Hizi Ndizo Sababu Kwa Nini Baadhi ya Watu Wanaopata Fedha Nyingi Huishia kuwa Masikini

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Bila shaka umewahi kushuhudia mtu anapata fedha nyingi sana ambazo zingeweza kumtoa katika umaskini. Lakini cha kushangaza mtu huyo baada ya muda anakuwa hana fedha ten ana anaishia kuwa umaskini. Tena siyo umaskini wa kawaida bali umaskini wa kutupwa kana kwamba hajawahi kupata fedha nyingi.

Kama umekuwa ukijiuliza kwa nini hali hiyo hutokea, basi fuatana nami katika makala haya ili ujue sababu. Sitaishia tu kukueleza sababu, bali nitakueleza nini cha kufanya ili kuepuka hali hiyo.

Kabla, hatujaingia kwenye sababu za hali hiyo, nikufahamishe tu kwamba kuna misingi mikuu mitatu muhimu kuhusu fedha ambayo kila mtu anapaswa kuifahamu na kuizingatia.

Msingi wa kwanza ni jinsi ya kutafuta au kupata fedha. Kwa bahati nzhuri, msingi huu, unafahamika kwa watu wengi. Hakuna mtu asiyejua namna fedha inavyopatikana japo si njia  zote zinazotumika kupata fedha ni nzuri au halali. Bila kujali kwamba ni njia halali au si halali lakini angalau kila mtu anajua namna fedha zinavyopatikana.

Tutaendelea kujadili katika jukwa hili, njia zipi ni halali na zipi si halali maana kuna njia ambazo machoni mwa watu huonekana ni halali lakini kumbe si halali kwa Mungu na hata katika jamii.

Msingi wa pili ni namna ya kutunza fedha baada ya kuzipata. Huu msingi ndio wenye changamoto kwa watu wengi. Watu wengi wanapata fedha lakini kwa kuwa hawajui namna gani wazitumie kwa manufaa au namna gani wazitunze, hujikuta fedha hizo zinaenda katika matumizi yasiyo sahihi au matumizi yasiyo na manufaa. Hata pale zinazopotumika kwenye mambo ya manufaa, wakati mwingine hutumika kwa namna isiyo sahihi. Kwa sababu hiyo, huu ni msingi muhimu sana kwa kila anayetaka kupata mafanikio ya kifedha.

Msingi wa tatu ni namna ya  kuifanya fedha uliyoipata izae ili upata fedha nyingi zaidi. Huu pia ni msingi muhimu na ndiyo unakufanya uendelee kuwa na mafanikio ya kifedha uliyoyapata. Kwa bahati mbaya msingi huu nao haufahamiki vizuri kwa watu wengi.

Kama nilivyoeleza mwanzoni, wapo watu ambao huwa wanafanikiwa kupata fedha nyingi, tena kwa njia halali kabisa na kwa muda fulani wanakuwa na maisha mazuri kabisa  lakini  baadaye, maisha yao yanaweza kubadilika na kuwa maisha duni kabisa.  Watu hao wanaweka kugawanywa katika makundi mbalimbali. Makundi makuu ya watu wa ina hiyo yako matatu. Kabla ya kuendelea na makala yetu, naomba nikueleze kidogo kuhusu makundi hayo matatu.

Kundi la kwanza ni kundi la watu wanaopata kiasi kikubwa cha fedha kwa mpigo bila ya kuwa wameweka juhudi zozote katika upatikanaji wa fedha hizo. Kwa maneno mengine, wanapata fedha bila “kuzitolea jasho”.

Mifano ya watu hawa ni pamoja na watu wanaocheza na kushinda michezo ya kubahatisha kama vile bahati nasibu (lottery), kubeti (sports betting), kamari, kasino na michezo mingine kama hiyo. Mfano mwingine ni wale wanaopata urithi wa mali nyingi  kutoka kwa wazazi au walezi wao.

Ili uweze kuelewa ninachoeleza, jaribu kufikiria maisha ya mtu yeyote unayemfahamu aliyewahi kushinda mchezo wa kubahatisha au aliyewahi kurithi kiasi kikubwa cha mali kisha uone ana maisha gani sasa. Bila shaka umepata jibu.

Kundi la pili ni wale wanaopata kiasi kikubwa cha fedha kwa mpigo baada ya kuwa wameweka juhudi zao wenyewe katika upatikanaji wa fedha hizo. Mfano wa watu hawa ni wanamichezo na wasanii ambao wanakuwa wameonesha umahiri mkubwa na umahiri huo unawafanya walipwe donge nono.

Mfano mwingine ni wastaafu wanapolipwa mafao yao ya kustaafu. Wachimba madini pia wanaangukia katika kundi hili. Baadhi ya watu wa kundi hili wapo kwenye hatari kubwa ya kupoteza fedha zao kwa haraka na kuingia kwenye maisha ya umasikini japo hatari yao si kubwa ukilinganisha na kundi la kwanza.

Kundi la tatu ni la watu wanaopata fedha kidogo kidogo na kwa muda mrefu. Kundi hili linahusisha watu ambao wameanzia maisha ya chini sana na wakapanda tararibu na hatimaye  kujikuta wanakuwa na kipato kikubwa cha fedha baada ya muda mrefu. Kipato hicho kinaweza kuwa kimepatikana kwa njia ya mshahara, biashara na shughuli nyingine za uzalishaji mali kama vile kilimo, ufugaji na kadhalika.

Ukilinganisha na makundi mengine niliyoyataja, uwezekano wa watu wa kundi la tatu kuingia kwenye umaskini kwa muda mfupi ni mdogo. Hata hivyo, baadhi ya watu wa kundi  hili hujisahau au hufanya makosa ya kutokuzingatia misingi ya fedha niliyoitaja hapo juu na kujikuta wanapoteza kila kitu ambacho wamekifanyia kazi kwa muda mrefu.

Hadi hapa sijakueleza ni kitu gani huwafanya watu wa kundi lolote kuingia katika umaskini wa kutupwa. Naomba kwa leo tuishie hapa lakini endelea kufuatilia mwendelezo wa makala haya ili uweze kujua sababu hizo.

Ili usipitwe na makala yoyote na pia ili uweze kusoma makala ya nyuma, tafadhali jiunge na mtandao huu wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio. Kwa kujiunga utaweza kupata makala katika barua pepe yako moja kwa moja kila yanapowekwa kwenye mtandao huu.

Mtandao wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio una makala mbalimbali kuhusu mafanikio hususani katika maeneo ya biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), malezi ya watoto, namna ya kuandaa na kuwasilisha mahubiri kwa watu wazima  na kwa watoto na mada nyingine nyingi.

Kujiunga na mtandao huu jaza fomu iliyoko hapa chini.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *