Epuka Tabia Hizi Mbaya Unapokuwa Katika Mazungumzo – 3

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Karibu tena katika mwendelezo wa makala kuhusu tabia mbaya unazopaswa kuziepuka unapokuwa katika mazungumzo muhimu na mtu. Katika mfululizo wa makala haya, tunaangalia tabia ambazo zinaweza kuharibu mazungumzo yako na mtu au watu wengine. Katika makala yaliyopita tuliangalia tabia mbaya tano. Tabia ya kwanza ni matumizi ya simu wakati wa mazungumzo. Tabia ya pili ni kejeli, utani na ubishi na ya tatu ni kutokumtazama mtu unayeongea naye. Tabia ya nne ni kukosa utulivu na ya tano ni kuonesha kujua kila kitu .

Kusoma makala ya nyuma bonyeza hapa na hapa

Leo tutaangali tabia zingine tano. Tabia hizo ni kutoa ushauri ambao hujaombwa, kuhodhi mazungumzo, kutojali hisia za watu wengine na kuongelea mambo yanayokuhusu wewe tu.

Kutoa Ushauri ambao Haujaombwa

Iwe, kwa mfano, ni ushauri wa kimatibabu, ushauri kuhusu chuo kikuu kizuri, gari nzuri ya kununua au ushauri mwingine wowote kama hujaombwa kuutoa, usichukulie kwamba ushauri wako unahitajika. Isipokuwa kama anadokeza kwa maneno yake au vitendo vyake kuwa anahitaji ushauri wako, unapaswa kujizuia  kutoa ushauri kwa mtu unayeongea naye maana si kila mtu anayekueleza tatizo lake anahitaji ushauri. Wengine hueleza mambo yao au matatizo yao ili kuyatoa tu kifuani.

Mtu anaweza kukueleza tatizo ili tu umuonee huruma au umpatie usaidizi wa  kihisia (emotional support) na sio ushauri juu ya nini cha kufanya. Huenda sio lazima awe anatafuta ushauri wowote kwa sasa na kwa hivyo kutoa ushauri ambao haujaombwa kunaweza kukufanya uonekane kuwa mtu wa ajabu au unayeingilia mambo ya watu. Usiwe mtu wa kujishughulisha na mambo ya watu wengine bila uhitaji wao.

Kuhodhi Mazungumzo

Unapofikiria kuhodhi au ukiritimba, bila shaka kinachokuja akilini mwako kwa kawaida ni udhibiti kamili na kuzuia watu wengine kuwa na chochote cha kufanya ili kuleta matokeo katika jambo fulani. Wapo baadhi ya watu wenye tabia hiyo. Wanapenda kuwa na uhodhi au ukiritimba katika mazungumzo. Wao wanapenda waongee pekee yao na kuwafanya wengine kubaki wasikilizaji tu.

Kuhodhi mazungumzo kunaweza kuharibu uhusiano. Unapoendelea kuongea na kuongea na usimpe nafasi mzungumzaji kutoa hoja zao, unaua mazungumzo. Kumbuka kuwa na mazungumzo ni tofauti na kutoa hotuba. Uhodhi wa mazungumzo ni sifa ya kawaida ya watu wabinafsi na wanaojijali zaidi wao kuliko wengine.

Mazungumzo hayawezi kuwa mazungumzo kama ni ya upande mmoja. Yaani, mtu mmoja pekee yake ndo anaongea! Hiyo itakuwa hotuba na siyo mazungumzo. Mazungumzo maana yake  unazungumza na mtu mwingine anasikiliza na yeye anazungumza na wewe unasikiliza. Hiyo ndo maana halisi ya mazungumzo.

Kwa hivyo, si sahihi kumnyima mtu mwingine fursa ya kuongea mnapokuwa katika mazungumzo. Bila shaka sote tunataka kuwa na mvuto kwa watu, lakini lazima ukumbuke kwamba watu wanavutiwa na watu wanaowajali na kuwathamini. Kwa hivyo, tafadhali acha kufikiria kuwa kila kitu kinakuhusu na pia jitahidi kuonesha kuwa unawathamini watu unaoongea nao. Njia moja wapo ya kuwathamini  wengine ni kuwapa fursa ya kuongea mnapokuwa katika mazungumzo nao.

Kutojali Hisia za Watu Wengine

Ni vizuri kusema mambo jinsi yalivyo kwa uwazi na moja kwa moja lakini akili ya kihisia (emotional intteligence) inatutaka kwamba tuongee kwa akili na huruma. Kuzungumza bila huruma ni kuzungumza na mtu bila kufikiria jinsi maneno yako yanavyomfanya ahisi au ajihisi. Haijalishi uko karibu kiasi gani na mtu, huruma, busara na kuongea kwa upendo hufanya maajabu.

Ulimi una nguvu, kwa wema au ubaya. Maneno sahihi ni uponyaji kwa wakati ufaao. Kutokujali hisia za wengine ni tabia mbaya na unaweza kumuumiza mtu bila kukusudia. Unapozungumza na mtu, usiseme tu kila kitu kinachokuja kichwani mwako. Tafakari kabla ya kusema, jaribu kuona mapema athari ambayo maneno yako yanaweza kusababisha kwa mtu unayeongea naye na uzungumze kwa upole.  Hii itakusaidia kutambua watu wengine wanapokeaje unachokisema. Utaweza pia kujua kama kile unachokisema hakiwavutii au hawafurahii mazungumzo yenu. Ikiwa unaona kwamba hawajisikii vizuri kujadili mada fulani, badilisha mada mara moja au tengeneza mazingira waanzishe mada wanayoifurahia au waliyo huru nayo. Jitahidi usiharibu uhusiano wenu kwa sababu tu hujui kudhibiti ulimi mwako.

Kuongelea Mambo Yanayokuhusu Wewe tu

Ikiwa umewahi kuwa na mazungumzo na mtu mwenye majigambo, unaweza kuelewa kile ninachozungumzia hapa. Baadhi ya watu wana tabia hii mbaya ya kujizungumzia kila mara. Kila kitu ni kuhusu yeye tu. Ataongelea mafanikio yake, mke wake mzuri, namna watoto wake walivyo na akili darasani, nchi zote alizotembelea, namna anavyoendesha biashara yake na kadhalika.  Kwa kawaida watu wa aina hii huongelea mazuri yao tun a hawawezi kuongelea mambo yasiyo mazuri kuwahusu.

Kufanya mazungumzo kuhusu wewe na wewe peke yako ni kuudhi na kujiaibisha kwa watu wengine. Unapaswa kumjali pia mtu unayezungumza naye. Watu wengine pia wana uzoefu na wana mambo mazuri ambayo wangependa kukushirikisha. Hata kama wao ni wenye haya na ni watu wasiojua mambo mengi kama wewe, waonyeshe kuwa unawajali kwa kuwauliza maswali ili kuwafanya waongee. Kama vile unavyofurahi kueleza mambo yako, wao pia wangependa kukushirikisha uzoefu wao pia. Lakini kuzungumza juu yako peke yako hufanya mazungumzo kukosa mvuto.

Ushauri wangu ni kwamba, kama unataka kueleza mambo yako kwa watu, njia sahihi ni kuandika kitabu cha wasifu wako ili watu watakaovutiwa na wewe wasome badala ya kuwachosha kueleza mambo yako katika mazungumzo maana huna hakika kama kila mtu atavutiwa na maelezo yako kuhusu wewe.

Kwa leo tuishie hapa. Karibu katika mwendelezo wa makala ili tuendelee kuona tabia zingine zisizofaa katika mazungumzo..

Endelea kufuatilia makala zaidi katika mtandao huu kwa ajili ya mafanikio yako katika nyanja mbalimbali za maisha.

Kama hujajiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini ili uweze kupokea makala kwenye barua pepe yako moja kwa moja.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *