fulani. Kama ukioana na mtu asiye imara katika imani kuna hatari na wewe ukashuka kiimani pamoja na familia yako wakiwemo watoto wako.
Ipo mifano mingi ndani na nje ya Biblia ya athari hasi za kuoana watu wa imani tofauti za dini. Ndoa ya Ahabu na Yezebeli ni mmoja wa mifano hiyo. Kwa kumuoa Yezebeli aliyekuwa mwanamke mrembo na mtoto wa mfalme, Ahabu alidhani ameoa mke bora lakini cha ajabu mwanamke huyu alikuja kuchafua kabisa nyumba ya Ahabu, watoto na wajukuu wake na taifa kwa ujumla kwa kuleta miungu ya kigeni ya wafilisti. Unaweza kusoma kisa hiki kuanzia 1 Wafalme 16 :28 hadi 2 Wafalme 21:3.
Ukiacha kisa cha Ahabu na Yezebeli, ipo mifano mingi katika maisha ambapo watu waliokuwa wameshika imani vizuri waliweza kuasi imani hiyo baada tu ya kuoana na mtu wa imani tofauti au mtu wa imani yake lakini ambaye hajasimama imara katika imani. Kama yanawatokea wengine, wewe ni nani hata yasikutokee ? Usalama dhidi ya hili uko kwenye kuoana na mtu wa imani yako na aliyesimama imara katika imani ili muweze kuimarishana.
Japo ni vigumu kujua hali ya kiroho ya mtu maana ni Mungu pekee anayeweza kuona kwa usahihi, hali ya kiroho ya mtu, ni muhimu sana kuangalia hali ya kiroho ya mtu unayepanga kuoana naye. Kuna viashiria vya nje unavyoweza kuvitumia kujua hali ya kiroho ya mtu.
Majibu ya maswali yafuatayo yanaweza kukusaidia kujua hali ya kiroho ya mwenzi wako mtarajiwa:
- Ana kawaida ya kusoma Biblia kila siku au mara kwa mara?
- Ana kawaida ya kufanya maombi binafsi mara kwa mara?
- Ana kawaida ya kuhudhuria ibada kanisani?
- Maisha yake yanaendana na mafundisho ya Neno la Mungu?
- Anashiriki kikamilifu kwenye shughuli za kanisa?
- Uelewa wake wa mafundisho ya kanisa ukoje?
- Unadhani anaweza kufundisha mafundisho ya imani kwa watoto wenu?
Jambo jingine la hatari ni kubadili imani ya dini yako ili kumfuata mchumba wako au mchumba wako kubadili dini ili afuate dini yako ili muweze kuoana. Kama mchumba wako atabadili dini kwa sababu amevutiwa na mafundisho ya dini yako, hilo ni jambo jema sana. Lakini ni kitu cha hatari sana kama atabadili dini kwa sababu tu anataka kuolewa au kuoa. Hapa atakuwa anakufuata wewe tu na siyo imani na siku akikupata (mkioana) anaweza kurudi kwenye imani yake. Na hata asiporudi kwenye imani yake anaweza asiyashike vizuri mafundisho ya imani yako kwa sababu hakuwa na sababu sahihi ya kushika imani hiyo. Hali hii inaweza kuwaletea changamoto katika maisha yenu.
Kwa kuzingatia changamoto hizi na nyingine ambazo sijazitaja, ni vema kuoana na mtu wa imani yako kama unataka kuwa na ndoa yenye amani, furaha na maelewano. Ikiwa kweli umedhamiria kuutafuta ufalme wa Mungu, kamwe usithubutu kuanza harakati zozote za uchumba na mtu yeyote ambaye si imani yako au wa imani yako lakini hali yake ya kiroho inatia shaka. Usalama ni kuoana na mtu ambaye tayari amesimama imara katika misingi ya imani ya dini yako. Mkiwa na imani moja ya dini mtaweza kutiana moyo na kusaidiana katika masuala ya kiroho. Kwa mfano mtaweza kuomba pamoja, kwenda pamoja katika sehemu ya ibada, kushiriki pamoja katika shughuli zinazohusiana na imani yenu kama vile kufanya uinjilisti, kuhudhuria matukio maalum ya kanisani na kadhalika. Kwa kufanya hivyo mtaweza kuimarisha umoja na ukaribu baina yet]nu hali inayoweza kuimarisha ndoa yenu
Je, ungependa kujifunza zaidi kuhusu mada hii?
Mada hii itaendelea. Kama unataka kuendelea kujifunza zaidi kuhusu masuala ya mahusiano na mada zingine za kiroho, unaweza kujiunga na mtandao huu wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio ili uweze kupata makala mbalimbali zitakazokusaidia kuboresha maisha yako ya kiroho.
Zaidi ya kujifunza kuhusu mahusiano, utapata pia makala juu ya masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, maisha ya kikristo, malezi ya watoto na mengine mengi. Kwa kujiunga na mtandao huu, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa.
Ili kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini.