Mtu Makini Kama Wewe Hupaswi Kushiriki Michezo ya Bahati Nasibu

Rafiki yangu mpendwa,

Mimi siyo mfuatiliaji kabisa wa vyombo vya habari. Lakini siku ya leo nimejikuta nasikiliza matangazo ya kituo kimoja cha radio wakati napata chakula katika mgahawa fulani. Kila baada ya muda kulikuwa na matangazo ya biashara yanayohamasisha wasikilizaji kubeti ili kubashiri matokeo ya mechi za mashindano ya kombe la dunia yanayoendelea huko Qatar. Kila baada ya tangazo hilo, watangazaji wa kipindi hicho walikuwa wanaongezea maneno ya kuhamasisha watu kuchangamkia fursa hiyo ya kubeti ili watajirike.

Baada ya kuongea kwa muda mrefu, watangazaji hao waliruhusu wasikilizaji wao kupiga simu na kutuma meseji ili kuchangia maoni kuhusu mada iliyokuwa inajadiliwa katika kipindi hicho. Sikufuatilia sana mada ya mjadala huo ilikuwa inahusu nini, lakini nilivutiwa na maoni ya msikilizaji mmoja aliyewauliza watangazaji waliokuwa wanahamasisha watu kubeti kama wao wenyewe wamewahi kubeti na wakashinda. Watangazaji hao hawakujibu moja kwa moja bali walipiga maneno tu hali iliyoonesha kuwa ama hawajawahi kubeti au walibeti lakini hawakushinda.

Swali hili la msikilizaji na majibu ya watangazaji ni lazima yaibue tafakuri ya kina kwa mtu yeyote makini kama wewe unayesoma makala haya. Baadhi ya maswali ya kutafakari ni pamoja na haya yafuatayo:

Kwa nini watangazaji wanahamasisha watu kubeti lakini wao wenyewe hawajawahi kushinda?

Je, hawajawahi kushinda kwa sababu hawajawahi kushiriki?

Kama hawajawahi kushiriki, kwa nini wanahamsisha wengine?

Kama wamewahi kushiriki, kwa nini hawakushinda?

Kama hao wanaohamaisha hawajawahi kushiriki, au kama wamewahi kushiriki na hawakushinda, kwa nini mimi na wewe tubeti?

Mtu makini kama wewe, lazima utafakari maswali haya kwa kina. Hivyo, nakualika ufuatane nami katika makala haya ili tutafakari kwa pamoja kama kubeti na michezo mingine ya kubahatisha inafaa kwa mtu makini kama wewe.

Ukiacha kubeti, kumekuwa na ongezeko la michezo mingine ya kubahatisha na watu wengi wamekuwa wakishiriki michezo hiyo. Mifano ya michezo hiyo ni Kasino (Casino), bahati nasibu ya Taifa (national lottery) na bahati nasibu ya kutumia ujumbe mfupi wa simu (sms lottery).

Michezo hii imepata umaarufu kiasi kwamba watu wasiokua na elimu sahihi ya fedha wanaamini kuwa wanaweza kupata utajiri mkubwa kwa kutumia kiasi kidogo tu cha fedha kama vile Sh. 500.

Watu wanaoshiriki michezo hiyo hudai kuwa ni uwekezaji kama uwekezaji wa aina nyingine. Hata hivyo, kwa kuitazama kwa undani katika jicho la kibiblia na kimaadili, michezo ya kubahatisha haina sifa ya uwekezaji na haifai kwa wakristo na watu wengine wenye maadili mema na wanaojitambua kama wewe.

Kwa nini hupaswi kushiriki Michezo ya kubahatisha?

Zifuatazo ni baadhi ya sababu kwa nini michezo hii haifai ni kama ifuatavyo:

  1. Hakuna mifano ya waliofanikiwa kupitia michezo ya kubahatisha

Katika njia zote halali za kujipatia kipato, ipo mifano ya watu waliofanikiwa kupitia njia hizo. Lakini katika michezo ya kubahatisha hakuna mifano ya waliofanikiwa na kama ipo basi ni michache mno. Hapa naomba tusiandikie mate wakati wino upo. Ni watu wangapi unaowafahamu ambao wamewahi kucheza michezo ya kubahatisha na wakashinda? Hapa taja watu unaowafahamu wewe mwenyewe, siyo wale uliohadithiwa na mtu mwingine.  Bila shaka hakuna na kama wapo ni wachache mno. Kama wapo, je ni wangapi kati yao wana mafanikio ya kifedha ambayo yametokana moja kwa moja na kushinda michezo ya kubahatisha?

Ukweli ni kwamba ipo mifano michache mno ya waliowahi kushinda michezo ya kubahatisha, lakini ni ukweli pia kwamba kati ya hao, huenda hakuna hata mtu mmoja aliyepata mafanikio ya kifedha kama matokeo ya kushinda mchezo wa kubahatisha.

Watu wanaopata fedha nyingi kwa ghafla, hasa kama hawakuzifanyia kazi, huwa hazikai. Hii ni kwa sababu ya kukosa elimu sahihi ya usimamizi wa fedha. Hali hii ndiyo huwakuta wanaoshinda michezo ya kubahatisha. Sasa, kama hakuna mifano ya watu waliofanikiwa kimaisha kupitia michezo ya kubahatisha, kwa nini wewe uhangaike nayo?

2. Michezo ya kubahatisha haiendani na mpango wa Mungu wa kujipatia riziki

Kwa mujibu wa Biblia, kazi ndiyo mpango wa Mungu wa kujipatia kipato na mahitaji yetu tangu katika bustani ya Edeni hadi leo. Michezo ya kubahatisha haihusishi kazi kwa mchezaji. Mungu amepanga kupitishia baraka zake za mafanikio kupitia katika kazi na siyo michezo ya kubahatisha kama Biblia inavyosema “Atakufunulia Bwana hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe (Kumbukumbu la Torati 28:12).

Ni kanuni ilivyo wazi kuwa kadiri unavyoongeza juhudi katika kazi, ndivyo unavyoweza kuongeza kipato chako. Kwa mfano, kama unafanya biashara, ukiongeza ubora wa kile unachofanya, ukifungua matawi zaidi na kuwafikia wateja wengi zaidi unaweza kuongeza kipato chako. Hali kadhalika, kama wewe ni mwajiriwa, ukifanya kazi kwa juhudi na weledi zaidi kazini kwako, unaweza ukapandishwa cheo na hivyo kuongezewa mshahara. Kwa kuwa michezo ya kubahatisha haihusishi kazi, hakuna namna utaweza kuweka juhudi ili uweze kujihakikishia ushindi. Wewe kazi yako ni kucheza tu kwa kuzingatia vigezo na masharti na kisha unasubiri bahati tu.

3. Mungu amekemea tamaa ya  utajiri  wa haraka haraka

Katika Mithali 28:20, Biblia inasema “Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele; lakini afanyaye haraka kuwa tajiri hakosi ataadhibiwa”. Katika fungu hili, tunaelekezwa kuwa waaminifu. Kuwa mwaminifu ni kuishi na kutenda kama Mungu anavyotaka ikiwa ni pamoja na kusimamia fedha kama Mungu anavyotaka.

Fungu hili pia linaelekeza kutokuwa na tamaa ya utajiri wa haraka. Kwa kifupi, tunaelekezwa kutokutumia njia zozote zinazoonekana kutupatia utajiri wa haraka haraka. Mifano ya kutafuta utajiri wa haraka haraka ni pamoja na kucheza michezo ya kubahatisha, upatu na biashara  yoyote haramu.

Uwezekaji unahitaji muda na ukitaka utajiri wa haraka haraka unaweza ukaishia kupoteza. Katika Mithali 28:20, tunaelezwa kuwa tukiwa na tamaa ya kupata utajiri wa haraka hatutakosa kuadhibiwa.

Hapa anayeadhibu siyo Mungu, bali matokeo mabaya ya kutaka utajiri wa haraka haraka ndiyo yanayomuadhibu mtu. Kwa mfano, kutokana na tamaa ya fedha za haraka haraka mtu anaweza kufanya uwekezaji usio makini na matokeo yake akapoteza fedha kirahisi na kujikuta akiwa na maisha magumu. Kwa maisha hayo atakuwa ameadhibiwa.

Fungu jingine linalotoa mwongozo katika uwekezaji ni Mithali 13:11 ambalo linasema “Mali iliyopatikana kwa haraka haraka itapunguka; bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa”. Ni jambo lililo wazi kuwa mali iliyopatikana kwa haraka haraka bila shaka haihitaji jitihada kuipata na hivyo mtu anakuwa hana uchungu nayo na anaweza akaitapanya ovyo ovyo na ikaisha haraka.

Lakini, mali iliyopatikana taratibu bila shaka inahusisha bidii fulani na hivyo mtu anakuwa na uchungu nayo na ataitumia kwa uangalifu na atapenda aizalishe zaidi ili iongezeke.

 Fundisho tunalolipata hapa ni kwamba Mungu hapendi tuhangaike na uwekezaji utakaotuingizia utajiri wa haraka haraka maana una hatari zake. Kwa mantiki hiyo, Wakristo hatupaswi kushiriki katika michezo ya kubahatisha.

4.  Michezo ya kubahatisha inahusisha ubinafsi

Ili uweze kushinda katika michezo ya kubahatisha ni lazima wengine washindwe. Kwa maneno mengine, unaposhinda kwenye michezo ya kubahatisha, unachukua fedha walizopoteza wengine.  Lakini neno la Mungu linatuambia “Mtu asitafute faida yake mwenyewe, bali ya wenzake” (1 Wakorintho 10:24). Vilevile, Amri ya kumi inasema “Usitamani…. Chochote alicho nacho jirani yako” (Kutoka 20:17).

 Mchezaji wa michezo ya kubahatisha anapoazimia kushinda pesa, kihalisi anatumaini kwamba wengine watapoteza pesa zao ili yeye afaidike. Hii ni roho ya ubinafsi wa hali ya juu.

Hizi ndizo baadhi ya sababu kwa nini michezo ya kubahatisha haifai kabisa kwa Wakristo na hata wasio Wakristo. Hivyo, mtu yeyote anayetaka mafanikio ya kifedha asijaribu kucheza michezo hii maana itampotezea muda na fedha. Hata kama michezo hii inakubalika kisheria katika nchi nyingi, haiwezi kuwa sababu ya wewe kushiriki katika michezo hiyo. Kaa mbali nayo kabisa. Tafuta fedha kwa kufanya kazi. Hiyo ndiyo sahihi na uhakika ya kupata mafanikio ya kifedha.

Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mada hii

Ili uachane na michezo ya kubahatisha, unahitaji kupata elimu zaidi kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji. Njia moja wapo ya kujipatia elimu hiyo ni kusoma vitabu vizuri kuhusu Mafanikio ya Kifedha. Mojawapo ya vitabu hivyo ni kitabu kuhusu Mafanikio ya kifedha katika Ndoa na Familia. Kupata maelezo zaidi kuhusu kitabu hiki, bonyeza hapa.

Je, unapenda kupata masomo endelevu kuhusu mafanikio?

Kama unapenda kupata masomo endelevu kuhusu fedha na masuala mengine ya mafanikio kwa muktadha wa kikristo, unaweza kujiunga na mtandao wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio.  Katika mtandao huu utapata maarifa mazuri katika maeneo ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), malezi ya watoto na mambo mengine mengi.

Kujiunga na mtandao huu jaza fomu hii hapa chini.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *