Kwa utaratibu wa Biblia, si kila mhitaji lazima asaidiwe

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Ni wajibu wa wakrisito kuwasaidia wahitaji katika jamii. Hivyo, zaidi ya kutoa zaka na sadaka kanisani, wakristo yawapasa kutenga kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji. Suala hili ni la kibiblia maana ziaidi ya kusisitizwa katika maadniko, ipo mifano mingi katika maandiko ya watu waliotoa misaada kwa wahitaji.

Mtume Paulo aliwahimiza Waefeso kufanya kazi kwa faida yao na ya wengine (Waefeso 4:28). Licha ya kuhimiza wengine, Paulo alifanya kazi kwa bidii kwa faida yake binafsi na ya wengine. Hii inadhihirika katika hotuba yake kwa wazee wa Efeso kabla ya kusafiri kwenda Mileto ambapo alisema “Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami”(Matendo 20:33, 34).

Mafundisho ya Paulo kwa maneno na vitendo yanaendana na mafundisho ya Yohana mbatizaji ambaye anashauri kwamba matunda ya kazi zetu yawasaidie watu wanaotuzunguka “Akawajibu akiwaambia, Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo” (Luka 3:11).

Pamoja na umuhimu wa kuwasaidia wengine ni dhahiri kwamba ili tuweze kuwasaidia wengine, ni lazima tuwe na kitu cha kuwasaidia. Tunapataje kitu cha kuwasaidia wengine? Ni kwa kufanya kazi. Hapa suala si kufanya kazi tu, bali kufanya kazi kwa bidii ili kupata vitu vya kututosha sisi na kuwasaidia wengine. Kama sisi wenyewe ni wahitaji, tutawezaje kuwasaidia wengine. Mkristo asiyefanya kazi, hana faida kwa familia yake na jamii inayomzunguka kwani hana kitu cha kuwasaidia. 

Ukisoma katika Luka 7:2-4, kuna kisa cha akida mmoja ambaye hakuwa Myahudi lakini alionekana wa maana katika jamii kiasi cha wazee wa kiyahudi kwenda kwa Yesu kumuomba aje amponye mtumwa wa huyo akida. Huyu akida alikubalika kutokana na huduma yake ya kuijali jamii kwani aliwajengea sinagogi. Je, wewe ni mmoja wa wakristo ambao kuwepo na kutokuwepo kwao hakuna tofauti katika familia na jamii yake? Je, familia yako na jamii yako wanafaidikaje na kazi yako?

Katika Matendo 9:36-41, tunakutana na kisa cha Dorkasi. Huyu ni mwanamke aliyekuwa msaada sana katika jamii yake kiasi kwamba jamii ilishindwa kujizuia mara baada ya kufariki kwake.  Biblia inaeleza kuwa watu walitumwa kwenda kwa Petro ili aje afanye huduma ya kurudisha uhai wa Dorkasi, yaani amfufue. Kazi ya Dorkasi ilikuwa yenye msaada kiasi cha jamii kuona hastahili kufa. Dorkasi alifanya kazi ya ushonaji nguo, ambazo zilimfanya awe na kitu cha kuisadia jamii yake.  Licha ya kuwasaidia wajane, alitoa sadaka pia kanisani.  Hebu kila mmoja wetu ajiulize, hivi nikifa leo, na kuwe na uwezekano wa kufufuliwa lakini kwa sharti kwamba jamii iridhie kufufuliwa kwangu, je, jamii itaridhia nifufuliwe? Mwenzi wangu  na familia yangu je, wataridhia?

Pamoja na kwamba ni wajibu wetu kuwasaidia wahitaji, lakini kuna watu ambao ni wahitaji kwa sababu tu hawataki kufanya kazi. Wapo watu wenye uwezo wa kufanya kazi lakini hawataki kufanya kazi au wanafanya kazi kwa uvivu na hivyo wanaishia kuwa wahitaji. Wapo wengine, hasa vijana waliobahatika kusoma, wanasubiri kupata kazi ya kuajiriwa tu na kwa kuwa siku hizi kuna tatizo la ajaira, vijana hao wamebaki kuwa wahitaji wakati wangeweza kufanya kazi za mikono wakajipatia kipato.

Watu wote ambao wana uwezo wa kufanya kazi lakini, kwa sababu yoyote ile, hawafanyi kazi, hatuwajibiki kuwapatia mahitaji yao badala yake tunawajibika kuwasaidia wafanye kazi. Utaratibu wa kibiblia wa kuwasaidia wahitaji, unawataka wahitaji wafanye kazi pale inapowezekana. Hakuna nafasi kwa uvivu katika maisha ya mkristo.

Katika agano la kale, Mungu alitoa maelekezo ya namna ya kuwasaidia wahitaji kupitia kufanya kazi: “Nanyi hapo mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa kabisa pembe za shamba lako, wala msiyakusanye masazo ya mavuno yako; utayaacha kwa ajili ya huyo maskini, na mgeni; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu” (Mambo ya Walawi 23:22). Maelekezo haya yanathibitisha juu ya umuhimu wa wahitaji kupata msaada kwa kufanya kazi. Hapa, Mungu hasemi kwamba wavune kila kitu na kisha wawagawie wahitaji bali Mungu anaelekeza kwamba wanapovuna waache sehemu fulani ya mavuno ili wahitaji waje wavune wenyewe. Katika utaratibu huu, hakukuwa na cha bure.

Kwa upande wake, mtume Paulo anaonya vikali juu ya watu wasiopenda kufanya kazi na anatoa maelekezo ya namna ya kushughulika nao: “Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula. Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine. Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe” (2 Wathesalonike 3:10-12).

Kwa maelkezo haya machache kutoka katika Biblia, ni dhahiri kuwa si utaratibu wa Mungu mtu apate mahitaji yake bila kufanya kazi ikiwa uwezo wa kufanya kazi anao. Kwa wale, ambao kwa sababu moja ama nyingine hawna uwezo wa kufanya kazi , hao tunaweza kusaidia bila wao kufanya kazi. Kwa sababu hivyo, tusivunje utaratibu wa Mungu kwa kutoa misaada kwa watu wasiotaka kufanya kazi. Hata kama ni watoto wetu, tusikubali wale chakula bila kufanya kazi. Tuwape majukumu ya kufanya ili apate haki ya kula chakula. 

Hivyo, kwa neema yake, Mungu atuwezeshe kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya mahitaji yetu na ya wale wasioweza kufanya kazi huku tukiwasaidia kufanya kazi wahitaji wenye uwezo wa kufanya kazi.

Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu masuala ya fedha na mafanikio?

Basi jipatie kitabu chetu kinachoitwa Siri za Mafanikio ya kifedha kwa Mkristo: Elimu isiyofundishwa Shuleni. Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

Je, unataka kupata mafunzo endelevu kuhusu mafaniko kwa mkristo?

Kama unataka kuendelea kujifunza kuhusu masuala mbalimbali juu ya mafanikio kwa mkristo unaweza kujiunga na mtandao huu ili uweze kupata makala mbalimbali. Kwa kufanya hivyo, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa katika mtandao huu.

Ili kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *