Hizi Ndizo Kanuni Za Kufanya Biashara Kwa Mkristo

Ndugu yangu mpendwa katika Kristo,

Hakuna ubishi kwamba biashara ni njia mojawapo ya uhakika ya kujipatia kipato kisicho na kikomo. Hivyo, ni vema kila mmoja anayetamani kufanikiwa kifedha awe na biashara hata kama na vyanzo vingine vya kipato. Kama utaamua kufanya biashara, yakupasa ujue kuwa biashara ina kanuni zake. Zipo kanuni za jumla ambazo mfanyabiashara yeyote anayetaka kufanikiwa ni lazima azifuate. Lakini pia, zipo kanuni maalum kwa ajili ya wafanyabiashara Wakristo. Je ni zipi hizo?

Mungu kwanza ndiyo kanuni muhimu kwa Mkristo inayotakiwa kumwongoza katika shughuli zake zote ikiwa pamoja na shughuli za biashara. Kanuni hii inamaanisha kumfanya Mungu wa kwanza katika kila jambo na aliitoa Yesu mwenyewe aliposema “Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa ‘ (Mathayo 6:31-33).

Kwa kifupi, kanuni hii inabeba mambo mengi ambayo mfanyabiashara aliyemfanya Mungu kuwa wa kwanza anapaswa kuyafanya. Mambo hayo ni kama ifuatavyo:

Kufanya biashara inayokubalika kwa Mungu na kwa serikali

Tunapofanya biashara, tunatafuta mahitaji yetu muhimu yaani chakula, mavazi, malazi na kadhalika. Hata hivyo, haya hayapaswi kuwa kipaumbele. Kipaumbele cha Mkristo anapofanya biashara ni kupata ufalme wa Mungu kwanza na hayo yote (mahitaji yake) yanafuata baadaye.  Hivyo, ikitokea mazingira ambapo inabidi ufanye kitu ambacho kimekatazwa na Mungu ili kufanikiwa katika biashara, Mkristo uliyemfanya Mungu kuwa wa kwanza hupaswi kukubali. Ni heri upoteze biashara yako kuliko kupoteza ufalme wa Mungu.

 Biblia inaelekeza “Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu (1Wakorintho 10:31). Bila shaka neno lolote inahusisha pia biashara.  Unapochagua biashara ya kufanya, chagua ile inayokubalika mbele za Mungu na mbele ya jamii au serikali. 

Zipo biashara ambazo zinaleta utukufu kwa Mungu lakini pia kuna biashara ambazo hazileti utukufu kwa Mungu. Biashara haramu kama vile uuzaji wa dawa za kulevya, ukahaba, vinywaji haramu kama vile pombe aina ya gongo ni biashara ambazo hazikubaliki kwa Mungu na kwa serikali pia.

Lakini zipo biashara zinazokubalika katika jamii na kwa serikali lakini kwa Mungu hazikubaliki. Kwa mfano, michezo ya kubahatisha kama vile bahati nasibu ya taifa, kubashiri matokeo ya mechi za mpira, maarufu kama betting,biashara ya baadshi ya dawa za kulevya kama vile bangi na milungi katika baadhi ya nchina biashara zingine zinakubalika katika jamii lakini bidhaa hizi hazifai hazikubaliki mbele za Mungu na hivyo biashara hizi hazifai kwa mkristo. Biashara hizi zinaweza kuonekana kuwa zinalipa na zinaweza kukupatia uhuru wa fedha lakini hii haiwezi kuwa sababu kwa wewe mkristo kujihusisha na biashara hizo.

Kuepuka mapato ya udhalimu

 Siku hizi uaminifu unapatikana kwa shida sana au haupo kabisa katika ulimwengu wa biashara wa leo. Wafanyabiashara wengi hutumia njia zisizo halali na zisizo za haki ili kuongeza mapato yao kama vile kudanganya katika matangazo yao ya biashara, kupandisha bei kiholela kunapotokea  uhaba wa bidhaa fulani, kutengeneza bidhaa zisizo na ubora, kuuza bidhaa zilizoisha muda wa matumizi na kadhalika. 

Mkristo hapaswi kufanya udanganyifu wa aina yoyote katika biashara yake. Anapaswa kuwa mwaminifu na mkweli wakati wote na daima ataongozwa na kanuni za Biblia, kama vile: “Hatukumdhulumu mtu ye yote, wala kumharibu mtu, wala kumkaramkia mtu”; “tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila”; “vipimo mbalimbali ni chukizo kwa BWANA; tena mizani ya hila si njema”? (2 Wakorintho 4:2; 7:2; Mithali 20:23).

Ipo dhana kwa baadhi ya watu kuwa ni vigumu kufanikiwa katika biashara mpaka mtu atumie njia zisizo za haki kama wengine wanavyofanya. Hapa ndipo mkristo anaweza kuonyesha imani yake kwa Mungu na kuthibitisha uongo wa dhana hii. Kusema kwamba mtu hawezi kufanikiwa katika biashara bila kutumia njia zisizo halali ni sawa na kusema kuwa Mungu hajali wale wanaompenda.

Ukweli ni kwamba Mungu ameahidi kuwafanikisha wote wanaoenenda sawa sawa na maagizo yake (Kumbukumbu la Torati 11:13-14, 28:1-14). Ni bora kuridhika na kipato kidogo unachokipata kwa kufanya biashara kwa uaminifu kuliko kipato kikubwa unachokipata kwa udhalimu kwa maana imeandikwa “Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?” (Marko 8:36).

Ikumbukwe kuwa njia ya mwongo ni fupi. Kama utafanya biashara kwa udhalimu, huwezi kufanya hivyo muda wote. Unaweza kupata faida mwanzoni lakini baadaye wateja wakigundua udhalimu wako watakukimbia. Usidhani kuwa kwa kuwa watu wengi wanafanya udhalimu basi uko salama. 

Kanuni ya Biblia ni hii: “Usiandamane na mkutano kutenda uovu” (Kutoka 23:2). Hivyo, usifuate wengi wanafanyaje, bali fuata kile ambacho ni chema mbele za Mungu bila kujali kama kwa kufanya hivyo utapata kipato kidogo.

Kumpa Mungu kilicho chake na Kaisari kilicho chake

Imeandikwa “Yesu akajibu, akawaambia, Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya Mungu mpeni Mungu. Wakamstaajabia sana” (Marko 12:17). Unapopata kipato kutoka kwenye biashara, kumbuka kumpatia Mungu kilicho chake na Kaisari pia.

Kilicho cha Mungu ni zaka na sadaka na cha Kaisari ni kodi. Kwa hiyo kabla hujatumia au kuweka akiba kipato kutoka kwenye biashara yako, kumbuka kutoa zaka na sadaka na pia toa kodi zote za serikali kwa uaminifu. Hili ni agizo la Mungu na wala siyo hiari yako.  

Haya ndiyo baadhi ya mambo ambayo Mkristo anapaswa kuyazingatia katika shughuli zake za kibiashara na shughuli zingine.

Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu biashara na mafanikio kwa ujumla ? Basi tafuta kitabu chetu kinachoitwa Siri za Mafanikio ya kifedha kwa Mkristo :Elimu isiyofundishwa Shuleni. Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *