Rafiki yangu Mpendwa,
Kuna aina nyingi za uwekezaji ambazo watu wamekuwa wakizifanya. Baadhi ya aina hizo ni uwekezaji katika ardhi na majengo kwa kuwa na ardhi ya kukodisha na kujenga nyumba za kupangisha, kuweka fedha benki ili kupata riba, kuwekeza katika vipaji na talanta ulizo nazo kama vile utunzi na uimbaji wa nyimbo, michezo mbalimbali, uandishi wa vitabu na kadhalika.
Aina hizi za uwekezaji zimekuwepo kwa miaka mingi. Lakini leo nataka nikushirikishe aina ya kisasa ya uwekezaji. Aina hiyo ni uwekezaji katika masoko ya dhamana. Hii ni aina nzuri ya uwekezaji kwa mtu wa kisasa kama wewe. Ninaposema mtu wa kisasa, ninamaanisha mtu anayeishi leo bila kujali kama ni kijana au mtu mzima.
Ninaposema uwekezaji katika masoko ya dhamana ni uwekezaji wa kisasa simaanishi kuwa ni uwekezaji mpya duniani bali ni mpya hapa nchini Tanzania. Kwa kuwa huu ni uwekezaji mpya, bado haufamiki sana kwa wananchi walio wengi wakiwemo wasomi. Kwa kutofahamika kwa wananchi wengi, wawekezaji wa kigeni ndiyo wamekuwa wakinufaika zaidi na uwekezaji huu.
Masoko ya Dhamana ni nini?
Masoko ya dhamana ni masoko yenye kuhusisha dhamana zinazomilikiwa na wadau mbalimbali. Neno dhamana kama lilivyotumika hapa na kama linavyofafanuliwa katika Sheria namba 5 ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya mwaka 1994, linamaanisha bidhaa za kifedha. Bidhaa hizo ni kama vile hisa, hatifungani za muda mfupi na zile za muda mrefu, vipande katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja na bidhaa zingine za kifedha zilizotolewa au zinazokusudiwa kutolewa na serikali, kampuni, mashirika na taasisi zilizopo ndani na nje ya nchi na kutambuliwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana.
Masoko ya dhamana yamegawanyika katika sehemu kuu mbili: masoko ya mitaji na masoko ya fedha. Masoko ya mitaji ni masoko yanayohusisha dhamana za muda mrefu. Haya ni masoko ya dhamana zenye kuiva baada ya muda wa zaidi ya mwaka mmoja. Dhamana hizi ni pamoja na hisa, hatifungani na vipande vya mifuko ya uwekezaji wa pamoja. Kwa upande mwingine, masoko ya fedha yanahusika na dhamana za muda mfupi ambazo ni pungufu ya mwaka mmoja. Dhamana hizo ni pamoja na hatifungani za muda mfupi na amana za muda maalum za makampuni.
Uwekezaji katika Hisa
Kwa kuwa bidhaa za kifedha ni nyingi, leo naomba nijikite katika dhamana moja tu. Dhamana hiyo ni hisa. Pengine kitu cha kwanza kuelewa katika uwekezaji wa hisa ni maana ya hisa. Kwa kifupi, hisa ni sehemu ya umiliki wa kampuni. Hivyo hisa moja inawakilisha asilimia ndogo ya umiliki katika kampuni. Kwa mfano ukinunua hisa za benki ya NMB, maana yake unamiliki sehemu ya benki hiyo. Hali kadhalika, ukinunua hisa za kampuni ya Simu za mkononi Vodacom, unakuwa mmiliki wa sehemu ya kampuni hiyo.
Kiwango cha umiliki wa kampuni hutegemea idadi ya hisa unazomiliki. Kwa mfano, kama kampuni ina hisa 5,000,000 na wewe ukanunua 10,000, maana yake unamiliki asilimia 0.2 % ya kampuni hiyo (10,000 ni 0.2% ya 5,000,000). Watu hualikwa kununua hisa katika kipindi fulani ama wakati wa kuanzisha kampuni au pale kampuni inapotaka kujipanua kimtaji na hasa inapoingia katika soko la mitaji.
Zipo faida nyingi za kuwekeza katika hisa. Naomba nikushirikishe faida mbili tu kwa leo.
Faida ya kwanza ni gawio
Gawio (dividend) ni malipo yanayofanywa na kampuni kwa wanahisa kutokana na faida ya kampuni. Ukiwa mmiliki wa hisa utapata gawio ikiwa kampuni yenu itapata faida katika kipindi hicho cha mwaka na wanahisa wakaridhia kutolewa kwa gawio. Kwa kawaida, gawio hutolewa mara moja au mara mbili kwa mwaka kutegemeana na sera za kampuni na maamuzi ya wanahisa. Gawio linaweza kulipwa kutokana na faida ya mwaka husika au malimbikizo ya faida za nyuma. Gawio linaweza kulipwa kwa fedha taslimu au kwa kuwaongezea hisa wanahisa.
Kama mmiliki wa kampuni, una haki ya kushiriki katika kufanya maamuzi ya kampuni hiyo kupitia vikao vya wanahisa. Maamuzi hayo ni pamoja kiasi cha gawio. Mapendekezo ya gawio hutolewa na bodi ya wakurugenzi wa kampuni na kuidhinishwa na Mkutano Mkuu wa wanahisa. Mwenye hisa nyingi huwa na sauti au ushawishi mkubwa katika kufanya maamuzi na hupewa gawio kubwa maana gawio hutolewa kwa uwiano wa hisa za kila mwanahisa. Mwanahisa pia una haki ya kuuza hisa zako wakati wowote. Hata hivyo, kuwa mmilikiwa wa hisa hakumaanishi kuwa wewe ndiye mwendeshaji wa shughuli za kila siku za kampuni au haimanishi kwamba wewe ni sehemu ya uongozi wa kampuni. Kuwa mmiliki wa hisa hakukupi mamlaka ya kuingilia shughuli za watendaji wa kampuni.
Faida ya pili ni Ongezeko la thamani
Unapowekeza kwenye hisa, mitaji hukua baada ya muda fulani na kuongozeka thamani (capital gain). Hivyo, wanahisa huweza kupata faida itokanayo na ongezeko la thamani iwapo bei ya hisa itaongezeka kwenye soko la hisa. Ikiwa, kwa mfano, ulinunua hisa moja kwa shilingi 500, na baada ya mwaka hisa hizo sokoni zikauzwa kwa Shilingi 1,000 basi unakuwa umepata ongezeko la thamani ya shilingi 500 kwa kila hisa. Hii ni faida tofauti na gawio. Ikiwa utawekeza katika kampuni nzuri utapata gawio na ongezeko la thamani ndani ya mwaka mmoja. Hii ni tofauti na kuweka fedha benki kama amana maana fedha hiyo haiongezeki thamani. Ukiweka fedha benki kama amana, utapata fedha ile ile ulioiweka pamoja na riba lakini fedha yako haiwezi kuongezeka thamani. Kiuhalisia, kutokana na mfumuko wa bei, fedha uliyoweka benki inapungua thamani yake japo kiasi kinabaki kilekile.
Ungependa kujifunza zaidi kuhusu hisa?
Hapa nimekushirikisha faida mbili tu kati ya faida nyingi za uwekezaji katika hisa. Kama unapenda kujifunza zaidi kuhusu hisa zikiwemo faida za hisa na mambo mengine mengi, jiunge na mtandao huu ili uweze kupata makala mbalimbali kuhusu masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), maisha ya kikristo, malezi ya watoto na mengine mengi. Kwa kufanya hivyo, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa katika mtandao huu.
Kujiunga, jaza fomu hii hapa chini.
Nabarikiwa sana Mtumishi wa Bwana
Karibu sana. Endelea kufuatilia
Good work…. Keepnit up
You are welcome.
Thank you for sharing this information
You are welcome. Continue following up from this site.