Hivi Ndivyo Watu Hutajirika kwa Kutumia Ushirikina – 2

Rafiki yangu katika Kristo,

Tunaendelea na mfululizo wa makala kuhusu uhusiano kati ya ushirikina na utajiri. Katika makala haya, tutaangalia kama ushirikina unaweza kusaidia kupata utajiri na mafanikio mengine au la.

Kupata makala ya nyuma kuhusu mada hii, bonyeza hapa.

Pengine, swali muhimu la kujiuliza ni hili: Je ni kweli ushirikina unaweza kuleta utajiri? Jibu la swali hili ni HAPANA. Ushirikina hauwezi kumletea mtu yeyote utajiri wala mafanikio ya aina nyingine, bali mtu mwenyewe ndiye anaweza kujiletea utajiri kwa kuwezeshwa na Mungu. Nafasi ya ushirikina katika mafanikio ya mtu ni kumpa tu imani isiyotetereka kwamba anaweza kupata mafanikio. Kwa imani hii mtu anafanya kila anachoweza ili afikie utajiri ambao amehakikishiwa kwamba unaweza kuupata kupitia ushirikina.

Imani ya kishirikina inafanyaje kazi?

Tunaweza kuelewa namna ushirikina unavyofanya kazi kama tutaelewa akili ya mwanadamu inavyofanya kazi. Wanasaikolojia hugawanya akili ya mwanadamu katika hali tatu. Ya kwanza ni akili tunayotumia kufikiri na kufanya maamuzi (conscious mind).  Akili ya pili ni ile inayopokea na kutoa kila unachofikiri bila kufanya maamuzi (sub-conscious mind). Na ya tatu ni akili yenye kuongozwa kwa imani (super-conscious mind).

Kwenye masuala ya mafanikio, kwa kiasi kikubwa, akili inayoathiri maisha ya mwanadamu ni subconscious mind. Hii ni akili ambayo haiwezi kutofautisha kati ya mema na mabaya bali inapokea tu chochote inacholetewa na inavitoa vitu hivyo katika maisha ya kawaida kama vilivyo. Hii ndiyo sababu mtu anapofikiria kitu fulani kila wakati huwa kinamtokea. Kwa mfano, mtu ukifikiria ugonjwa fulani mara kwa mara, unaweza kujikuta unaugua ugonjwa huo au mtu akiwa anaongelea ajali, anaweza kupata janga hilo.

Hivyo ndivyo ilivyo hata kwenye mafanikio ya aina yoyote ikiwemo utajiri. Mtu anayewaza mafanikio mara kwa mara ana uwezekano wa kuyapata na mtu ambaye mawazo yake yamejazwa na umaskini kila wakati, anaweza kujikuta anatumbukia kwenye dimbwi la umaskini au kama ni maskini anaweza kuendelea kuwa maskini. Kwa kifupi, akili ya mwanadamu huvuta kile anachofikiria mara kwa mara na kukileta katika maisha yake.

Kwa nini baadhi ya watu hufanikiwa na wengine hawafanikiwi?

Kwa muktadha wa hayo niliyoyaeleza, swali la wazi ambalo bila shaka umejiuliza ni hili, kama ni kweli kwamba akili huvuta kile unachofikiria mara kwa mara, iweje sasa baadhi ya watu hufanikiwa na wengine hawafanikiwi kimaisha wakati watu wengi hufikiria mafanikio zaidi kuliko kutofanikiwa?

Kama nilivyoeleza hapo awali, sub-conscious mind hupokea kila kitu kinacholetwa kwake na haina uwezo wa kutofautisha mema na mabaya.Yaani, mawazo fulani yakiingia akilini mwako, sub-conscious mind,  huwa inayafanyia kazi na kuleta mazingira ya mawazo hayo katika maisha yako. Kwa mfano, kama unafikiria sana kuwa na maisha ya mafanikio kiuchumi, akili yako, itaanza kukutengenezea mazingira hayo lakini kama baadaye utawaza kuwa huwezi kufanikiwa kwa sababu fulani fulani, akili yako itachukua mawazo hayo hasi na kukuletea mazingira ya kushindwa. Kwa namna hiyo, unaweza usipate mafanikio kwa sababu ya kukosa uhakika na kitu kimoja unachotaka maishani mwako.

Imani za ushirikina zinawasaidiaje watu kufanikiwa?

Pamoja na kwamba ushirikina kwa wenyewe hausaidii kabisa kukuletea mafanikio ya aina yoyote, lakini imani ya mtu husika katika mafanikio ndiyo inamfanya afanikiwe. Kinachotokea hapa ni kwamba mtu anaaminishwa kwamba kwa kufanya kitu fulani ni lazima apate mafanikio anayoyataka. Kwa mfano, mtu anaweza kuambiwa na mganga wa kienyeji kwamba ili upate utajiri inabidi afanye vitu fulani kama vile kuvaa pete ya ina fulani, hirizi, shanga au asioge kwa mwezi mzima.

Mtu akipewa masharti haya, atajitahidi kufanya hivyo kwa uaminifu mkubwa huku akiwa na asilimia mia moja kwamba atapata utajiri. Ikitokea kweli amepata utajiri, kilichomfanya awe tajiri siyo pete, hiziri, shanga au kutooga kwa mwezi mzima bali  ni ile imani yake na mawazo kwamba anaenda kupata utajiri kitu ambacho angeweza kukifanya hata bila ya kuvaa pete, hirizi, shanga na kutooga kwa mwezi mzima. Zaidi ya masharti yanayojenga Imani, waganga wa kienyeji hutoa masharti mengine ambayo yanamtaka mtu kufanya vitu fulani ambavyo ndivyo hasa huleta utajiri. Tutayachambua masharti hayo kwenye masomo ya mbele.

Hii haitokei kwa wanaoamini ushirikina tu, bali hata waumini wa dini mbalimbali. Ndiyo maana kuna watu wanadai wanapokea miujiza ya utajiri baada ya kuombewa na wengine baada ya kutimiza masharti fulani waliyopewa na kiongozi wa dini kama vile kutoa sadaka au fungu la kumi, kununua kitambaa, maji na mafuta ya upako.

Miujiza hii inayodaiwa kutokea inatokana na imani za watu kwamba wanaweza kupata utajiri. Swali la kujiuliza ni hili, kama kweli utajiri unatokana na kutimiza masharti unayopewa na viongozi wa dini kama vile kutoa sadaka na fungu la kumi, kununua mafuta ya upako na kadhalika, mbona kuna watu wengi matajiri duniani ambao hawajawahi kabisa kutoa sadaka na fungu la kumi wala kutumia mafuta ya upako?

Kwa kusema haya simaanishi kuwa watu wasitoe sadaka wala fungu la kumi. La hasha. Utoaji wa sadaka na fungu la kumi ni ibada ambayo iko kwa mujibu wa Maandiko na wote waliompokea Yesu hawana budi kutoa. Lakini ninachotaka kusema tu ni kwamba unapotoa sadaka na fungu la kumi msukumo wako usiwe kupata utajiri bali utoe sadaka kama shukrani kwa Mungu wako kwa mambo makubwa anayokufunyia na utoe fungu la kumi kama utii kwa Mungu wako.

Mpenzi msomaji, hapa nimeeleza kwa kifupi na juu juu sana ili kukupa picha tu ya nafasi ya imani katika mafanikio. Nakukaribisha uendelee kufuatilia mtandao huu ili uweze kuendelea kujifunza kwa undani zaidi masomo haya lakini nikupe tu tahadhali wamba usiendelee kudanganywa kwamba unaweza kupata utajiri kwa ushirikina au kimiujiza.

Nimalizie kwa swali la tafakari. Je, umewahi kujiuliza, inawezekanaje waganga wa kienyeji wawapatie watu utajiri na mafanikio mengine wakati waganga wenyewe hawana mafanikio hayo? Jibu la swali hili tutalipata katika sehemu inayofuata ya mwendelezo wa makala haya. Endelea kufuatilia.

Je, unataka kupata makala endelevu kuhusu mafanikio kwa mkristo?

Kama unataka kuendelea kujifunza kuhusu masuala mbalimbali juu ya mafanikio kwa mkristo unaweza kujiunga na mtandao huu ili uweze kupata makala mbalimbali. Kwa kufanya hivyo, utapata makala kupitia email yako kila yanapowekwa katika mtandao huu.

Ili kujiunga, jaza fomu niliyoko hapa chini.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *