Rafiki yangu mpendwa , tunaendelea na mfululizo wa makala kuhusu mada ya mikopo na madeni.
Katika makala yaliyopita, tuliangalia namna ambavyo mtu ambaye hana madeni anavyoweza kuepuka kuingia katika madeni. Katika makala ya leo, tutaangalia namna mtu aliye tayari katika madeni anavyoweza kutoka katika madeni hayo na kuwa huru.
Kuondokana na mikopo kunaweza kufananishwa na vita ya kupigania uhuru wa nchi. Watanzania tunafurahia maisha mazuri leo kwa sababu baadhi ya wahenga kama vile Mwalimu Julius Nyerere na wenzake walijitoa mhanga kupambana hadi tukapata uhuru. Walipitia magumu mengi na baadhi yao walipoteza maisha.
Hivyo ndivyo ilivyo kwenye kutafuta uhuru dhidi ya madeni. Yakupasa kuwa tayari kupitia mateso na maisha magumu ili uweze kuwa huru. Huwezi kutoka katika madeni kama hutakuwa na dhamira ya dhati ya kufanya hivyo.
Mwandishi maarufu wa vitabu vya kikristo aitwaye Ellen G.White katika kitabu chake kiitwacho Counsels on Stewardship, uk. 257 ana haya ya kusema kuhusu namna ya kutoka katika madeni:
“Usisite, usikate tamaa wala kurudi nyuma. Ikane ladha tamu, kataa uendekezaji wa uchu wa vyakula/vinywaji, hifadhi senti zako upate kulipa madeni yako. Yamalize haraka iwezekanavyo. Utakapoweza kusimama tena kama mtu huru, ikiwa hudaiwi na mtu yeyote kitu chochote, utakuwa umepata ushindi mkubwa”.
Hatua za kuchukua ili uondoke kwenye mikopo mibaya
Baadhi ya hatua unazoweza kuchukua ili kuwa huru na madeni ni hizi zifuatazo :
- Kama una madeni mengi, anza kwa kuorodhesha madeni yote uliyonayo ikiwa ni pamoja na madeni rasmi uliyokopa benki na kwenye taasisi za taasisi na madeni uliyokopa kwa ndugu, jamaa, marafiki na au kwenye biashara za wengine.
2. Andaa mpango maalum wa kulipa madeni yako. Unaweza kuanza kulipa madeni unayolipa moja kwa moja na kisha yale unayokatwa kutoka kwenye mshahara kama wewe umeajiriwa.
3. Unaweza kupanga kulipa kwa asilimia. Kama utapanga kulipa madeni yako kwa asilimia, inashauriwa iwe kuanzia asilimia 10 %. Ni vizuri ukapanga kulipa kwa asilimia kubwa kwa kadiri iwezekanavyo ili uweze kutua furushi la madeni mapema.
4. Weka mpang maalum wa kuweka akiba. Pamoja na kuanza mpango maalum wa kulipa madeni, hakikisha unaweka akiba kwa ajili ya dharura na uwekezaji. Usipokuwa na akiba, unaweza kujikuta unaingia tena kwenye madeni iwapo dharura itatokea
5. Kama una mkopo zaidi ya mmoja, amua uanze na mkopo upi. Zipo njia tatu za kuamua uanze kulipa mkopo upi kwanza;
a. Kuanza kulipa mkopo ambao ni mkubwa zaidi. Hii itakuwezesha kutua furushi zito la madeni mwanzoni ili kupata unafuu kadiri mzigo unavyopungua;
b. Kuanza kulipa deni dogo zaidi, hii itakupa hali fulani ya ushindi kwa kuona deni linapungua;
c. Kuanza kulipa deni linalokuumiza zaidi, kwa ukubwa wa riba, au usumbufu wa aliyekukopesha. Hapa unaanza kulipa mkopo ambao una riba kubwa zaidi, au mkopo kutoka kwa mtu msumbufu.
6. Kama mkopo pekee ulionao ni wa kukatwa kwenye mshahara, fanya mapitio ya mkopo huo na uone namna ya kulipa na kuumaliza mapema iwezekanavyo hata kabla ya muda wake.
7. Usifanye kosa la kuhamisha au kuuza mkopo wako kutoka beni moja aua taasisi ya kifedha moja kwenda nyingine au kutoka kwa mkopeshaji mmoja kwenda kwa mwingine. Kwa mfano, kama unadaiwa na benki ya CRDB, usifanye kosa la kwenda kuchukua mkopo benki ya NMB ili kutumia sehemu ya mkopo huo kulipa mkopo CRDB na kubakiwa na change kwa ajili ya shughuli zako nyingine. Ukifanya hivi utaingia gharama zaidi na itakuchukua muda mrefu zaidi kumaliza deni.
8. Ongeza kipato chako ili usilazimike kuingia kwenye madeni tena. Baadhi ya njia unazoweza kuzitumia kuongeza kipato ni kama ifuatavyo:
- Kufanya kazi kwa bidii na kwa juhudi na maarifa zaidi,
- Kuanzisha biashara kama huna na kama unayo anzisha biashara nyingine au panua uliyo nayo,
- Uwekezaji wa aina mbalimbali
- Kuuza vitu ulivyonavyo ambavyo huvitumii.
- Kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha.
Soma: Ukifanya Haya Utajiepusha na Hatari ya Kuingia Kwenye Madeni Mabaya
Kuhusu Kukopesha
Japo mara nyingi wanaoteswa na mikopo ni wakopaji lakini kuna wakati wakopeshaji hasa wakopeshaji binafsi, nao huwa wanaingia katika changamoto pale waliowakopesha wanaposhindwa kurejesha mkopo. Pamoja na kwamba Biblia inaruhusu kukopesha, ni vizuri kuwa makini kabla ya kuamua kumkopesha mtu yeyote.
Mtu unayemkopesha anaweza asiwe mwaminifu na akashindwa kurejesha fedha yako na ukaipoteza. Matokeo yake kunaweza kutokea uadui kati yako na huyo uliyemkopesha kama utashindwa kumsamehe. Ili kuepuka matatizo haya na mengineyo, yafuatayo ni baadhi ya mambo ya msingi unayopaswa kuyazingatia kabla ya kuamua kumkopesha mtu yeyote:
- Angalia kwanza uwezekano wa kumsadia badala ya kumkopesha. Kama utaona ni vigumu kumsadia, basi mkopeshe kiasi cha fedha ambacho uko tayari kukipoteza ikitokea ameshindwa kukulipa. Kumbuka kuwa unapokopesha, lolote linaweza kutokea. Mtu uliyemkopesha anaweza kushindwa kukulipa kwa sababu yoyote ile iwe sababu ya msingi au akaamua tu kutokukulipa.
- Ili kumsaidia mtu anayeomba mkopo awe na nidhamu ya matumizi ya fedha, usimkopeshe kwa ajili ya matumizi yasiyo ya muhimu wala yasiyo ya lazima. Kwa maneno mengine, usimkopeshe mtu fedha anayoenda kuitumia kwa mahitaji yasiyohusiana na kuokoa uhai au yasiyohusiana na uzalishaji wenye lengo la kupata faida.
- Usimkopeshe mtu kiwango cha fedha ambacho unadhani hataweza kurejesha. Hivyo, dadisi makusudi ya mkopo na mpango wa marejesho na ujiridhishe kuwa anaweza kurejesha mkopo ikiwa mambo yataenda kama yalivyo au ikiwa hayatatokea mambo yaliyo nje ya uwezo wake. Ikiwa hutaridhika kwamba anaweza kurejesha mkopo, basi usimkopeshe.
Kudhamini Wakopaji
Ni jambo la kawaida mtu anapoomba mkopo hasa kwenye benki na taasisi za fedha kutakiwa kuwa na wadhamini. Majukumu ya mdhamini ni pamoja na kuhakikisha kuwa mkopaji anarudisha mkopo kulingana na makubaliano.
Mdhamini anaweza kuwajibika kwa lolote litakalomtokea mkopaji ikiwepo kukimbia au kushindwa kulipa mkopo wake. Endapo mkopaji atashindwa kutekeleza majukumu yake hayo, mdhamini atawajibika kwa kulipa deni analodaiwa mkopaji.
Kutokana na hatari zinazoweza kutokea kwa mdhamini iwapo mkopaji atashindwa kulipa mkopo, Biblia inatoa tahadhari juu ya kudhamini mkopaji. Baadhi ya mafungu yanayotoa tahadhari hiyo ni:
“Amdhaminiye mgeni hakosi ataumia; Achukiaye mambo ya dhamana yu salama” (Mithali 11:15);
“Aliyepungukiwa na akili hupana mkono na mtu; Na kuwa mdhamini mbele ya mwenzake (Mithali 17:18);
“Usiwe mmoja wao wapanao mikono; Au walio wadhamini kwa deni za watu; Kama huna kitu cha kulipa; Kwani ukaondolee kitanda chako chini yako? (Mithali 22:26-27).
Kutokana na tahadhari hizi kutoka katika Neno la Mungu, ni vizuri tukafikiria mara mbili kabla ya kumdhamini mtu. Kama hauko tayari kulipa deni iwapo mkopaji atashindwa kulipa kwa sababu yoyote ile bora usimdhamini.
Ungependa kujifunza zaidi kuhusu mada hii?
Kama unapenda kujifunza ziadi kuhusu mada hii, jipatie kitabu kizuri kiitwacho “Siri za Mafanikio ya Kifedha katika Ndoa na Familia: Kanuni za Kibiblia na Kiuchumi na Kukabiliana na Migogoro na Changamoto za Kifedha Katika Ndoa na Familia”, basi fanya utaratibu ukipate.
Katika kitabu hiki, utajifunza mambo mengi kuhusu elimu ya fedha kwa muktadha wa kibiblia na namna unavyoweza kuitumia elimu hiyo katika kusimamia fedha zako kama mwanandoa na mwanafamilia. Ndani ya kitabu hiki, suala la mikopo na madeni limechambuliwa kwa kina. Ili kupata maelezo zaidi kuhusu kitabu hiki na namna ya kukipata bonyeza hapa.
Makala haya yataendelea………..
Endelea kufuatilia mtandao huu ili upate mwendelezo wa makala haya. Ili usipitwe na yoyote, unaweza kujiunga na mtandao huu wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio ili uweze kupata makala moja kwa moja kupitia e-mail yako kila zinazowekwa kwenye mtandao.
Kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini au bonyeza hapa.