Kabla hujaingia kwenye ujasiriamali soma hapa kwanza
Karibu tena mpenzi msomaji katika mwendelezo wa waraka wa wazi kwa wahitimu wa elimu ya juu wa mwaka 2023. Katika makala yaliyopita ambayo ilikuwa sehemu ya pili ya waraka huu, nilikupatia mambo kadhaa unayopaswa kuyafahamu kabla hujaanza kusaka ajira. Kati ya mambo hayo, nilikushauri kufanya maamuzi ya kujiajiri kwa kutumia uwezo na vipaji ulivyonavyo ukichanganya na elimu uliyoipata. Njia mojawapo ya kujiajiri ni kupitia ujasiriamali. Katika makala ya leo nitakueleza mambo muhimu unayopaswa kuyafahamu kabla hujaamua kuwa mjasiriamali.
Kusoma makala ya nyuma bonyeza hapa
Katika makala yaliyopita, nilisisitiza na leo ninarudia tena kusisitiza kuwa ule ushauri maarufu kabisa wa nenda shule, soma kwa bidii, faulu vizuri na utapata kazi ya uhahika, inayolipa vizuri na kukuwezesha kuwa na maisha mazuri, ni ushauri uliopitwa na wakati. Wengi wamefuata ushauri huo, wakasoma kwa bidii katika ngazi zote za elimu na kupata ufaulu mzuri na wakahitimu wakiwa na matumaini makubwa kwamba wanakwenda kupata kazi nzuri. Lakini walipoingia mtaani walikuta hali tofauti kabisa. Pamoja na kuwa na ufaulu mzuri, hawakupata ajira na wakajikuta njia panda wakiwa hawajui nani wamlaumu.
Kwa bahati mbaya, baadhi ya watu, wakiwemo wanasiasa, wamekuwa wakiwalaumu wahitimu wasio na ajira wakiwaita wazembe na wasiojiongeza. Lawama kama hizi zimekuwa hazina msaada wowote kwa wahitimu. Pengine wanachopaswa kulaumu ni mfumo wetu wa elimu na si wahitimu wenyewe. Si haki kumlaumu mhitimu kwa kushindwa kujiajiri ambaye kwa muda wote wa zaidi ya miaka 18 (kuanzia chekecheka hadi chuo kikuu) ameandaliwa kuwa mwajiriwa. Angekuwa ameandaliwa kujiajiri halafu akashindwa, lawama hizi zingekuwa sahihi.
Wanaotoa lawama hizi, wamekuwa wanatumia mifano ya wahitimu wachache waliokosa ajira na kuchukua hatua ya kwenda kujiajiri kupitia ujasiriamali. Hawa wahitimu wachache wanaofaninikiwa kujiajiri, wana kitu ndani yao ambacho wengine hawana na hicho ndicho kinawasukuma kujiajiri. Hatuwezi kusubiri wachache wenye msukumo wa tofauti ndiyo wachukue hatua. Ni muhimu kila anayehitimu atafute hicho kitu ambacho wengine wanacho na ndipo aingie kwenye kujiajiri.
Kabla ya kuingia kwenye ujasiriamali, kuna kweli muhimu ambazo kila mhitimu anapaswa azifahamu lakini kwa bahati mbaya huwa haziwekwi wazi. Mimi nimeamua niwaeleze kweli hizo. Baadhi ya kweli hizo ni kama ifuatavyo:
1. Ujasiriamali si rahisi kama unavyofikiria: Ujasiriamali unahitaji mtu aliyejitoa kikwelikweli kwa sababu ili ufanikiwe katika ujasiriamali unahitajika kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Mambo hayo ni kama vile kutengeneza au kutafuta bidhaa/huduma, kutafuta masoko, kuuza bidhaa/huduma, na mengine mengi. Mambo haya yanaweza kuwa magumu kwa wahitimu wengi maana katika masomo yao wamefundishwa kubobea kwenye eneo fulani tu. Ujasiriamlia unakuhitaji ubobee na ufanye mambo mengi tofauti tofauti.
2. Ujasiriamali ni hatari. Tafiti kuhusu usimamizi wa biashara zinaonyesha kuwa nusu ya biashara zinazoanzishwa huwa zinakufa kabla ya miaka mitano, huku asilimia 33.3% tu zikifanikiwa kufikisha miaka kumi. Hii inamanisha kuwa 50% tu ya biashara mpya ndio hufanikiwa kuvuka miaka mitano na 67.7% ya biashara mpya hufa kabla ya kufikisha miaka kumi.
Kwa upande wake, jarida maarufu linalochapisha masuala ya biashara na uchumi la Forbes lilifanya utafiti kwa kushirikiana na kampuni ya kibiashara ya Bloomberg na kubaini kwamba biashara nane kati ya kumi zinazoanzishwa hufa ndani ya miezi 18 ya kwanza.
Pamoja na matokeo tofauti ya tafiti hizi lakini kitu kimoja ni dhahiri. Biashara zinazokufa ni nyingi kuliko zinazofanikiwa. Hivyo, wewe mhitimu unayewaza kuingia kwenye ujasiriamali unaweza kujionea jinsi hatari ilivyo kubwa. Yaani, nafasi ya kushindwa ni kubwa kuliko ya kufanikiwa. Wahitimu wengi wa elimu ya juu hawana uwezo wa kukabiliana na hatari kubwa kama hiyo.
3. Ujasiriamali unahitaji watu sahihi: Watu wengi hudhani ujasiriamali ni kuwa na wazo bora na la kipekee tu. Pamoja na wazo zuri, mafanikio ya kibiashara yanategemea uwepo wa watu sahihi wanaolifanyia kazi wazo hilo. Kupata watu sahihi wa kushirikiana nao katika biashara ni changamoto kubwa sana siku hizi. Watu wengi ni wabinafsi na si waaminifu siku hizi. Wengi wanaangalia maslahi yao tu. Lazima mjasiriamali apambane sana kupata watu watakaoelewa maono yake na kuungana naye kuyapambania mpaka yafanikiwe. Ukipata watu wasio sahihi wanaweza kuchangia kuanguka kwa biashara yako.
4. Ujasiriamali utakutenga na jamii. Katika hatua za awali za biashara unapaswa ujitoe kweli kweli na uifanye biashara kuwa kipaumbele na uachane kabisa na mambo mengi ya kijamii ili ufanikiwe. Tofauti na kazi ya kuajiriwa ambayo ina muda wa kuingia na kutoka kazini, ujasiriamali unaweza usiwe na muda unaoeleweka wa kuingia na kutoka kazini. Katika ujasiriamali, unapaswa kufanya kazi muda mwingi na kujiepusha kabisa na starehe na anasa mbalimbali. Bahati mbaya wahitimu wengi wa elimu ya juu ni vijana ambao wanapenda “kula bata”. Watu wa aina hii hawataweza kufanikiwa katika ujasiriamali, hasa katika kipindi cha awali.
5. Manufaa ya ujasiriamali siyo kwa ajili yako tu. Ujasiriamali una manufaa mengi kwako. Hata hivyo, manufaa hayo hayapaswi kuishia kwako tu. Ujasiriamali utakuwezesha kutatatua changamoto ambazo zinaikabili jamii yako na kuongeza thamani kwenye maisha yao kama vile kuwapatia bidhaa na huduma, kuwapatia nafasi za ajira na kadhalika. Lakini watu wengi wanashindwa kunufaisha jamii yao kwa sababu ya ubinafsi.
Kabla sijamaliza, nisisitize kuwa nimeeleza kweli hizi si kwa nia ya kukuogopesha au kukukatisha tamaa. Bali nimefanya hivyo, ili kukueleza hali halisi na kukuandaa kiakili na kisaikolojia ili unapoingia kwenye ujasiriamali uingie ukijua ukweli. Hii itakusaidia kujipima na kisha uamue kama utaweza au la kuliko kuingia bila kujua halafu ukakutana na mambo magumu na ukawa umepoteza muda wako.
Baada ya kuangalia kweli hizi, katika sehemu ijayo tutaangalia ni shughuli zipi za ujasariamali ambazo mhitimu wa elimu ya juu anaweza kufanya. Endelea kufuatilia.
Je, unataka kupata makala endelevu kuhusu mafanikio kwa mkristo?
Basi unaweza kujiunga na mtandao huu ili uwe unapata makala kupitia email yako kila yanapowekwa katika mtandao huu.
Ili kujiunga, jaza fomu iliyoko hapa chini.
Hello
Hapa umetoa maoni au umeuliza swali?