Hizi Ndizo Kanuni za Matumizi ya Simu ambazo Watu Wastaarabu Huzifuata

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Katika ulimwengu wa leo uliogubikwa na teknolojia, mawasiliano ya simu ni sehemu muhimu sana ya maisha yetu ya kila siku. Simu za zimekuwa zikitumika kwa kiasi kikubwa katika mawasiliano ya binafsi na ya kikazi. Hata hivyo, ni muhimu kufuata kanuni za adabu na mienendo sahihi katika matumizi ya simu ili kuhakikisha mawasiliano mazuri na kuepuka kutofautiana au kuumiza hisia za wengine. Katika makala haya, tutajadili baadhi ya kanuni muhimu za mawasiliano ya simu. Kanuni hizo ni kama ifuatavyo:

  1. Jitambulishe

Unapompigia simu mtu ambaye hamfahamiani au mnafahamiana lakini hauna uhakika kama ana namba yako ya simu, baada ya salamu, jitambulishe kabla hujaeleza unachotaka kuongea naye. Si vema kuingia moja kwa moja kwenye mazungumzo na kusubibiri uliyempigia agundue wewe ni nani au akuulize. Si vema pia kuanza kumuuliza yeye ni nani kabla wewe wewe mwenyenye hujajitambulisha.  

Baada ya kujitambulisha, jiridhishe kwamba yule uliyempigia ni yeye kabla hujaanza mazungumzo. Unaweza kufanya hivyo kwa kumuuliza, “naongea na……. (taja jina lake au cheo chake)”. Hii ni muhimu kwa sababu unaweza kuwa umekosea namba ya simu, au yeye mwenyewe amebadilisha  namba ya simu au inawezekana simu ni yake lakini aliyepokea simu ni mtu mwingine.

2. Omba Muda wa uliyempigia

Unapopiga simu, ni ustaarabu kuomba muda wa kuongea na mtu kabla hujaingia kwenye mazungumzo. Kwa mfano, unaweza kusema, ”tunaweza kuongea dakika……? (taja makadirio ya muda unaotarajia kutumia)” au “tunaweza kuongea kwa dakika……?” au “una muda tuzungumze dakika……?”

Ni muhimu kuomba muda wa uliyempigia kwa sababu kupokea simu haimanishi kwamba huyo mtu ana muda au yuko katika mazingira mazuri ya kuzungumza. Mtu anaweza kupokea simu lakini yuko katika mazingira ambayo hayuko huru kuzungumza au baada ya dakika chache utakuwa unafanya kitu ambacho huwezi kuzungumza kwa simu.

Zaidi ya kuomba muda, ni muhimu kuheshimu muda wa mwenzako. Epuka kuzungumza kwa muda mrefu kuliko inavyohitajika. Kwa mfano, unampigia mtu muda wa kazi na akakubali kukupa muda wake, si ustaarabu kuongea muda mrefu. Fupisha mazungumzo ili aendelee na kazi zake.

  1. Usipige simu mara nyingi

 Ikitokea umempigia mtu simu na hajapokea, si busara kuendelea kumpigia simu. Kupiga simu kwa mtu mara nyingi ni kusababisha usumbufu usio na sababu. Ukiona mtu hajapokea simu, amini kwamba bila shaka kuna sababu ya msingi. Usikimbie kudhani kwamba amekupuuza. Anaweza kuwa yuko katika mazingira ambayo hawezi kupokea simu au yuko mbali na simu. Ukipiga simu mara mbili haipokelewi, inatosha. Usiendee kupiga zaidi, badala yake unaweza kuandika ujumbe mfupi au ukajaribu tena baadaye. Kwa mtu mstaarabu, akikuta umempigiwa simu (missed calls) hata kama ni mara moja tu atakutafuta baadaye. Kama atapitiwa na asikutafute, unaweza kujaribu tena kumpigia.

4. Kupokea simu kwa Heshima na kwa Wakati

Unapopigiwa simu, ni muhimu kupokea kwa heshima na haraka iwezekanavyo. Ikiwa hauwezi kupokea simu, unaweza kujibu kwa ujumbe mfupi au kujaribu kuwasiliana na mtu huyo baadaye. Hali kadhalika, ikiwa umepokea ujumbe, jaribu kujibu haraka iwezekanavyo, hata kama ni kwa kuonyesha tu kwamba umepokea ujumbe huo na utaujibu baadaye. Si ustaarabu kuacha kupokea simu, au kutokumpigia baadaye mtu aliyekukosa au kutojibu ujumbe wa simu bila sababu ya msingi. Hii inaweza kumfanya mtu mwingine ajisikie kutoheshimiwa au kusababisha wasiwasi kwake. Wakati mwingine, kutokupokea simu au kutokujibu meseji kunaweza kuwa ni kwa hasara yako mwenyewe maana inawezekana simu hiyo ilikuwa kwa ajili ya jambo fulani muhimu kwako.  

5. Epuka Kuzungumza kwa Sauti Kubwa

 Kuzungumza kwa simu kwa sauti kubwa ni kelele na ni kukosa ustaarabu. Sauti ya juu inaweza kusababisha usumbufu ikiwa kuna watu wengine karibu yako. Hivyo, kanuni ya kufuata ni kuzungumza kwa sauti ambayo yule unayeongea naye ataweza kukusikia vizuri na wale walio jirani yako usiwapigie kelele.

Ili kuepuka haya yote inashauriwa kutumia kanuni ya hatua 10. Yaani, ikiwa unahisi huwezi kuongea kwa sauti ya kawaida, nenda umbali wa hatua kumi kutoka kwa watu wengine.

  1. Usiongee mambo binafsi au mambo ya siri kwa simu

 Faragha ni muhimu sana katika mawasiliano ya simu. Unapozungumza mambo yako binafsi au mambo ambayo ni siri, si vema kuongea mbele za watu. Usianike mambo yako binafsi kwa watu wasiohusika. Kama unataka kuongea mambo binafsi au ya siri, ni vizuri ukasubiri uko pekee yako au tumia kanuni ya hatua kumi.

Ni muhimu pia kuheshimu faragha ya wengine kama unavyotaka faragha yako iheshimiwe. Epuka kusikiliza simu ya mtu au kusoma ujumbe katika simu yake bila idhini yake au kusambaza habari za kibinafsi za mtu kwa simu bila ridhaa yake.

7. Epuka Kupiga Simu kwa Wakati Usiofaa

 Kupiga simu kwa watu wengine wakati ambao si sahihi kunaweza kusababisha usumbufu na kukera. Ni muhimu kuzingatia muda wa kupiga simu. Kwa mfano, usipige simu wakati wa usiku au asubuhi sana ambapo mtu anaweza kuwa amelala isipokuwa ikiwa ni muhimu sana au kuna dharura. Pia, kama unajua mtu ana shughuli muhimu, ni vyema kuepusha kupiga simu katika kipindi hicho.

8. Kuzima Simu Wakati wa Mikutano au Matukio Muhimu

 Ni busara kuzima simu au kuweka kwenye hali ya ukimya (silent mode) au mitetemo (vibration mode) wakati wa mikutano au matukio muhimu kama vile ibada. Kufanya hivyo kunahakikisha kwamba hautavuruga au kusumbua wengine na pia inaonyesha heshima kwa watu wengine wanaohudhuria matukio hayo. Hii itakuhakishia umakini wako na wa watu wengine katika kufuatilia kinachoendelea katika tukio husika.

Ukiacha mikutano na matukio muhimu, hata wakati unapokuwa katika mazungumzo muhimu na mtu, si ustaarabu kutumia simu yako. Ikitokea unataka kupiga simu, kupokea simu au kutuma ujumbe ni vizuri kumuomba radhi na ridhaa mtu unayeongea naye. Si ustaarabu kukatisha mazungumzo kwa kupokea simu, kupiga simu au kutuma ujumbe wa simu bila kumuomba unayeongea naye. Ukifanya hivyo, atachukulia kuwa hujali kabisa au umepuuza mazungumzo yenu.

Kwa kufuata kanuni hizi, tunaweza kukuza mahusiano mazuri na kufanya mawasiliano ya simu kuwa uzoefu wa kufurahisha na mzuri zaidi na tutaepuka kusababisha usumbufu kwa wengine au kuumiza hisia zao.

Endelea kufuatilia makala zaidi katika mtandao huu kwa ajili ya mafanikio yako katika nyanja mbalimbali za maisha.

Kama hujajiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini ili uweze kupokea makala kwenye barua pepe yako moja kwa moja.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

2 comments / Add your comment below

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *