Nendeni Chuoni Mkijua Hakuna Ajira Na Mliofeli Pambaneni na Hali Zenu.
Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Karibu katika sehemu ya pili ya waraka wa wazi kwa wahitimu wa kidato cha sita 2023.
Katika sehemu ya kwanza ya waraka huu niliwakumbusha wale waliofaulu mtihani wa kidato cha sita kuwa kwa sasa dunia nzima kuna tatizo la ajira na hivyo wanapoenda chuoni wajue hilo na wajipange kukabiliana na hali hiyo na kwa kuanzia wawe makini katika kuchagua kozi za kusoma. Hali kadhalika, niliwashauri wale ambao ufaulu wao hauwawezeshi kuendelea na masomo ya elimu ya juu kuwa kufeli shule siyo kufeli maisha na hivyo wapambane na hali zao kwa ama kutafuta njia mbadala ya kuendelea na masomo au kutafuta njia ya kuwaingiza kipato. Katika sehemu hii ya pili ya waraka, nitajielekeza katika kutoa ushauri wa jumla kwa wahihitimu wote, waliofaulu na ambao hawakufaulu mitihani yao.
Kama unataka kusoma sehemu ya kwanza ya waraka huu, bonyeza hapa.
Kwa kuhitimu kidato cha sita, yapo mambo muhimu ambayo unapaswa kuyazingatia ili uweze kufanikiwa katika nyanja mbalimbali za maisha yako, yakiwemo mafanikio ya kiuchumi,kijamii na kiroho . Baadhi ya mambo hayo ni kama ifuatavyo:
Elimu ya darasani ina mwisho lakini elimu ya maisha haina mwisho. Ni bahati mbaya kwamba watu wengi husoma kwa ajili ya mitihani tu na baada ya kumaliza masomo, huwa hawapendi kabisa kusoma chochote. Hapa ndipo wengi huwa wanapishana na mafanikio. Sasa, nyie wahitimu wa kidato cha sita, niwaeleze tu kuwa siri ya mafanikio iko kwenye kujifunza mambo mapya kila siku. Hata kama utaachana na elimu ya darasani, lakini uwe mwanafunzi wa kudumu wa elimu ya maisha.
Hivyo, bila kujali utaendelea na masomo au la, kujifunza ni kitu kisichokwepeka. Ili ufanikiwe maishani, ni lazima kila siku ujifunze kitu kipya, kwa kusoma vitabu vizuri, kusoma makala nzuri na kuhudhuria semina na mafunzo mbalimbali. Jifunze zaidi stadi za maisha zisizofundishwa shuleni kama vile elimu ya fedha, biashara na uwekezaji. Kutazama tamthilia, kufuatilia habari za watu mitandaoni, kusoma habari za udaku na magazeti siyo kujifunza.
Soma: Utashangaa Kusikia Siri hii Kutoka kwa Wasomaji wa Vitabu
Wakati wa kuanza kutengeneza kipato chako ni sasa. Kwa kuwa wewe sasa ni mtu mzima , achana na utegemezi wa kifedha. Bila kujali kama utaendelea kupewa fedha na wazazi au walezi wako au utakuwa unapata fedha kwa njia nyingine kama vile mkopo wa elimu ya juu, bado unapaswa kuanza kubuni njia za kujitengenezea kipato cha ziada.
Kwa wale mnaondelea na masomo ya elimu ya juu, ni vizuri mkaanza mazoezi ya kutengeneza fedha sasa ili upate uzoefu na hata ukimaliza masomo usipate taabu kutafuta ajira au kutafuta mtaji wa kuanzishishia biashara au uwekezaji. Jiandae sasa ili ukimaliza tu masomo yako, ukanyage tu mafuta na kuondoka kwa kasi kubwa.
Nirudie kuwakumbusha tu kuwa mnaenda kusoma lakini ajira hazipo. Hivyo mnapaswa kujiandaa kupambana na hali zenu baada ya kumaliza masomo na kukosa ajira. Kuanzia sasa, anzeni kufikiria ni biashara au uwekezaji gani unaoweza kufanya ukiwa chuoni bila ya kuathiri masomo yako. Kumbuka popote pale palipo na watu, kuna bidhaa au huduma wanazihitaji, basi fikiria ni bidhaa au huduma gani ina uhitaji mkubwa hapo chuoni na uanze kuiuza. Usibweteke na “pocket money” kutoka kwa wazazi au walezi au “boom” la chuo. Usipoanza kufanya biashara ukiwa chuoni, basi jiandae kusaga lami kwa miaka kadhaa baada ya kumaliza masomo huku ukitembea na bahasha za kaki bila mafanikio.
Kwa wale ambao hamtaendelea na masomo, hamna uchaguzi, ingieni “mzigoni” mara moja. Tafuteni pesa kama hamna akili nzuri. Tafuta kila njia halali ya kutafuta pesa. Wekeni muziki, acheni maneno. Biashara ni asubuhi, jioni ni mahesabu.. Ujana ndiyo asubuhi na uzee ni jioni. Tumieni vizuri ujana wenu ili msilaumu kila mtu uzeeni. Umizeni akili zenu ujanani ili msiumize mwili yenu uzeeni.
Usiwe tegemezi kifikra na kimaamuzi. Bila shaka, wahitimu wote wa kidato cha sita mna umri wa miaka 18 na kuendelea. Hivyo, ninyi ni watu wazima na mnapaswa kuwa watu mnaojitegemea kwa maamuzi. Hivyo, yawapasa kujifunza kufanya maamuzi muhimu ya maisha yenu wenyewe. Huu si wa wakati wa kuiga mambo wala kufanya maamuzi kwa makundi bali ni wakati wa kufanya kitu chenye maana kwako binafsi. Kwa kusema haya simaanishi usiombe ushauri. Bado unaweza kuhitaji ushauri kwa mambo mengi lakini unapoomba ushauri omba ukiwa na wazo lako juu ya jambo hilo badala ya kwenda ukiwa huna wazo lolote na kutegemea mtu mwingine akuamulie.
Uamuzi wa kwanza baada ya matokeo kutoka ni usome kozi gani kama umefaulu na kama hukufaulu amua ufanye nini ili maisha yaendelee. Katika uamuzi huu, usifuate mkumbo wala kuiga wenzako. Ni uamuzi nyeti kabisa kuhusu mustakabali wa maisha yako. Huu ni uamuzi wa hatima ya maisha yako. Hivyo, tulizana vizuri, usikurupuke ili usije kujuta baadaye.
Uishi kwa kuongozwa na malengo. Katika maisha yako, epuka kabisa kuishi bila malengo katika jambo lolote unalolifanya Epuka kufanya vitu kwa mazoea, au kwa sababu kila mtu anafanya. Kabla hujafanya chochote, ni vizuri kuwa na uelewa juu ya wapi kitu hicho kitakukupeleka na jua ni mikakati ipi utakayotumia kufikia huko unakoelekea. Kama hakikupeleki popote katika kufikia malengo yako ya maisha, achana nacho hata kama kila mtu anakifanya.
Jihadhari na watu unaohusiana nao. Upo msemo kawamba ndege wanaofanana huruka pamoja. Na tabia zako ni wastani wa tabia za watu watano wanaokuzunguka. Kama unataka kuwa na mafaniko katika maisha yako, unapaswa kuwa makini na watu wanaokuzunguka. Hapa nimaanisha marafiki na watu wengine wa karibu. Usiwe na urafiki na watu “wasiojielewa”, yaani watu ambao hawana malengo ya maisha na hivyo hawajui wanaelekea wapi.
Ili kupekana na watu “wasiojielewa”, fanya mchujo wa watu ambao unakuwa nao muda mrefu hasa katika muda binafsi tofauti na muda wa jumuia kama vile muda wa darasani. Ni bora uwe na marafiki wachache wanaojielewa na wenye msaada kwako kuliko kuwa na marafiki wengi ambao wanakupoteza.
Kwa wale mtakaoenda katika vyuo vya elimu ya juu, hakutakuwa na kubanwa banwa tena kama ilivyokuwa katika shule ya sekondari. Kila mtu yuko huru kufanya mambo yake. Msipokuwa makini mnaweza kuanza tabia za hovyo kama vile ulevi na uzinzi. Mambo haya yanaweza kuwaharibia kabisa mustakabali wa maisha yenu. Kumbuka utaenda chuoni kusoma na siyo “kula bata”. Tumia muda wako kusoma, kufanya kazi ya kuingiza fedha, kupumzika na kufanya ibada na siyo “kula bata”. Kaa mbali kabisa na “wala bata”.
Katika makala yajayo nitawaletea waraka kwa wahitimu wa elimu ya juu. Endeleeni kufuatilia.
Je, unataka kupata makala endelevu kuhusu mafanikio kwa mkristo?
Basi unaweza kujiunga na mtandao huu ili uwe unapata makala kupitia email yako kila yanapowekwa katika mtandao huu.
Ili kujiunga, jaza fomu iliyoko hapa chini.
May the Almighty God, bless you as you save Him, through impacting these knowledge to a society.