Unahitaji Kujua Kweli Hizi Kabla ya Kuchukua Mkopo Wowote

Rafiki yangu Mpendwa,

Suala la madeni yatokanayo na mikopo linawatesa wengi. Sababu mojawapo ya hali hii ni kwamba kuna kweli nyingi ambazo watu hawazijui kuhusu mikopo na pia kuna upotoshaji mwingi sana kuhusu mikopo.

Kwa mfano:

  • Je, unajua vigezo vya kuzingatia kabla ya kuchukua mkopo?
  • Je, unajua wakopeshaji huwa wanammanisha nini wanapokuambia kuwa “unakopesheka”?
  • Je, unajua kuwa ni hatari kuchukua mkopo kwa ajili ya biashara mpya?
  • Je, unajua kuwa dhana kwamba huwezi kuendelea bila mkopo haina ukweli?

Fuatana nami nami  katika makala haya ninapoangazia hoja hizi:

Kigezo cha kuzingatia unapochukua mkopo ni kimoja tu

Ikitokea unahitaji kukopa, kigezo muhimu cha kuzingatia katika kuamua kama uchukue  mkopo huo au la ni kimoja tu. Kigezo hicho ni hiki: Usilipe mkopo kwa pesa zako, bali lipa kwa pesa za watu wengine. Kigezo hiki kinamaanisha kwamba uchukue mikopo mizuri, mikopo ambayo inazalisha na siyo mikopo inayokugharimu wewe.

Kwa kutumia kigezo hiki, Mkopo pekee unaoweza kuchukua ni mkopo wa uzalishaji kama vile mkopo kwa ajili ya biashara ambayo tayari imeshasimama na hivyo unaupeleka mkopo huo  moja kwa moja kwenye sehemu yenye faida, kwa lengo la kuongeza faida zaidi.

Faida utakayopata kwenye biashara ndiyo itatumika kulipa mkopo huo na siyo fedha kutoka kwenye vyanzo vyako vingine. Hivyo, yakupasa ukokotoe vizuri hesabu zako na  ujiridhishe kuwa faida utakayopata itatosha angalau kulipa mkopo na wewe ukabakiwa na sehemu ya faida.

Usichukue Mkopo Kwa Ajili ya Mtaji wa Biashara Mpya

Kuwa makini na mkopo kwa ajili ya mtaji wa biashara mpya. Usichukue kabisa mkopo wa aina hiyo.  Huo unaweza usiwe mkopo mzuri, kwa sababu unapoanza biashara mpya, hakuna faida yoyote unayoweza kupata. Lakini pia, unakuwa hauna uelewa wala uzoefu na biashara hiyo. Ikumbukwe kuwa biashara zina changamoto na hatari (risks) nyingi.

Kabla ya kuchukua mkopo kwa ajili ya kukuza mtaji wa biashara mpya. inashauriwa kujipa muda wa kutosha ili  kujua changamoto na hatari za biashara yako na ukishaifahamu vizuri, ndipo unaweza kuchukua mkopo kwa ajili ya kukuza mtaji biashara hiyo.

Ukikopa ili upata mtaji wa kuanzisha biashara mpya, utaanza kulipa marejesho ya mkopo kabla hata biashara haijaanza kukupatia faida. Katika hali hii, utalazimika kuchukua mtaji kwenye biashara ili kulipa mkopo au kulipa mkopo kwa kutumia fedha kutoka kwenye vyanzo vingine.

Kujua tofauti kati ya mikopo mizuri na mikopo mibaya bonyeza hapa

Unaweza pia kupata kitabu kizuri kuhusu elimu ya mikopo na mambo mengine kuhusu fedha kwa kubonyeza hapa

Usihadaike na Kauli za Wakopeshaji

Kuna watu huwa wanajikuta wamechukua mikopo baada ya kushawishiwa na kauli za wakopeshaji na hata watu wengine ambao wana mikopo.

Kwa kuwa siku hizi taasisi za kukopesha ni nyingi, ukiwa mfanyakazi ambaye mshahara ni wa uhakika au unafanya biashara ya uhakika na una mali za kuweka dhamana, wakopeshaji watakuwinda sana wakukuposhe maana watakuwa na uhakika kuwa utaweza kurejesha mkopo wao. Kwa sababu hiyo watatumia kila mbinu kukushawishi wakitumia kauli mbalimbali.

Kumbuka kuwa mikopo ni biashara kama biashara nyingine. Mojawapo ya mbinu ya kupata wateja katika biashara ni ushawishi. Hivyo, wakopeshaji nao wako kwenye biashara, na ili wapate wateja lazima wawashawishi watu kwa mbinu mbalimbali.

Baadhi ya kauli za wakopeshaji ni kama vile “wewe unakopesheka” au “mfanya biashara asipokopa hawezi kukua kibiashara” au “Mtu huwezi kuishi bila kudaiwa” au ‘usipokopa utachelewesha maendeleo yako” au “hakuna mtu anayeendelea duniani bila kukopa” au “kama serikali inadaiwa, sembuse wewe?” na kauli nyingine nyingi.

Kosa ambalo hupaswi kulifanya ni kukopa kwa sababu tu eti wengine wanakopa au kwa sababu wakopeshaji wamekuambia unakopesheka au kwamba usipokopa unajicheleweshea maendeleo.

Mkopeshaji anapokwambia “unakopesheka” hana maana kuwa mkopo huo utakuwa mzuri kwako au ana uchungu sana na maendeleo yako, bali anachomaanisha ni kwamba mkopo anaokushawishi kuchukua, ana uhakika kuwa una uwezo wa kuulipa.

Hivyo, usikope kwa sababu unakopesheka bali kopa kwa sababu unahitaji mkopo na kwamba mkopo huo ni mzuri kwako.

 Je, ni Kweli Kwamba Huwezi Kuendelea Bila Kukopa?

Pamoja na maonyo na mifano halisi ya hatari za mikopo kutoka ndani na nje ya Maandiko Matakatifu, watu wengi wanapuuzia uwezekano wa hatari hizo kutokana na kuaminishwa kuwa mikopo ni muhimu sana katika kufikia mafanikio ya kiuchumi.

Ipo dhana katika jamii nyingi duniani hususani katika biashara kuwa ni vigumu kuendelea bila kukopa. Baadhi ya watu  wanapinga mafundisho yanayotoa tahadhari dhidi ya hatari za mikopo kwa madai kwamba mafundisho kama hayo yanawafanya watu wasiendelee kiuchumi.

Watu kama hao huwa wanatoa mifano mingi ya watu waliofanikiwa kwa kutumia mikopo na watu ambao wanasuasua kimaendeleo kwa sababu ya kutokuchukua mikopo. Hata hivyo, watu hao huwa hawatoi mifano ya watu walio na hali mbaya kimaisha au kibiashara kwa sababu ya mikopo.

Ni kweli kabisa kwamba mikopo inaweza kukusaidia kupiga hatua kubwa kimaendeleo. Na ipo mifano dhahiri ya hilo. Lakini si kweli kwamba huwezi kuendelea bila kuchukua mkopo.

Ipo mifano mingi ya watu ambao walifanikiwa kibiashara na kimaisha bila kuchukua mikopo bali  wamefanikiwa kwa kuzingatia tu kanuni za msingi kuhusu usimamizi wa fedha zao au biashara zao ikiwemo kuwa na vyanzao vingi vya mapato, kuweka akiba kwa ajili ya uwekezaji na pia kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha zao.

Huenda watu hawajui, lakini yapo makampuni makubwa duniani ambayo hayana mkopo wowote na mengi kati ya hayo hayajawahi kuchukua mkopo wa aina yoyote. Ukiacha makampuni, wapo pia watu binafsi waliofikia mafanikio makubwa ya kiuchumi bila mikopo. Kwa leo sitawataja kwa kuwa sijapata ridhaa yao. Naomba kwa leo nikutajie tu baadhi ya makampuni yasiyo na mikopo.. Baadhi ya makampuni hayo ni kama ifuatavyo:

Apple – Hii ni kampuni ya kimataifa ya teknolojia ya Marekani ambayo inaunda na kuuza bidhaa mbalimbali za teknolojia, programu za kompyuta na huduma za mtandaoni. Bidhaa za kampuni ya Apple ni pamoja na simu za mkononi za iPhone, vishikwambi vya iPad, kompyuta za Mac na bidhaa zingine. Hii ndiyo kampuni inayoongoza kwa thamani kubwa duniani.

Amazon – Hii ni kampuni kubwa kabisa duniani ya uuzaji wa bidhaa mtandaoni. Kwa kipimo cha mapato na mtaji wa soko, ni kampuni ya pili baada ya Alibaba Group kwa jumla ya mauzo. Amazon ni kampuni ya pili kwa thamani duniani (nyuma ya kampuni ya Apple), kampuni kubwa ya intaneti kwa mapato duniani, na baada ya Walmart, ni mwajiri wa pili mkubwa nchini Marekani.

Mwanzilishi wa Amazon ni Jeff Bezos ambaye kwa sasa  ndiye tajiri namba mbili duniani na kabla ya hapo aliwahi kuwa tajiri namba moja duniani kwa muda wa miaka minne mfululizo (2017-2020) kabla hajazidiwa na Elon Musk.

The American Express – Ni kampuni ya Marekani inayojishughulisha na masuala ya fedha na ndiyo mmiliki wa credit card iitwayo American Exopress ambayo inachukua karibu robo ya miamala yote ya credit cards nchini Marekani.

Starbucks – Ni kampuni ya kimataifa yenye makao yake makuu nchini Marekani ambayo inajishughulika na uuzaji wa kinywaji cha kahawa na bidhaa nyingine za kahawa. Hii ndiyo kampuni kubwa duniani katika biashara hiyo.

Kauli kwamba huwezi kuendelea bila mkopo hasa kwenye biashara si sahihi. Hivyo, ninarudia tena ushauri wangu kuwa, usichukue mkopo wowote kama mkopo huo utaulipa kwa fedha zako mwenyewe. Kigezo pekee cha kuchukua mkopo ni kama mkopo huo utaulipa kwa fedha za wengine.

Mkopo pekee unaoweza kuuchukua na ukaulipa kwa fedha zako mwenyewe ni mkopo ambao utakuwezesha kuokoa maisha yako au ya watu wako wa karibu. Na utafanya hivyo baada ya njia zingine zote kushindikana. Zaidi ya hapo, kamwe usichukue mkopo. Hata hivyo, hata mkopo wa kukuwezesha kuokoa maisha yako au ya watu wa karibu nao unaepukika ikiwa utajioanga vizuri na kuweka mipango mizuri ya kukabiliana na dharura na majanga kama vile kuweka akiba na kuwa na bima mbalimbali.

Makala haya yataendelea………..

Endelea kufuatilia mtandao huu ili upate mwendelezo wa makala haya.  Ili usipitwe na makala yoyote, unaweza kujiunga na mtandao huu wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio ili uweze kupata makala moja kwa moja kupitia email yako kila kunapowekwa makala mpya.

Kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *