Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Kabla Bwana wetu Yesu Kristo hajapaa kwenda mbinguni, alitupatia wajibu muhimu unaohusiana na kuwaandaa watu kwa ajili ya ufalme aliokuwa anaenda kutuandalia. Wajibu huo ni kuhubiri habari njema za wokovu kutoka kwa Mungu, yaani Injili na vilevile kuwafundisha watu kuyashika maelekezo yote ya Mungu.
Agizo la Yesu kuhusu wajibu huu tunalipata katika vitabu vya injili. “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe’’(Marko 16:15). “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari” (Mathayo 28:19,20).
Kwa kuwa hili ni agizo au amri, hatuna budi kulitekeleza kama kweli sisi tunampenda Mungu maana Yesu mwenyewe alinasema “ Mkinipenda mtazishika Amri zangu. Hata hiyo, kabla ya kuanza kutekeleza agizo hili, yatupasa kulielewa vizuri maana pasipo kulielewa vizuri agizo hili hatutaweza kufanya kile tunachopaswa kufanya.
Hivyo, katika makala ya leo tutaangalia kwa kifupi maneno haya, kuhubiri na kufundisha, yana maanisha nini. Je, yana maanisha kitu kile kile au yana tofauti?
Je, unajua tofauti kati ya kuhubiri na kufundisha?
Mara nyingi, maneno kuhubiri na kufundisha hutumiwa na watu kwa kuchanganywa. Mtu anaweza kuwa anamaanisha kufundisha lakini akatumia neno kuhubiri au akatumia neno kuhubiri wakati anamaanisha kufundisha.
Ukweli ni kwamba maneno kuhubiri na kufundisha yana maana tofauti japo kwa namna fulani yanakaribiana na kuingilina sana katika maana na matumizi.
Katika Biblia, neno kuhubiri linatokana na neno la Kiyunani kerusso ambalo kwa lugha ya Kiingereza ni herald ambalo kwa Kiswahili maana yake ni tangaza, ashiria, piga mbiu. Neno kerusso lilitumika kumaanisha mtu aliyekuwa anatangaza habari muhimu kwa watu hasa kutoka kwa mfalme au mtu mwingine mwenye mamlaka ya utawala katika jamii.
Kwa upande mwingine, neno kufundisha, kama linavyotumika katika Biblia, linatokana na neno la Kiyunani didasko ambalo limetafsiriwa kama teacher kwa Kiingereza na kwa Kiswahili linamaanisha mwalimu. Didasko lilimaanisha mtu aliyekuwa anaelezea au kufundisha kitu fulani kwa watu fulani ili wakielewe.
Kutokana na maana ya neno la asili hapo juu, kuhubiri kama linavyotumika leo, linaamaaniha kutangaza habari njema (injili) kwa watu. Habari hizi ni kutoka kwa Mungu ambaye ni mfalme wa wafalme. Kwa upande mwingine, kufundisha ni kuelezea mambo mbalimbali kuhusiana na habari njema (injili) kwa watu na kuwaelekeza namna ya kuishi kwa kufuata maelekezo ya habari hizo.
Naomba nitumie kielelezo cha tangazo kutoka kwa Rais wa nchi kufafanua tofauti kati ya kuhubiri na kufundisha. Tangazo nitakalotumia ni msamaha kwa wafungwa walioko magerezani.
Fikiria Mkuu wa Gereza fulani hapa nchini, anatokea mbele ya wafungwa kutangaza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa kadhaa kwa kutumia mamlaka aliyo nayo kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.
Pale Mkuu wa Gereza anapotoa tangazo hilo ambalo ni habari njema, anafananishwa na mtu anayehubiri. Anakuwa anatangaza kile kilichotokea ambacho kitabadilisha hali ya mambo kwa wafungwa.
Ikiwa tangazo hilo litawafikia wafungwa na wakaanza kuuliza maswali na Mkuu huyo wa Gereza akaanza kufafanua na kuyajibu maswali hayo ili kuwasaidia kuelewa tangazo hilo ili waweze kulitekeleza atafananishwa na mtu anayefundisha. Hapa ujumbe ni ule ule ila tofauti ni namna unavyowasilishwa.
Kuhubiri na kufundisha kuna fananaje?
Pamoja na tofauti zilizopo kati ya kuhubiri na kufundisha, matumzi ya maneno haya yanaingiliana. Mahubiri hujenga msingi kwa ajili ya mafundisho. Lengo la mahubiri ni kuongoa (kubadilisha maisha ya watu), wakati lengo la mafundisho ni kukuza imani, dhamiri na tabia.
Wakati mwingine, kuhubiri na kufundisha huenda pamoja. Unapohubiri, unaweza ukawa unafundisha pia na unapofundisha unaweza ukawa unahubiri pia. Hata katika Biblia, maneno kuhubiri na kufundisha yanaenda pamoja katika baadhi ya mafungu bila kuweka wazi tofauti baina yake. Mifano ya mafungu hayo ni Matendo 5:42; 15:35; 28:31, Wakolosai 1: 28 na 1 Timotheo 2:7; 5:17.
Mfano mwingine ni katika tamko la Yesu la utume alilolitoa kwa wanafunzi wake. Mathayo anazungumzia tamko hili kama kufundisha (Mathayo 28:18, 19) na Marko anasema ni kuhubiri (Marko 16:15).
Vilevile, Biblia inamwelezea Yesu kama mhubiri na mwalimu na wakati mwingine mafungu tofauti ya Biblia yatumia neno kufundisha wakati mafungu mengine yanatumia neno kuhubiri kuelezea tukio lile lile. Kwa mfano, wakati Mathayo 4:23 anaeleza kuwa Yesu alikuwa anafundisha katika masinagogi ya Galilaya; Marko na Luka wanaeleza kuwa alikuwa anahubiri (Marko 1:39, Luka 4:44).
Hivyo, tunaweza kusema kuwa kuhubiri na kufundisha ni vitu viwili tofauti lakini vinafanana kwa namna fulani. Mtu mmoja anaweza kuwa mhubiri na mtu huyo huyo anaweza kuwa mfundishaji (mwalimu) pia. Hivyo ni muhimu kila mtu ajifunze namna nzuri ya kuhubiri na kufundisha.
Je, unapenda kujifunza zaidi kuhusu ustadi wa kuandaa na kuwasilisha mahubiri ?
Kama unataka kujifunza kuhusu namna ya kuandaa na kuwasilisha mahubiri yenye mvuto kwa hadhira, unaweza kujipatia kitabu kizuri kiitwacho Homilia kwa Walei: Ustadi wa Kuandaa na Kuwasilisha Mahubiri.
Kitabu hiki kimeandikwa kwa namna ambayo ni rahisi kueleweka kwa kila mtu kikimlenga hasa yule asiye na elimu ya Teolojia. Kitabu hiki kinawafaa watu wote wanaohubiri Neno la Mungu katika maeneo mbalimbali kama vile katika ibada ya kawaida kanisani, ibada maalum za kanisani kama vile ibada ya maombi katikati ya juma, mikutano ya uamsho na majuma ya maombi, mahubiri ya hadhara na matukio mengine ambapo mahubiri hutolewa.
Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na Email: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.
Je, unataka kupata mafunzo endelevu kuhusu mafaniko kwa mkristo?
Kama unataka kuendelea kujifunza kuhusu masuala mbalimbali juu ya mafanikio kwa mkristo unaweza kujiunga na mtandao huu ili uweze kupata makala mbalimbali. Kwa kufanya hivyo, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa katika mtandao huu.
Ili kujiunga, jaza fomu niliyoko hapa chini.
Nazidi kubarikiwa na masomo haya.