Epuka Tabia Hizi Mbaya Unapokuwa Katika Mazungumzo – 4

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Tumekuwa na mfululizo wa makala kuhusu tabia ambazo hazifai katika mawasiliano. Tayari tumeshaona tabia mbaya 11 hadi sasa. Karibu katika sehemu ya mwisho ya makala haya ambapo tunaenda kuangalia tabia zingine tano zisizofaa katika mawasiliano.

Kusoma makala ya nyuma bonyeza hapa

Katika makala ya leo tutaangalia tabia zifuatazo: kujaribu kumshinda mzungumzaji mwingine, kupuuza hoja za watu wengine, kuuliza maswali kuhusu mambo binafsi, Kunyamaza na kuacha mazungumzo kuwa ya upande mmoja na kuvaa vifaa masikioni. Karibu twende pamoja.

Kujaribu kumshinda mzungumzaji mwingine

Unapokuwa kwenye mazungumzo na mtu au watu, epuka kugeuza mazungumzo kuwa mashindano ya hoja ambapo wewe unataka kuonekana mshindi. Usiyafanye mazungumzo kuwa debate au mahakama.  Katika shule za msingi na sekondari huwa kuna mashindano ya hoja maarufu kama debate. Hapo watu huwa katika pande mbili zenye hoja kinzani na huwa wanashindanisha hoja hizo kwa lengo la kushinda.Sehemu nyingine ambapo watu kushindanisha hoja kwa lengo la kushinda ni mahakamani.

Kwa bahati mbaya, baadhi ya watu wanapokuwa katika mazungumzo, huongea kana kwamba wako kwenye debate au ni mawakili mahakamani. Kama hauko kwenye debate na wewe si wakili mahakamani, tafadhali epuka kugeuza mazungumzo ya kawaida yaonekane kama shindano.

Katika mazungumzo, epuka kishawishi cha kuwaonesha watu wengine kwamba uzoefu wao hauna chochote kwako. Kwa mfano, mtu anasimulia jinsi alivyokaribia kuachwa na ndege na kulazimika kuendesha gari kana kwamba yuko kwenye mashindano ya magari ili awahi ndege hiyo. Ili kumuonesha kuwa uzoefu wake haulingani na wako, unamwambia kuwa na wewe uliwahi kupitia uzoefu huo na ikabidi ndege itue kwa dharura ili kukuchukua mahali ulipokuwa. Ndio, najua mfano huu umetiwa chumvi lakini unapata kile ninachomaanisha.

Fikiria mfano mwingine, ambapo mtu anasimulia safari yake ya nje ya nchi na anaelezea habari za mji aliotembelea. Ili kumuonesha kuwa wewe ni zaidi yake, unaelezea kuwa na wewe uliwahi kutembelea mji huo na miji mingine minne ya nchi hiyo. Katika mazungumzo, hatupaswi kuoneshana ni nani anayefanya vizuri zaidi katika jambo fulani.

Kugeuza mazungumzo kuwa jukwaa la kukufanya uonekane bora zaidi kuliko wazungumzaji wengine kunakuonesha kama mtu anayejijali mwenyewe tu na mtu unayejiona kuwa hakuna mwingine anayekuzidi. Mara nyingi, mazungumzo ya aina hiyo huwa yemejaa uongo unaotengenezwa ili kuwavutia au kuwashinda wengine. Hicho ndicho nilichomaanisha kwenye mfano wa ndege kutua kwa dharura kumchukua mtu aliyechelewa ndege.

Hata kama ni kweli kwamba una uzoefu mzuri zaidi au ulifanya jambo vizuri zaidi kuliko watu unaoongea nao, si vizuri kuongea katika namna ambayo utawaonesha wengine kuwa uko juu yao katika mambo hayo. Unaweza kutaja uzoefu wako bila kuonesha kuwa uzoefu wa wengine si lolote wala chochote ukilinganisha na wa kwako.

Kupuuza hoja za watu wengine

Tabia hii haitofautiani sana na ile ya kujaribu kuwashinda wengine. Wapo baadhi ya watu ambao wanaamini  kuwa mara zote hoja zao ni za maana kuliko za wengine. Ni jambo la kipuuzi sana kupuuza hoja za mtu unayezungumza naye. Ni tabia mbaya sana kufanya hivyo, iwe unaitamka kwa uwazi au inadokezwa na lugha yako ya mwili,

Hakuna mtu anayependa maoni yake kutupiliwa mbali kama hayana umuhimu. Kwa hivyo, si vema kutumia maneno kama yafuatayo: “umeongea pumba tu”, “unachoongea hakina mashiko”, “unaongea vitu visivyo na uhusiano na hoja yetu”, “unaongea bila kufikiri” n.k. Badala yake, tafuta njia ya heshima zaidi ya kusema hili. Kwa mfano,  unaweza kusema: “nadhani inabidi uchunguze zaidi unachokisema kama kina ukweli”, :hebu tafuta taarifa zaidi kuhusu suala hili, naona kama kuna vitu haviko sawa”, “mimi nina mtazamo tofauti kidogo na wako”, “suala hili naliona kwa mtazamo mwingine” na kadhalika. Kwa njia hii, utatofautiana na mtu kwa namna inayoonesha heshima zaidi na kumlindia mtu utu wake na kuepusha  kumfanya ajisikie hajui kitu au amedharaulika.

Kuuliza maswali ya kuhusu mambo binafsi

Baadhi ya watu wana tabia ya kuuliza maswali ambayo yanayohusu mambo binafsi ya mtu. Hebu fikiria mtu anakuuliza mshahara  wako au wa mume/mke wako ni  kiasi gani na anatarajia utamjibu. Au mtu mwingine anakuuliza, kama mke wako alikuwa bikira wakati mnafunga ndoa. Mambo kama haya ni binafsi sana na si busara kutaka kuyajua isipokuwa tu kama mtu mwenyewe ataanzisha mada hiyo na kuamua kukueleza mambo hayo. Vinginevyo, unapaswa kujiepusha kuanzisha mada hizo au kuuliza maswali yatakayowapelekea kujadili mambo nyeti ya binafsi. Kuuliza maswali kama hayo kunaweza kumkasirisha mtu na kukuona kama umemkosea adabu bila kujali uko karibu kiasi gani na mtu huyo.

Mila na desturi za jamii zinaweza kukusaidia kujua mambo yapi ni ya faragha au binafsi na yapi siyo. Kwa mfano, katika baadhi ya jamii au nchi, kumuuliza mama mjamzito ana mimba ya miezi mingapi ni jambo lisilotarajiwa maana  inachukuliwa kuwa ni jambo binafsi na la faragha. Lakini katika jamii zingine, hilo siyo jambo la faragha. Hali kadhalika katika baadhi ya jamii katika nchi fulani, kuuliza umri au kipato cha mtu ni jambo la kawaida wakati katika jamii zingine ni jambo binafsi na la faragha. Hivyo ni muhimu sana unapoenda mahali ambapo hujui mila na desturi zao kuwa makini sana juu ya aina ya maswali unayouliza kuhusu mambo binafsi ya watu.

Kunyamaza na kuacha mazungumzo kuwa ya upande mmoja

Kuna baadhi ya watu hukaa kimya wakati wote wa maongezi na kutochangia chochote. Kumpuuza mzungumzaji mwingine na kumuacha azungumze bila wewe kujibu ni kukosa adabu. Hii inaweza kuchukuliwa kumaanisha kuwa hupendezwi na mazungumzo kwa hivyo hakuna haja ya kuyachangia. Ndiyo, kunyamaza ni muhimu wakati mwingine, lakini angalau lugha yako ya mwili inapaswa kuonyesha kuwa unajali kile mtu huyo anachokisema.

Kuvaa vifaa vya masikioni

Baadhi ya watu wana tabia ya kuvaa vifaa vya masikioni (earphones au head phones). Kwa vyovyote vile, hiki ni  kilele cha ufidhuli katika mazungumzo. Ikiwa hutaki kuwa na mazungumzo wakati huo, sema tu. Unawezaje kuziba masikio yako na kutarajia mtu mwingine unayezungumza naye aendelee na mazungumzo? Jambo ni hili, unaweza kusikia vizuri hata ukiwa na headphone masikioni mwako lakini lugha ya mwili unayoongea inasema sikusikii, nyamaza na uondoke zako. Sihitaji mazungumzo na wewe. Si vizuri na ni si ustaarabu kuwa na earphones masikioni unapozungumza na watu.

Huu ndo mwisho wa mfufulizo wa makala ndefu kuhusu tabia zisizofaa wakati wa mazungumzo. Kama tutaachana na tabia hizo, bila shaka tutakuwa na mazungumzo yenye tija kwa ajili ya kuboresha mahusiano yetu katika ndoa, familia, kazini na katika jamii kwa ujumla.

Endelea kufuatilia makala zaidi katika mtandao huu kwa ajili ya mafanikio yako katika nyanja mbalimbali za maisha.

Kama hujajiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini ili uweze kupokea makala kwenye barua pepe yako moja kwa moja.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

1 comment / Add your comment below

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *