Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Tafiti zinaonesha kwamba mawasiliano ni mojawapo ya mambo yanayooongoza katika kusababisha migogoro ya ndoa na kusababisha kukosekana kwa amani katika ndoa na familia na hatimaye kuvunjika kwa ndoa. Tatzio mojawapo linalochangia kukosekana kwa mawasilinao mazuri katika ndoa ni mwanandoa mmoja au wote kuwa wasikilizaji wabovu.
Huenda wewe ni mmojawapo wa watu ambao ni wasikilizaji wabovu lakini hujuia kwamba wewe ni msikilizaji mbovu. Katika makala haya, tunaenda kuangalia aina mbalimbali za wasikilizaji wabovu ili kama wewe ni mmojawapo uweze kujifahamu na kuchukua hatua za kurekebisha hali hiyo ili uweze kunusuru ndoa yako.
Aina za wasikilizaji wabovu
Kuna aina tano za wasikilizaji wabovu, ambao ni kama ifuatavyo
- Msikilizaji mchovu. Huyu alishasikia yote tangu zamani. Huiweka akili yake katika hali ya kutohitaji kuongeza kitu tena, hata akitakiwa kutoa mawazo hana cha kuongeza.
- Msikilizaji mwenye kuchagua. Huyu huchagua kusikiliza mambo yanayomvutia tu na kuacha mengine. Wengi wao, hawapendi kusikiliza mambo yaliyo kinyume na mtazamo wao, wasiyokubaliana nayo na yanayowaudhi. Ni dhahiri kuwa hatuwezi kufanya maamuzi sahihi ikiwa tutasikiliza baadhi tu ya mambo. Tunahitaji kupata ukweli wote na uhalisia wa mambo ili kufanya uamuzi sahihi
- Msikilizaji mwenye kujilinda. Huyu hubadilisha maneno yote yaliyosemwa kuwa mashambulizi kwake binafsi. Kila lisemwalo ni kwa ajili yake na hapendi kusahihishwa kwa hali iwayo yote. Hata kama hoja ni ya jumla kwa watu wote, yeye huitazama kama inayomlenga yeye binafsi.
- Msikilizaji mkatizaji. Huyu hutumia muda mwingi kutafuta jibu na siyo kusikiliza kile kinachozungumzwa. Huvutiwa na mawazao yake tu. Mara zote husubiri kupata upenyo wa kukatiza mazungumzo ili kuchomeka mawazo yake katikati ya mazungumzo. Utamsikia akisema, “Hilo ni dogo, nisikilize mimi kilichonitokea juzi… au bora wewe, mimi zaidi…” Aina hii ya usikilizaji huondoa motisha kwa mzungumzaji na badala yake humwachia yeye kueleza yote ha hivyo kuvunja mawasiliano.
- Msikilizaji asiye na hisia. Huyu hawezi kusoma hisia katika maneno yanayotumika katika mazungumzo. Hili ni tatizo kwa wanaume walio wengi ambao hushindwa kuelewa hisia zinazowakilishwa na maneno yanayosemwa na wanawake. Kwa mfano, mke anapoomba kusindikizwa sokoni, anaweza asimaanishe kupelekwa. Hii ni lugha ya kutaka kujua ikiwa kweli unampenda na kumjali. Jibu la “sina nafasi sasa, nahitajika kazini au kwani leo kuna nini hadi uombe kupelekwa….,” huleta maumivu kihisia kuliko kusema. Badala yake , jibu kumbe ungeweza kutoa jibu kama vile: “oh, pole rafiki. Natambua wewe ni mama mwema na umekuwa unapambana siku zote kwenda sokoni pamoja na uwingi wa kazi ulizo nazo. Kukupa furaha ndiyo tamanio langu siku zote. Natamani sana nikusindikize. Lakini sasa hivi nina kazi hii hapa ( aione au kuilewa) na inahitajika leo, natamani iishe ili tufurahi pamoja. Naomba tushauriane cha kufanya”. Kwa maneno haya mwanamke mwenye akili hawezi kukasirika wala kuleta lawama.
Ufanye nini kama wewe ni msikilizaji mbovu ?
Kama wewe ni msikilizaji mbovu na unatamani kuacha hali hiyo, unaweza kufanya yafuatayo:
- Zingatia kanuni muhimu za kuwa msikilizaji bora ili kuleta amani katika mahusiano. Kanuni hizi ni pamoja na:
- kumtazama mzungumzaji kwa makini, kukaa mkao wa kusikiliza, kuonyesha ishara za kuvutiwa na mazungumzo, kuuliza maswahi kwa usahihi na ujitahidi kusikiliza zaidi kuliko kusema.
- Tatua matatizo kwa haraka na kwa kutumia njia za kujenga ili kuboresha mawasiliano. Chagua muda muafaka na mahali sahihi, kuwa wazi, baki kwenye mada, onesha heshima, weka orodha ya njia za kusuluhisha tatizo, chagua njia sahihi na ufanyie kazi makubaliano yaliyofikiwa.
- Zingatia kanuni muhimu za mzungumzaji bora ili kuleta tumaini katika mawasiliano. Chagua muda muafaka wa kuwasiliana na mwenzi wako, tumia sauti nzuri yenye amani , sema kwa usahihi kile unachokusudia, jenga mtazamo chanya katika mazungumzo, jiandae kuheshimu mawazo ya mwenzi wako, jali hisia za mwenzi wako na mahitaji yake, na jenga mazingira ya kuwa na mazungumzo ya pamoja mara kwa mara. Kutozungumza mara kwa mara na kila mmoja kuwa na ratiba yake kunavuruga mnyororo wa mawasiliano.
Pamoja na kuzingatia ushauri huo hapo juu, ni muhimu nsana kuzingatia ushauri wa neno la Mungu usemao “Hayo mnayajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika; kwa maana hasira ya nwanadamu haitendi haki ya Mungu” (Yakobo 1: 19 – 20). Vilevile yakupasa kumfanya Mungu kuwa kimbilio na ngome nyakati zote ili kuwa na yeye atakuwezesha kuwa na mawasiliano sahihi katika ndoa.Kumbuka …kwa maana hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu (Yakobo 1:20).
Je, ungependa kujifunza zaidi kuhusu mada hii?
Kama unataka kuendelea kujifunza zaidi kuhusu mada hii, unaweza kujiunga na mtandao huu wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio ili uweze kupata makala mbalimbali zitakazokusaidia kuboresha mahusiano yako iwe mahusiano ya ndoa au uchumba au mahusiano mengine katika familia, maeneo ya kazi na katika jamii kwa ujumla.
Zaidi ya kujifunza kuhusu mahusiano, utapata pia makala juu ya masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, maisha ya kikristo, malezi ya watoto na mengine mengi. Kwa juinga na mtandao huu, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa. Ili kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini