Hizi Ndizo Sababu Kwa Nini Baadhi ya Watu Wanaopata Fedha Nyingi Huishia kuwa Maskini- 2

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Je, umewahi kushuhudia mtu anapata fedha nyingi sana ambazo zingeweza kumtoa katika umaskini, lakini baada ya muda anakuwa hana fedha tena na anaishia kuwa umaskini wa kutupwa? Unajua kwa nini?

Zipo sababu nyingi zinazopelekea hali hii. fuatana nami katika makala haya ambapo tutajadili baadhi ya sababu hizo.  Sababu tutakazojadili zinawahusu hasa wale wanaopata fedha nyingi kwa mpigo ambao wanaweza kuwa wamezipata kwa kuweka juhudi kubwa au wamezipata bila kuweka juhudu yoyote. Lakini wakati mwingine, sababu hizi zinaweza kuwahusu hata wale wanaojenga utajiri wao taratibu.

Kusoma makala ya nyuma kuhusu mada hii, bonyeza hapa

Sababu zenyewe ni kama ifuatavyo:

  1. Dhana kwamba ukiwa na fedha nyingi wewe ni tajiri

    Ipo dhana kwa watu wengi kwamba kipimo cha utajiri ni kumiliki fedha nyingi. Kwa sababu hiyo, watu wengi wamekuwa wakifikiri kwamba unapopata fedha nyingi basi wewe umekuwa tajiri. Hata hivyo, dhana hii si sahihi ikiwa hautazitumia fedha hizo kukuletea fedha zaidi. Ukiwa na fedha nyingi ambazo unazitumia tu bila kuzizalisha, wewe siyo tajiri bali ni maskini mtarajiwa.  

    Dhana kwamba ukiwa na fedha nyingi wewe ni tajiri, imewafanya watu wengi kuishi maisha ya kitajiri kwa maana ya kuwa na matumizi makubwa bila kujua kwamba matajiri halisi hawafanyi matumizi kwa kutumia fedha walizo nazo bali hutumia fedha wanazopata kutoka kwenye uwekezaji unaowazalishia.

    Kwa maneno mengine, matajiri hutumia faida na siyo fedha wanayomiliki bila kuizalisha. Hapo ndipo ilipo tofauti. Wewe unatumia fedha uliyonayo bila kuizalisha lakini tajiri anazalisha fedha aliyo nayo na kutumia faida. Wewe unayetumia fedha uliyo nayo bila kuizalisha hatimaye fedha hiyo itaisha tu na utakuwa maskini lakini yule anayezalisha fedha aliyonayo na kutumia faida, fedha yale itazidi kuongezeka zaidi na zaidi na kuwa tajiri zaidi.

    2. Mtazamo finyu kuhusu kiwango cha fedha

    Kwa kujua au kutojua, kila mtu hapa duniani ambaye anatafuta fedha au aliye na fedha, kuna kiwango cha fedha kwenye akili yake ambacho anaona kinamtosha kuendesha maisha. Hivyo, kila mtu anapopanga mipango yake ya kupata kipato hulenga kupata kipato kinachoendana na kiwango alichonacho akilini mwake.

    Kama, kwa mfano, kipato chako ni laki tano, unaweka hiki kama kiwango kwenye akili yako. Hivyo hata mipango yako mingi inayoweka kuhusu fedha itakuwa kwenye kiwango cha hiyo laki tano au zaidi kidogo.

    Sasa, mtu aliyeweka kiwango cha laki tano akilini, ikitokea anapata shilingi milioni mia tano, zinakuwa nyingi sana kulingana na kile kiwango kilichoko akilini mwake kwa kuwa hajawahi kuzifikiria wala kupanga kuwa nazo.

    Katika mazingira hayo, mtu huyo atajikuta anafanya vituko katika matumizi ya fedha hizo hadi pale zitakapopungua kufikia kiwango kile kilichoko akilini mwake au kiwango alichozoea kukipata. Hili ni suala la kisaikolojia zaidi na mara nyingi, humtokea mtu bila hata kujua.

    Ngoja nitoe mifano halisi ya kile ninachokieleza hapa. Niliwahi kusimuliwa kisa cha mchimbaji madini ambaye alifanya vituko baada kupata fedha nyingi. Mojawapo ya vituko hivyo ni kutumia bia kama maji ya kuoga. Yaani, alikuwa ananunua bia nyingi na kuzimwaga kwenye ndoo na kuoga bia hizo. Mtu huyo leo ni maskini wa kutupwa. Mtu mwingine ambaye nilishuhudia mwenyewe, alichukua mkopo mkubwa na kuamua kukodi gari la abiria (daladala) ili liwe linamchukua kila siku kutoka nyumbani kumpeleka ofisini na kumrudisha jioni. kila siku. Mkopo huo uliisha na hakuufanyia kitu cha maana na aliishia kufa maskini.

    3. Matumizi kuongezeka pale kipato kinapoongezeka

    Katika Sayansi ya fedha, kuna kitu cha ajabu sana kuhusu matumizi. Kitu hicho ni kwamba fedha huwa haikosi matumizi. Kitu hiki ni sababu mojawapo inayochangia watu kurudi kwenye umasikini pale wanapopata fedha nyingi kwa mkupuo. Hii inatokea pale mtu anaporuhusu matumizi yakue haraka kwa kadiri kipato kinavyoongezeka. Unakuta mtu alikuwa na maisha fulani na wakati mwingine ni maisha mazuri tu lakini anapopata fedha nyingi anaamua kuishi maisha ya juu zaidi kwa kadri fedha inavyoruhusu.

    Sasa unaporuhusu matumizi yako yaongezeke kwa sababu tu kipato kimeongezeka, matumizi hayo yanaongezeka kwa kasi kubwa sana na yanachukua sehemu kubwa ya fedha zako. Kama hutafanya jitihada za kuizalisha fedha hiyo kwa kasi ile ile uliyoongeza matumizi, hakuna namna fedha hiyo itadumu hata kama ni kubwa kiasi gani.

    4. Uwekezaji usio na tija

    Baadhi ya watu wanaopata fedha nyingi huamua kuzizalisha zaidi ili kuwa na uhakika wa kipato endelevu. Hili ni jambo zuri kabisa lakini wengi huishia kufanya maamuzi mabovu kwa sababu ya kutokuwa na ujuzi au uzoefu na masuala ya uwekezaji.

    Mwandishi George Classon katika kitabu chake, The Richest Man in Babylon, anashauri kuwa mtu asiwekeze katika eneo ambalo halifahamu vizuri. Kwa mujibu wa Classon, fedha humpotea yeyote anayewekeza kwenye eneo ambalo hana uelewa au eneo ambalo halijathibitishwa na wale ambao wana ujuzi juu yake. Hivyo, kabla ya kufanya uwekezaji wowote, ni muhimu kupata ushauri kutoka kwa watu wenye ujuzi au uzoefu katika eneo hilo. Lakini pia wewe mwenyewe itabidi uchukue muda kujifunza juu ya uwekezaji unaotaka kuufanya ili uwe na uhakika na kile unachokifanya kwa ajili ya usalama wa fedha yako.

    Mfano wa wahanga wa uwekezaji mbovu ni wastaafu. Tumekuwa tukishuhudia wastaafu baada ya kupata mafao yao, wanakwenda kuwekeza kwenye maeneo ambayo hawayajui vizuri na wanaishia kupigwa na kitu kizito. Kwa mfano, unakuta mstaafu anatumia mafao yake kufanya biashara ya daladala lakini kwa sababu hana uzoefu na magari anaishia kuuziwa gari bovu na gari hili linamletea hasara kubwa. Tatizo hapa si kwamba biashara ya daladala hailipi maana wengi wanaifanya na wamefanikiwa. Tatizo ni kwamba mstaafu huyu hana uzoefu wala ujuzi na magari.

    5. Ndugu, jamaa na marafiki.

    Kwa kawaida, fedha zinavutia watu. Watu hao ni wa aina mbalimbali, wenye nia njema na pia wenye nia mbaya. Kwa bahati mbaya, ukiwa na fedha unavutia zaidi watu wabaya, yaani wale wanaokuja kwako ili wanufaike na fedha zako. Kwa maneno mengine, wanapenda zaidi fedha yako kuliko wewe. Wanakuja kwako ili uwatatulie matatizo yao.

    Usipokuwa makini, fedha yako inaweza kuishia kutatua matatizo ya watu tu na fedha ikiisha hautawaona tena. Sisemi kuwa usiwasaidie watu, ni muhimu kusaidia watu maana fedha zako zisiposaidia jamii basi hauna sababu ya kuwepo duniani. Lakini ni vizuri ufanye hivyo kwa mahesabu ili misaada yako kwa watu isikuache maskini.

    Hadi hapa tumeona baadhi ya sababu zinazowafanya watu wanaopata fedha nyingi kuishia kuwa maskini. Sasa, nini cha kufanya ili hali hii isitokee? Endelea kufuatilia mwendelezo wa makala haya ili upate majibu ya swali hili. Kwa leo, naishia hapa. Karibu katika makala yanayofuata.

    Ili usipitwe na makala yoyote na pia ili uweze kusoma makala ya nyuma, tafadhali jiunge na mtandao huu wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio. Kwa kujiunga utaweza kupata makala katika barua pepe yako moja kwa moja kila yanapowekwa kwenye mtandao huu.

    Mtandao wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio una makala mbalimbali kuhusu mafanikio hususani katika maeneo ya biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), malezi ya watoto, namna ya kuandaa na kuwasilisha mahubiri kwa watu wazima  na kwa watoto na mada nyingine nyingi.

    Kujiunga na mtandao huu jaza fomu iliyoko hapa chini.

    About Simeon Shimbe

    Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

    Leave a Reply

    Your email address will not be published. Required fields are marked *