Je, Unajua Kuna Aina Ngapi za Mahubiri?

Kama wewe ni mfuatiliaji mzuri wa mhaubiri, bila shaka ulishagundua kuwa zipo aina nyingi za mahubiri ya kutegemeana na aina ya tukio au ibada, aina ya hadhira, aina ya mhubiri na kadhalika. Vilevile, aina ya mahubiri, yanaweza kutofautiana kulingana na namna unavyoamua kuyaainisha.

Katika makala hii, naenda kukushirikisha ina kuu tano za mahubiri. Mhubiri anaweza kuamua kutumia aina hizo kwa kadri anavyoona inafaa.

Aina kuu tano za mahubiri ni kama ifuatavyo :

Mahubiri ya fungu moja au mawili

Mahubiri ya fungu moja ni aina ya mahubiri ambayo hujengwa juu ya fungu moja au mawil tu. Huhusisha kuchunguza, kuyachambua na kugundua kweli zote zilizomo ndani ya fungu au mafungu husika na kuziwasilisha kwa hadhira kwa mtindo rahisi na wenye kueleweka.

Udhaifu wa aina hii ya mahubiri ni uwezekano wa kutokuwa ya kibiblia. Ninaposema mahubiri ya kibiblia ninamaanisha mahubiri yaliyojengwa juu ya biblia. Kuna hatari kwa mhubiri kutumia fungu la Biblia kama ngazi ya kupandia kuelekea kwenye mawazo yake mwenyewe maana inaweza kuwa kazi ngumu kutumia fungu moja au mawili tu na kuhubiri kwa muda mrefu huku ukisalia kwenye maudhui ya fungu au mafungu hayo.

Mahubiri ya kufafanua

Hii ni aina ya mahubiri yanayotokana na mafungu matatu au zaidi. Hubiri hili linaweza kuhusisha aya nzima, sura nzima au kitabu kizima. Kwa mfano, unaweza kuamua kuhubiri kwa kutumia kitabu cha Isaya, kuanzia sura ya kwanza hadi ya mwisho, ukielezea mafundisho yaliyomo, fungu kwa fungu au sura kwa sura mpaka unamaliza kitabu chote.

Udhaifu wa aina hii ya hubiri unaweza kuwa ni msisitizo katika ufafanuzi badala ya kusisitiza matumizi maishani. Unapohubiri aina hii ya hubiri ni vizuri ukakumbuka kuwa sehemu muhimu ya hubiri ni matumizi ya hubiri maishani na siyo ufafanuzi wa maandiko.  Mahubiri ya aina hii yanahitaji muda mrefu kujiandaa hivyo yanaweza yasitumike sana kwa mtu ambaye hana muda wa kutosha kujiandaa.

Mahubiri ya kufafanua yanaweza kuwa ya kibiblia zaidi kwa kuwa mhubiri huwa anajikita katika muktadha wa aya, sura na kitabu chote kwa ujumla. Hivyo, kiini cha maandiko ndicho ambacho hubeba mahubiri yake yote. Mahubiri yanapokuwa ya kibiblia, waumini nao huimarika na huwa na ufahamu mzuri na wa kina wa Neno la Mungu na matumizi yake maishani.

Mahubiri ya mada

Mahubiri  ya mada yanatokana na mafundisho makuu ya imani, fundisho moja au kundi la mafundisho kadhaa ya imani.  Mhubiri hutumia mafungu mbalimbali ya maandiko yanayohusu mada au fundisho husika ili kuthibitisha fundisho hilo au mada hiyo.

Mifano ya mafundisho ni pamoja na Uungu ya Yesu, ubatizo, uumbaji, Roho Mtakatifu na kuja kwa Yesu mara ya pili. Mhubiri huchagua somo fulani kisha huchunguza kila kitu ambacho Biblia inasema juu ya somo hilo.

Mahubiri ya matukio maalum ni mfano mwingine wa mahubiri ya mada. Mahubiri haya yanatokana na msukumo wa matukio maalumu uliyoalikwa, uliyopanga au uliyopangwa kuhudumu.

Mifano ya matukio maalum ni ibada ya ndoa, msiba, kuweka nyumba wakfu, kuweka wakfu viongozi wa kanisa, sherehe za kuagana, tukio la uchangiaji wa ujenzi wa kanisa, kubariki watoto na sherehe mbalimbali kama vile sherehe ya kumbukumbu ya kuzaliwa, ubatizo, meza ya Bwana na mahafali. Mada ya mahubiri haya na mafungu utakayotumia vinapaswa viendane na tukio husika.

Mahubiri juu ya maisha ya mashujaa wa Biblia

Mahubiri haya yana lengo la kutumia maisha na matendo ya watu waliosimuliwa ndani ya Biblia ili kuwatia nguvu hadhira kwamba hata wao wanaweza pia kuwa mashujaa wa imani.

 Mifano ya mashujaa wa Biblia ni pamoja na Musa, Yona, Abrahamu, Gideoni, Daudi, Paulo, Yusufu na Nuhu. Si mashujaa wote wa Biblia waliishi maisha yanayompendeza Mungu wakati wote. Kuna wakati walianguka na kuinuka. Kwa kusimulia kuinuka na kuanguka kwao kunadhihirisha kuwa hata mashujaa wakubwa wa imani walikuwa na mapungufu yao kama sisi nasi tulivyo na mapungufu.

Mahubiri ya aina hii yanatufanya tujue kwamba wao si tofauti na sisi na kwa visa vyao tunatiwa moyo kwamba pamoja na mapungufu yetu bado tunaweza kuokolewa kama tutaendelea kumwamini Yesu na hivyo kupokea neema yake. Mahubiri haya pia hutukumbusha kuwa katika visa vyote vya historia kuna mtu mmoja tu mkamilifu ambaye ni Yesu Kristo.

Mahubiri mchanganyiko

Ni aina ya mahubiri ambayo ni mchanganyiko wa aina zote zilizoelezwa hapo juu. Kwa mfano, hubiri moja linaweza kuwa na sehemu ya kufafanua, mada na mashujaa wa biblia.

Hizi ndizo aina kuu za mahubiri ambazo kila mhubiri anapaswa kuzifahamu. Kama wewe ni mhubiri wa mara kwa mara, itapendeza kama utakuwa unabadilisha aina ya mahubiri ili kuleta mvuto na ‘ladha’ tofauti kwa hadhira yako. Ili uweze kufanya hivyo, unapaswa kuelewa aina mbalimbali za mahubiri.

Je, Ungependa Kujifunza Zaidi Kuhusu Mada hii?

Kama unataka kujifunza kwa kina kuhusu mada hii na mambo mengijen kuhusu namna ya kuandaa na kuwasilisha mahubiri yenye mvuto kwa hadhira, unaweza kujipatia kitabu kizuri kiitwacho Homilia kwa Walei: Ustadi wa Kuandaa na Kuwasilisha Mahubiri.

Kitabu hiki kimeandikwa kwa namna ambayo ni rahisi kueleweka kwa kila mtu kikimlenga hasa yule asiye na elimu ya Teolojia. Kitabu hiki kinawafaa watu wote wanaohubiri Neno la Mungu katika maeneo mbalimbali kama vile katika ibada ya kawaida kanisani, ibada maalum za kanisani kama vile ibada ya maombi katikati ya juma, mikutano ya uamsho na majuma ya maombi, mahubiri ya hadhara na matukio mengine ambapo mahubiri hutolewa.

Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na Email: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

Je, unataka kupata mafunzo endelevu kuhusu mafaniko kwa mkristo?

Kama unataka kuendelea kujifunza kuhusu masuala mbalimbali juu ya mafanikio kwa mkristo unaweza kujiunga na mtandao huu ili uweze kupata makala mbalimbali. Kwa kufanya hivyo, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa katika mtandao huu.

Ili kujiunga, jaza fomu niliyoko hapa chini.

About Devotha Shimbe

Devotha Shimbe ni Mwalimu na mwanasaikolojia. Amepata pia mafunzo ya Theolojia. Devotha amejitoa kumtumikia Mungu katika maisha yake yote na amekuwa akifundisha na kutoa semina mbalimbali kuhusu mahusiano na maisha ya kiroho kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *