Kila Siku Unauza Kitu Bila Kujua: Mara zote Fanya Kilicho Sahihi Unapouza

Rafiki yangu mpendwa,

Karibu tena kwenye somo lingine la utoaji wa huduma bora kwa wateja, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa masomo tuliyoyaanza wakati wa Wiki ya Huduma kwa Wateja iliyoadhimishwa duniani kote tarehe 7-13 Oktoba. Masomo haya ni mchango wangu katika  maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja. Naamini umeweza kupata maarifa muhimu yanayoweza kusaidia kuboresha biashara yako, kazi yako, na hata maisha yako binafsi. Kwa kufanya hivyo, utaweza kuimarisha mahusiano yako na wale wanaokuzunguka, wakiwemo wateja, wafanyakazi wenzako, na hata familia yako.

Hata kama Wiki ya Huduma kwa Wateja imepita, utoaji wa huduma bora ni jukumu endelevu. Hatuwezi kuhitimisha kwamba tumemaliza kujifunza au kuboresha huduma zetu kwa sababu ya wiki maalum; badala yake, tunapaswa kuendelea kufanya hivyo kila siku. Kwa hiyo, leo tutazungumzia kitu kingine muhimu sana ambacho kinapaswa kuzingatiwa katika biashara yako, kazi yako, na hata maisha yako binafsi. Kitu hicho ni maadili (values) ya kibiashara, kikazi na hata binafsi. Ni muhimu sana kama mfanyabiashara, mfanyakazi, au mtu wa kawaida kuwa na misingi unayoshikilia, mambo ambayo hutayavunja hata kama mazingira yatakushawishi kwa kiasi kikubwa. Hii ni sehemu ya maadili yako, na yatakusaidia kusimama imara huku wengine wakiwa wanapotea.

Kusoma makala ya nyuma bonyeza hapa

Yapo mambo mengi ambayo unaweza kujiwekea kama misingi ya maadili yako.Leo nitajadili mambo matatu kati ya mengi.Mambo hyao ni ubora, uadilifu an uaminifu.

Ubora katika Kazi Yako na Huduma

Ubora ni kufanya kazi kwa viwango vya juu zaidi, bila kujali kama unalipwa kidogo au kazi hiyo inachukuliwa kuwa ndogo. Mara nyingi tunakutana na watu wanaofanya kazi kwa kutojali ubora, pengine kwa sababu ya kutolipwa vizuri au kwa sababu ya kukosa hamasa. Hata hivyo, kufanya kazi kwa ubora kunakujenga wewe binafsi, kunakupatia sifa nzuri, na mwishowe hukuletea mafanikio makubwa.

Fikiria kuhusu fundi seremala ambaye anatengeneza fanicha. Anaweza kuchagua kutumia mbao za bei nafuu au kukwepa kutumia zana sahihi ili kumaliza kazi haraka. Matokeo yake, fanicha zake hazitadumu muda mrefu na wateja wake wataanza kumkimbia. Kinyume chake, fundi mwingine anaweza kuwekeza katika vifaa bora na kuchukua muda wake kuhakikisha kila kipande cha fanicha kinafanywa kwa ustadi wa hali ya juu. Licha ya kazi hiyo kuchukua muda zaidi, mwishowe fundi huyu atapata sifa nzuri, wateja watarudi tena, na biashara yake itaendelea kuimarika.

Hivyo basi, kutoa huduma yenye ubora unapaswa kuwa kipaumbele chako, iwe unafanya kazi kama fundi, mfanyakazi wa ofisini, au hata unauza bidhaa. Ubora unajenga jina lako, na unapokuwa na jina zuri, watu watakutegemea na utapata mafanikio makubwa zaidi.

Uadilifu katika Maamuzi

Uadilifu ni uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, hata pale ambapo hakuna anayekuona au unapokabiliwa na vishawishi. Ni vigumu kufanya uamuzi wa kimaadili wakati unakabiliwa na fursa ya kupata faida haraka kwa njia isiyo sahihi. Lakini kumbuka kwamba faida ya haraka inaweza kukupeleka kwenye anguko la haraka zaidi.

Hebu tuangalie mfano wa mfanyabiashara anayeshawishika kuuza bidhaa ambazo amejua kuwa ni za bandia au hazina ubora unaotakiwa. Anaweza kufikiria kuwa anapata faida ya haraka kwa kuuza bidhaa hizo kwa bei nafuu, lakini mwishowe wateja wake wataelewa ubovu wa bidhaa hizo na wataacha kufanya biashara naye. Hata hivyo, mfanyabiashara anayeamua kusimamia uadilifu, hata kama inamaanisha kupata faida ndogo kwa kuuza bidhaa bora, mwishowe atajijengea uaminifu na wateja wake, ambao watarudi tena na tena.

Uadilifu unatuhusu sote, si wafanyabiashara pekee. Katika maisha ya kila siku, kama mfanyakazi au mwanafamilia, unapaswa kufanya maamuzi yenye maadili. Kwa mfano, unaweza kukutana na fursa ya kuchukua pesa za ofisi bila mtu kujua. Lakini kufanya hivyo kunaharibu uaminifu na, mara nyingi, matokeo yake ni anguko la heshima yako binafsi.

Biblia inatufundisha katika Luka Luka 16:10 kuwa “Aliye mwaminifu katika lililo dogo huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo huwa dhalimu katika lililo kubwa pia.” Fungu hili linafundisha kuwa uadilifu katika mambo madogo hujenga msingi wa uadilifu katika mambo makubwa.Hivyo aytupasa kuwa waadilifu katika mambo yote tukianzia na madogo.

Uaminifu

Uaminifu ni miongoni mwa nguzo za msingi katika biashara na mahusiano ya kijamii. Ikiwa wateja wako hawawezi kukuamini, hawatarudi tena. Ikiwa wafanyakazi wenzako hawawezi kukuamini, itakuwa vigumu kwao kushirikiana na wewe. Uaminifu ni nguzo ambayo inakuwezesha kuwa na mahusiano thabiti na endelevu katika kazi, biashara, na maisha yako binafsi.

Fikiria kuhusu mjasiriamali ambaye amejijengea sifa nzuri kutokana na uaminifu wake. Anapokosa bidhaa au huduma kwa muda, wateja wake hawatahangaika kutafuta mbadala kwa sababu wanajua atarudi na kuwa hudumia kwa usahihi. Hata kama kuna matatizo madogo ya muda, uaminifu wa mjasiriamali huyu unamuweka salama mbele ya wateja wake.

Kwa upande mwingine, mtu asiye mwaminifu anaweza kupata faida ya haraka, lakini mwishowe, ataanguka kwa sababu wateja hawataendelea kumwamini. Ubinafsi, ukosefu wa uaminifu, na kutojali maadili vinavyomfanya mtu asifikirie matokeo ya vitendo vyake havina nafasi katika biashara au mahusiano ya muda mrefu.

Ellen G. White (1827-1915)  aliyekuwa mwandishi na kiongozi wa kiroho aliwahi kuandika katika kitabu chake cha The Great Controversy, pg. 460 kuwa “Do right because it is right, and leave the consequences with God. Nukuu hii inasisitiza kwamba tunapaswa kufanya yaliyo sahihi, hata kama hatujui matokeo yake, kwa kuwa matokeo yapo mikononi mwa Mungu.

Uadilifu

Ni rahisi kutafuta njia za mkato ili kufanikiwa haraka, lakini mafanikio ya haraka mara nyingi yanakosa misingi thabiti. Mfano mwingine tunaweza kuangalia ni wa mfanyakazi ambaye anajitahidi kuwajibika hata pale ambapo mwajiri wake hayupo. Kama unafanya kazi za ofisi na unapata nafasi ya kucheza na muda au kufanya kazi nusu nusu kwa sababu hakuna anayekuangalia, unatakiwa ujiulize kama hilo ni jambo sahihi. Mtu mwenye uadilifu ataendelea kufanya kazi kwa bidii, hata kama hakuna anayemsimamia moja kwa moja.

Mfano huu ni wa kawaida kwa watu waliofanikiwa kimaisha: mafanikio yao hayaji kwa bahati mbaya, bali ni matokeo ya kujitoa kwao kufanya kazi kwa viwango vya juu bila kuficha wala kupunguza ubora wa huduma zao.

Kwa kumalizia, ni wazi kwamba ili kufanikiwa katika biashara, kazi, na maisha binafsi, ni lazima kuzingatia maadili ya ubora, uadilifu, na uaminifu. Haya si mambo ya kuchagua kufuata wakati mwingine na kupuuza wakati mwingine; ni misingi inayopaswa kuongoza maamuzi yako kila siku. “Kama mtu anajua kufanya mema lakini hayafanyi, huo ni dhambi” (Yakobo 4:17). Sauti ya ndani ambayo inakuambia kipi ni sahihi na kipi si sahihi ni mwongozo wako wa kila siku.

Kwa hiyo, katika kila jambo unalofanya, hakikisha unazingatia maadili haya. Ubora utajenga jina lako, uadilifu utakuweka kwenye njia sahihi, na uaminifu utajenga mahusiano thabiti ya muda mrefu. Mwishowe, utafanikiwa kwa njia endelevu na ya heshima.

Kumbuka: Mara zote fanya kilicho sahihi, hata kama hakuna anayekuona.

Endelea kufuatilia mfululizo huu wa makala za huduma bora kwa wateja kupitia blogu yetu. Ili usipitwe na makala yoyote mpya, jiunge nasi kwa kujaza fomu iliyo hapa chini, na makala mpya zitakufikia moja kwa moja kwenye barua pepe yako.

Leave a Comment