Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Msemo “kula bata” umekuwa maarufu sana katika siku za hivi karibuni ukiwa unatumiwa zaidi na vijana. Msemo huu unatumika kumaanisha kufurahia maisha. Japo kila mtu anatafsiri yake kuhusu kufurahia maisha, mara nyingi “kula bata” ni kufurahisha maisha kunakohusisha kutumia pesa katika mambo mbalimbali kama vile burudani, kula na kunywa vitu vizuri, matembezi katika maeneo maalum kama vile ufukweni, mbuga za wanyama na kadhalika. Kwa ujumla, kula bata ni shughuli inayofanyika wakati wa mapumziko baada ya mtu kufanya kazi ili kufurahia matunda ya jasho la mtu na kumrejeshea mtu utulivu wa akili na nguvu zaidi za kuendelea kuchapa kazi. Kwa kifupi, kula bata ni mapumziko yenye furaha.
Je, “kula bata” ni vibaya?
Hakuna ubaya wowote katika “kula bata” ili mradi tu kufanya hivyo hakukiuki Sheria za Mungu na za nchi na pia unazingatia nidhamu ya matumizi ya fedha na raslimali zingine. Huenda hufahamu lakini Mungu mwenyewe ndiye mwanzilishi wa “kula bata” na hakutuacha gizani kuhusu namna gani tunaweza “kula bata”. Katika Amri kumi za Mungu, amri ya nne inawaagiza wanadamu wote “kula bata”. Amri hiyo inasema “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa (Kutoka 20:8-11). Kwa kuwaelekeza wanadamu kutofanya kazi siku ya Saba maana yeke aliwaambia “wale bata” siku hiyo.
Kuna tatizo gani “nisipo kula bata”?
“Kula bata” ni muhimu tangu kuumbwa kwa ulimwengu na imekuwa muhimu zaidi katika dunia ya leo, ambapo hali ya maisha inazidi kuwa ngumu kila siku na watu wengi wanalazimika kufanya kazi kupita kiasi ili kupata mafanikio kifedha kiasi kwamba wana hatarisha ndoa, familia na hata afya zao. Wakati mwingine, kwa sababu ya kazi wanasahau hata kumpa Mungu muda wa kutosha. Pamoja na umuhimu wa kufanya kazi ambao tumekwisha ufafanua, lakini sisi kama wakristo, hatupaswi kufuata upepo wa dunia hii wa kukimbizana na maisha kiasi cha kusahau mpango wa Mungu wa kuwa na kiasi katika kila jambo kama Warumi 12: 2 inavyosema “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu”.
Tusipoangalia kazi zetu zinaweza kutuletea madhara sisi wenyewe na familia zetu badala ya kulutea manufaa yaliyokusudiwa na Mungu. Tunaweza kujidanganya kwamba tunafanya kazi kupita kiasi kwa manufaa ya familia zetu lakini kumbe tunafanya hivyo kwa hasara ya familia zetu. Mama Theresa, mtawa na mmisionari wa kanisa Katoliki aliyekuwa anafanya kazi nchini India aliwahi kusema kuwa “Nadhani ulimwengu umegeuka kichwa chini-miguu juu na unahangaika sana kwa sababu kuna upendo kidogo nyumbani na katika maisha ya familia. Hatuna muda kwa ajili ya watoto wetu, hatuna muda kwa ajili ya wenzi wetu wa ndoa. Hakuna muda wa kufurahiana”. Ujumbe huu una ukweli kwa kiasi gani kwako leo? Tafakari.
Kila kiumbe kinahitaji pumziko ili kurudisha nguvu zilizotumika. Miili yetu imeumbwa kwa namna ya ajabu kiasi kwamba huwa inatuashiria ni wakati gani tunapaswa kupumzika. Hata hivyo, kwa sababu mbalimbali mara nyingi huwa tunapuuzia ishara tunazopewa na miili yetu. Kwa mfano, unaposikia usingizi ni ishara kwamba unahitaji kupumzika kwa kusinzia. Ni mara nyingi tu tumesikia watu wamepata maradhi kwa sababu ya kutopumzika na hivyo kulazimika kulala kitandani kwa muda mrefu na kupoteza muda wa kufanya kazi kwa sababu tu ya kupuuzia ishara za asili zitolewazo na miili yetu! Mungu alituwekea muda wa pumziko la kila siku na pumziko la siku moja kwa juma.
Mungu alisema “tule bata” kwa muda gani na kwa naman gani?
Ukisoma Mwanzo 1, utakutana na maneno “ikawa jioni ikawa asubuhi”. Maneno haya huashiria mgawanyiko wa siku kati ya usiku na mchana. Mungu aliandaa utaratibu wa kupumzika ambapo aliweka mchana kwa ajili ya kufanya kazi na usiku kwa ajili ya kupumzika ili kuruhusu kufanyika kwa mchakato wa kuurudishia mwili nguvu zake. Mwili wa mwanadamu unahitaji pumziko la kila siku. Pumziko la kila siku linahusisha kupata usingizi wa kutosha. Kabla ya kuvumbuliwa kwa teknolojia ya umeme, watu walifanya kazi wakati wa mchana tu na kulala wakati wa usiku. Huu ndio ulikuwa mpango wa asili wa Mungu. Lakini baada ya kuvumbuliwa kwa teknolojia ya nishati ya umeme, mpango wa Mungu haufuatwi tena. Sasa watu wanafanya kazi usiku na mchana. Lakini, sisi kama wakristo, lazima tuwe makini katika kuzingatia mpango wa asili wa Mungu. Hata kama tutaamua kufanya kazi usiku, kulingana na aina ya kazi tunazofanya, ni lazima tuhakikishe kuwa tunapata usingizi wa kutosha baada ya kazi.
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa kuna madhara makubwa yatokanayo na mtu kutolala vya kutosha. Madhara hayo yanahusisha uwezekano mkubwa wa kupata kisukari, unene uliokithiri (obesity), ufaulu duni katika masomo, matatizo ya akili na ajali za barabarani zinazosababisha majeraha, ulemavu na vifo. Wataalam wa afya wanashauri kuwa mtu mzima apate usingizi kwa muda usiopungua saa nane kwa siku. Kwa upande wa watoto, inashauriwa kuwa wapate usingizi kwa muda mrefu zaidi kutegemeana na umri wa mtoto. Madhara ya kukosa usingizi katika mwili yanalinganishwa na madhara ya pombe. Jiulize, unafanya mambo gani yanayopelekea kukosa usingizi wa kutosha hasa usiku? Mambo hayo yana umuhimu au faida gani kiroho au kiuchumi ?
Zaidi ya kuwa na pumziko la kila siku, Mungu katika Mwanzo 2:1-2 na Kutoka 20:8-11 anatoa maelekezo ya kupumzika siku moja kwa juma. Mungu mwenyewe alipumzika siku ya moja baada ya kumaliza kazi ya uumbaji na hivyo akaonesha kwa vitendo umuhimu wa kupumzika. Kwa hiyo, Mungu alituagiza kufanya kitu ambacho yeye mwenyewe alikifanya. Hata hivyo, ni lazima tufahamu kuwa pumziko la siku ya saba ni kwa faida yetu, na siyo kwa faida ya Mungu.
Mungu anatuagiza tuikumbuke siku ya saba na kuitukuza. Kuitakasa siku ya saba, ambayo inatajwa kama Sabato katika Biblia (Kutoka 20:8) ni kuitumia kwa kusudi lile lile iliyowekewa. Siku ya Sabato ilikusudiwa kuwa siku ya ibada kwa wanadamu wote pamoja na maombi ya faragha. “Siku ya saba ni sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu” (Mambo ya Walawi 23 :3). Yesu mwenyewe ni kielelezo cha utunzaji wa Sabato maana ilikuwa ni desturi yake kufanya hivyo. “Na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi Yake” (Luka 4 : l6). Maandalio ya kuitunza vizuri Sabato ni kuandaa vitu vyote vinavyoweza kuhitajika ili kuwa tayari kuacha kufanya kazi za kawaida, za kidunia wakati Sabato inapoanza, na kuutumia muda wetu kwa mambo matakatifu, ya mbinguni (Kutoka l6:22-23; Luka 23:54). Sabato siyo siku ya kufanya kazi za kawaida, wala uzembe, wala burudani. Ni kwa ajili ya kupumzika, kiroho na kimwili ; kwa ajili ya kutafakari ; ibada ya faragha na ya wote ; kwa ajili ya furaha takatifu, na kwa kusaidiana. Siku hii Ilikusudiwa kuwa siku ya furaha, uchangamfu, na bora kuliko zote katika zile siku saba.
Pamoja na faida za kiroho za pumziko la Sabato, kuna faida za kimwili pia. Pumziko la Sabato linatufanya tuachane na mahangaiko, misongo na uchovu wa siku sita. Sabato ni njia ya Mungu ya kutufanya tupate nguvu mpya ya mwili na akili kwa ajili ya wiki nyingine. Hata hivyo, siku ya Sabato si siku ya kukaa bure. Ni siku ya ibada ; hivyo ni siku ya kuimarisha mahusiano yetu na Mungu. Kwa hiyo, tunapaswa kuitumia vizuri siku hii kwa ajili ya kukua kiroho sis binafsi pamoja na watu wengine.
Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mpango wa Mungu kuhusu mafanikio yako? Basi jiunge na mtandao wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio kwa kubonyeza hapa. Mtandao huu umeanzishwa kwa kusudi la kuwapatia maarifa ya msingi kuhusu masuala ya fedha, biashara, mahusiano (uchumba, ndoa na malezi ya watoto) na mambo ya kiroho. Katika mtandao huu utapata maarifa katika maeneo ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano, malezi ya watoto na mambo ya kiroho.
1 comment / Add your comment below