Rafiki yangu katika Kristo,
Maneno “ushirikina” na uchawi si mageni masikioni mwetu na kwenye fikra zetu. Imekuwa ni kawaida kuona katika sehemu mbalimbali watu wakiitwa wachawi au washirikina kwa sababu mbalimbali.
Kwa mfano, katika jamii niliyozaliwa na kukulia, wanawake wenye macho mekundu hasa vikongwe hutuhumiwa kujihusisha na uchawi kwa kuwaloga watu wengine. Lakini pia, baadhi ya matajiri na waliofanikiwa katika jamii nyingi, hutuhumiwa kuwa wamepata mafanikio hayo kwa njia za kishirikina.
Hapa Tanzania, inasemekana kuwa, zaidi ya asilimia tisini ya wananchi wake wanaamini katika imani za kishirikina. Yaani, kuna wale ambao wanazitumia imani za kishirikina kufanikisha mambo yao na kuna wengi ambao hawazitumii ila wanaamini kuwa kuna wanaozitumia kufanikisha mambo yao.
Kutokana na imani za ushikirikina hapa nchini tumeshuhudia mauaji ya vikongwe, na pia tumeshuhudia mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino). Tumekuwa kila siku tukiona watu wanazungumuzia na hata kuhubiri kuhusu freemason na habari nyingine za kichawi.
Pia tumeona watu wakitoa ushuhuda kwamba walikuwa wanafanya mambo haya ya kichawi na hivyo kuua watu au kufanya mambo mengine ya hatari ili kufikia mafanikio katika kazi, biashara, mahusiano,siasa, michezo na hata dini.
Swali ni je imani hizi ni za kweli? Je ni kweli watu wanafikia mafanikio makubwa kupitia imani hizi za kishirikina? Maswali haya na mengineyo, nitayajibu katika mfululizo wa makala kadhaa kuanzia toleo hili.
Sitaki nikupe jibu rahisi tu kwamba uchawi upo au haupo au uchawi una ngvu au hauna nguvu kama ambavyo mmekuwa mkipata majibu haya rahisi. Mimi nitakwenda taratibu na kuingia ndani kidogo kuona ni jinsi gani imani hizi zinaweza kuwa na nguvu au zisiwe na nguvu. Pia nitakupatia njia nzuri ya wewe kuweza kufikia mafanikio makubwa bila hata ya kutumia uchawi.
Nitakueleza hayo kwa kutumia uelewa na uzoefu wa kawaida na pia nitatumia sayansi ya tabia (behavioural science), saikolojia ya binadamu (human psychology) na Biblia kuona ni jinsi gani yale yanayozungumzwa na kufanywa ni ya kweli au ya uongo.
Kupitia mfululizo wa makala haya, utaweza kupata mwanga mkubwa utakaofungua milango ya mafanikio bila ya kuvaa hirizi au kuaminishwa vitu visivyo vya kweli.
Katika mfululizo wa makala haya, tutajifunza yote yanayohusiana na mafanikio na uchawi na mwisho tutaondoka na fomula ambayo tutaweza kuitumia kufikia mafanikio makubwa.
Uchawi ni nini na unatofautianaje na ushirikina?
Kabla ya kuendelea mbele, ni vema tupate maana ya uchawi na ushirikina.
“Uchawi” ni neno la Kibantu na “ushirikina” ni neno lililotoholewa kutoka neno “shirk” katika lugha ya Kiarabu.
Kwa neno “uchawi”, Wabantu hutaka kueleza imani katika nguvu za pekee za kufanyia maajabu yasiyowezekana kwa nguvu za kawaida, kama vile, kuruka na ungo, kuwadhuru (kuwaloga) watu kutoka mbali, kuhamisha mazao ya watu kutoka shamba moja kwenda shamba jingine, kuwatumikisha watu walio usingizini, kugeuza watu kuwa nyoka au ngedere, kupita katika milango na madirisha yaliyofungwa na kadhalika.
Neno “shirk” lina maana nyingi. Kati ya maana hizo, neno “shirk” hutumiwa na waarabu kumaanisha kitendo cha mwanadamu kukishirikisha kitu nguvu ambazo ni za Mungu peke yake. Kwa mfano, mtu kuamini kwamba kitu fulani, tuseme mtu au kijiti kinaweza kumlinda anayekitumia, kunyesha mvua au kuleta bahati na kadhalika.
Hivyo, kimsingi maneno haya mawili yanaeleza imani ile ile moja kwamba kuna nguvu za pekee ambazo kwazo wanadamu wanaweza kutendea mambo ya ajabu tofauti na nguvu za Mungu.
Matumizi ya neno lipi kati ya uchawi au ushirikina ni maamuzi yetu. Wanaoelekea kubaki na Ubantu hutumia zaidi neno “uchawi” na wale wanaotaka kuvuka ngazi za lugha ya Kibantu, kwa kujua au kwa kutokujua, hulitumia zaidi neno “ushirikina”.
Je, uchawi upo au ni imani tu?
Kumekuwa na mitazamo mbalimbali juu ya uwepo au kutokuwepo kwa uchawi na imani juu yake. Pamoja na mitazamo hii, lakini ukweli ni kwamba uchawi upo maana hata biblia inathibitisha hilo.
Tangu zamani za Farao wa Misri na nyakati zilizofuata wanatajwa wachawi wengi katika maandiko (Kutoka 7:11; Yoshua 13:22; 1 Samweli 28:9; 2 Wafalme 21:1-2,6; Isaya 19:3; Isaya 57:3; Danieli 2:2; Danieli 5:7).
Hata baada ya Yesu Kristo kuzaliwa, nyakati za kanisa la awali wachawi waliendelea kuwepo. Kwa mfano, alikuwepo mchawi mmoja aliyeitwa Simoni aliyekuwa akifanya uchawi katika taifa la wasamaria (Matendo 8:9-11). Mchawi mwingine anayetajwa ni Bar-Yesu au Elima (Matendo 13:6-8).
Mungu aliweka sheria kwa lengo la kuwaondosha wachawi nyakati hizo (Kutoka 22:18; Mambo Ya Walawi 20:27) na akaeleza jinsi watu wake wasivyopaswa kuloga au kufanya ushirikina na mashetani maana hayo ni machukizo kwa Bwana (Mambo ya Walawi 19:26; Kumbukumbu la Torati 18:9-14). Kama uchawi usingekuwepo, Mungu asingeweka sheria hii. Hivyo, suala la kuwepo kwa uchawi liko wazi katika maandiko na nje ya maandiko matakatifu.
Katika makala yajayo tutaangalia kama uchawi unaweza kumsaidia mtu kupata mafanikio ya kiuchumi au la. Endelea kufuatilia.
Je, unataka kupata makala endelevu kuhusu mafaniko kwa mkristo?
Kama unataka kuendelea kujifunza kuhusu masuala mbalimbali juu ya mafanikio kwa mkristo unaweza kujiunga na mtandao huu ili uweze kupata makala mbalimbali. Kwa kufanya hivyo, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa katika mtandao huu.
Ili kujiunga, jaza fomu iliyoko hapa chini.