Rafiki yangu mpendwa,
Katika makala yangu iliyopita, nilieleza vile namna ambavyo Mungu aliagiza “tule bata”. Katika makala hiyo nilieleza kuwa kula bata kunatafsiriwa kama kupumzika na kufurahia maisha. Kupitia biblia, Mungu ameelekeza tuwe na muda kupumzika vya kutosha kila siku na siku moja kwa kila juma. Leo nitakushirikisha kitu muhimu cha kuzingatia kabla ya “kula bata”
Kabla Mungu hajawaambia watu wale bata, aliagiza kwanza wafanye kazi. Kwa maneno mengine, si mpango wa Mungu “kula bata” bila kufanya kazi. Amri inatuagiza kupumzika. Maana yake kupumzika kufanya kazi. Sasa, kama hutafanya kazi kwa siku sita, je, siku ya saba utapumzika kutoka kwenye nini? Kwa bahati mbaya, watu wengi wanapenda “kula bata” kuliko kufanya kazi na wanafanya kazi kwa sababu tu hawana namna ya kuishi bila kufanya kazi. Na kama kungekuwa na uwezekano wa watu kupata mahitaji yetu bila kufanya kazi, na tukaambiwa kuchagua kati ya kazi na “kula bata”, bila shaka wengi wangechagua “kula bata”. Wala usimfikirie mtu mwingine, bali jiulize wewe mwenyewe, ungechagua nini? Kazi au “kula bata”? Hebu uwe mkweli, ungefanya kazi ili kupata nini? Hata kama hautasema wazi uchaguzi wako lakini ukweli ndo huo, watu wengi hawapendi kufanya hasa hasa zinazotumia nguvu , bali wanapenda “kula bata” tu.
Ukisoma Biblia utagundua kuwa kazi ndiyo njia iliyowekwa na Mungu ya kujipatia riziki. Biblia inatueleza kuwa baada ya Mungu kumuumba mwanadamu kwa mfano wake (Mwanzo 1:26-27), “Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza” (Mwanzo 2:15).
Je, kazi ni laana?
Baadhi ya watu, wakiwemo Wakristo, wana mtazamo kwamba kazi ni laana kwa kuwa ni adhabu ya Mungu kwetu baada ya wazazi wetu wa kwanza (Adamu na Hawa) kula tunda walilokatazwa. Mtazamo huu umepelekea watu hao wachukie kufanya kazi. Je, ni kweli kwamba kazi ni laana? Hebu tuichunguze kidogo Biblia kuhusu hili.
Fundisho la Biblia ni tofauti na dhana kwamba kazi ni matokeo ya dhambi na hivyo ni laana. Ni vizuri ieleweke kuwa, mwanadamu alipoanza ‘‘kula kwa jasho” (Mwanzo 3:17-19), haikuwa mwanzo wa kazi kama baadhi ya watu wanavyodhani. Kwa mujibu wa kitabu cha Mwanzo, Mungu anaelezwa kuwa ndiye muasisi wa kazi, maana ndiye wa kwanza kufanya kazi hapa duniani. Mungu alifanya kazi ya uumbaji kwa muda wa siku sita na siku ya saba akapumzika (Mwanzo 1:31, 2:1, 2). Kwa kuwa Mungu ni mwema, kazi nayo kwa asili ni njema maana Mungu hawezi kushiriki kufanya kitu kisicho chema. Vilevile, Mwanzo 1:31 inasema “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita”. Mungu alifanya tathmini ya kazi yake na kuiona ni njema sana na aliifurahia. Kwa mantiki hii, kazi inapaswa kuwa kitu cha kufurahia na siyo kitu cha kutukera au kutuudhi.
Kwa kuwa kazi ilianza kabla ya anguko, Adamu na Hawa walikuwa wanafanya kazi hata kabla ya kuanguka dhambini (Mwanzo 2:15). Ikiwa kazi ingekuwa laana au jambo ovu, Mungu asingeagiza wanadamu kufanya kazi.
Kazi baada ya anguko
Baada ya anguko la mwanadamu (Mwanzo 3) kulitokea mabadiliko katika kazi. Kama mwitikio wa dhambi ya Adamu na Hawa, Mungu alitoa matamko kadhaa dhidi yao. “Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi” (Mwanzo 3:17-19). Baada ya tamko hili la Mungu, kazi ikawa ngumu kuliko awali. Neno “kwa uchungu” lililotumika hapa, linaashiria changamoto, ugumu, uchovu na kuhangaika. Zaidi ya kazi kuwa nguvu, mwanadamu alianza kula mazao kutoka kondeni badala ya bustanini.
Pamoja na ukweli kwamba kazi si laana, lakini dhambi iliathiri utendaji wa kazi na kuifanya kazi ikawa ngumu zaidi. Kwa maneno mengine, baada ya anguko, kazi ilikuwa ngumu lakini muhimu zaidi kwa sababu ilibidi mwanadamu afanye kazi zaidi kuliko awali ili kupata mahitaji yake. Kwa sisi tunaoishi baada ya anguko yatupasa kufanya kazi zaidi na kwa bidii zaidi kuliko walivyofanya Adamu na Hawa.
Kazi katika mbingu mpya na nchi mpya
Katika Ufunuo 22:3 inaelezwa kuwa katika mbingu mpya na nchi mpya hakutakuwa na dhambi tena. Pamoja na kutokuwepo dhambi, nabii Isaya anaeleza kuwa kila atakayeingia katika nchi mpya na mbingu mpya atakuwa akifanya kazi na wote watafurahia kufanya kazi. Vilevile, hakuna mtu atakayefanya kazi kwa ajili ya mwingine. Hapa tena tunaona kuwa kazi haihusiani kabisa na laana maana kazi ilikuwepo Edeni kabla ya dhambi na itakuwepo mbinguni baada ya dhambi kukomeshwa.
Pamoja na kwamba mpango wa awali wa Mungu kuhusu kazi uliharibiwa na dhambi, ipo siku Mungu atarejesha hadhi ya kazi kama alivyokusudia ambapo hatutakula kwa jasho tena bali tutailima bustani na kuitunza katika mbingu mpya na nchi mpya. Kabla Mungu hajaturejeshea kazi ya kuilima na kuitunza bustani, mtazamo wetu kuhusu kazi unapaswa kuakisi mtazamo wa Yesu: “Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake” (Yohana 4: 34). Hivyo, kwa wasafiri wote wa kwenda mbinguni, yanapasa kufanya kazi kwa bidii maana ni baraka na wala siyo laana na ni njia aliyotupatia Mungu ya kujipatia mafanikio hapa duniani kabla hatujaenda kuishi maisha mazuri zaidi mbinguni. Kabla ya “kula bata” tufanye kazi, “tusile bata” bila kufanya kazi.
Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mpango wa Mungu kuhusu mafanikio yako? Basi jiunge na mtandao wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio kwa kubonyeza hapa; https://mkristomafanikio.co.tz/ Mtandao huu umeanzishwa kwa kusudi la kuwapatia maarifa ya msingi kuhusu masuala ya fedha, biashara, mahusiano (uchumba, ndoa na malezi ya watoto) na mambo ya kiroho. Katika mtandao huu utapata maarifa katika maeneo ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano, malezi ya watoto na mambo ya kiroho.